Ingia

Karibu Tena, Rafiki. Ingia kuanza kusoma vitabu

JISAJILI

Ukimaliza kujisajili hapa, lipia riwaya kwa M-pesa!

Kurudisha Neno la siri

Fortgot your password? Don't worry we can deal with it

SOMA BURE - PATAPOTEA


Taarifa ziliponifikia kwanza nilizipuuzia. Niliendelea na shughuli zangu kwani niliziona kuwa ni taarifa za ajabu na zisizo na msingi wowote. Lakini ziliponifikia mara ya pili zilinifikirisha sana. Zilishangaza, haswa nikiwa kama mwandishi wa vitabu ambaye niliambiwa kuwa Mwendawazimu alikuwa ameng’ang’ania kitabu nilichoandika. Ikafanya nibaki najiuliza maswali mengi kichwani.
Kichaa, au kajifanya kichaa?
Mwendawazimu kang’ang’ania kitabu changu cha riwaya.
Kitabu nilichoandika kwa mkono wangu; iweje
Mwendawazimu aking’ang’anie?
Amependa nini kwenye kitabu changu kiasi kwamba
amekuwa tayari kufa kuliko kupoteza hicho kitabu?

Nilijiuliza maswali mengi sana. Nikabaki na mshangao hasa baada ya kuambiwa kuwa watu wa mamlaka ya mji wa Kigoma walifika kumwondoa Mwendawazimu huyo eneo alilokuwa akiishi, kufuatia wakazi wa eneo hilo kulalamika kwenye mamlaka husika kuwa alikuwa akiwafanyia fujo na wakati mwingine kuhatarisha amani ya mtaa. Zoezi la kumwondoa Mwendawazimu huyo liliambatana na kuchoma moto banda lake la nyasi alilokuwa akilitumia kama makazi yake. Ni wakati wanachoma banda la Mwendawazimu huyo ndipo lilipotukia lile tukio ambalo liliwashangaza wengi na sasa limevuta hisia zangu na kuona kuwa taarifa hizi ni za ajabu. Unaambiwa Mwendawazimu alipoona banda lake linawaka moto, yeye alikimbilia ndani ya banda lililokuwa likiteketea kwa moto. Wakati watu wakiwa wanapiga kelele kuwa huenda aliamua afie ndani ya banda lake, mara yule mwendawazimu alitoka huku akiwa anakohoa. Mshangao uliwashika sana pale alipotoka akiwa ameshikilia kitabu kiitwacho SAA 72. Kitabu ambacho mwandishi wake ni mimi. Huku akikohoa, alikuwa akikifuta na kukipuliza kitabu kile kwa namna ya kukisafisha. Alifanya hivyo kwa mahaba makubwa kwa kitabu kile huku. Sasa watu wakabaki wanajiuliza, kwa nini mwendawazimu huyo alikuwa tayari kuhatarisha maisha yake ili mradi tu aokoe kile kitabu.
Kina nini kitabu hicho?
Kitabu kinapendwa na mwendawazimu?
Ama kweli, jambo hili liliwashangaza wengi.
Si wao tu, hata mimi mwandishi wa hicho kitabu nilishangazwa na kitendo cha mwendawazimu kuwa na mahaba na kitabu changu.
Sikuichukulia kama taarifa ya kawaida tu. Kichaa kuwa tayari kufa kuliko kukipoteza kitabu cha riwaya nilichokiandika, ilikuwa habari ya kusisimua.
Ghafla nikajikuta ninaingiwa na kiu.
Kiu ya kutaka kuongea na kichaa huyo, ili ikiwezekana nijue nini kimemvutia kwenye kitabu changu.
Kama mwandishi wa kitabu SAA 72, ningejisikia fahari kama mtu maarufu angejitokeza hadharani na kusifia kitabu changu. Lakini, kitabu changu kuuteka moyo wa mwendawazimu ilichochea udadisi wa juu sana ndani ya akili yangu.
Nilikuwa likizo. Halafu, Kigoma siyo mbali labda nitasafiri kwa siku nyingi. Nilifikiri nikaona, kwa nini nisiende, nifanye kama sehemu ya matembezi wakati wa hii likizo yangu?
Hivyo nikawa tayari kusafiri. Safari ndefu toka Arusha hadi Kigoma kuonana na Mwendawazimu huyo.
Nilifanya maandalizi ya haraka.
Safari ya kuelekea Kigoma kuonana na mwendawazimu ilianza siku ya Alhamisi asubuhi.
Nikiwa ndani ya basi liitwalo KIAZI KITAMU, safari yangu ya kutoka Arusha kwenda Kigoma ilianza asubuhi ya saa 12. Kichwani nikiwa na maswali mengi kuhusiana na mwendawazimu mwenye mahaba na kitabu changu cha riwaya. Miongoni mwa maswali hayo ilikuwa ni, alikipata wapi hicho kitabu?
Alinunua?
Aliokota?
Alipewa?
Alimkwapua mtu?
Au?
Je, ataweza kunitambua mimi kama mwandishi wa kitabu pindi nikijitambulisha kwake?
Je, nini kimemvutia kwenye hicho kitabu hadi kikamfanya aingie kwenye banda linalowaka moto ili tu akisalimishe kitabu kisiteketezwe kwa moto? Huyu kichaa anaweza kunipa historia ya maisha yake?
Hayo pamoja na maswali mengine yalifumuka kwa wingi kichwani mwangu. Vipi kama amekichukia?
Maana kuking’ang’ania haimaanishi amekipenda. Sikuwa na majibu, nisigeweza kujijibu hadi hapo nitakapoonana naye ana kwa ana!
Subira ilihitajika hadi nifike Kigoma, mwendawazimu alikuwa na majibu yote.
Nilijiegemeza kwenye kiti na kumwachia dereva wa basi hilo afanye kazi yake. Nikasinzia ule usingizi wa safarini!

Safari yetu haikuwa na shida njiani. Tuliwasili Kigoma majira ya saa saba na robo usiku. Ilikuwa safari yenye kuchosha sana. Hakuna kitu nilichohitaji wakati huo zaidi ya kitanda kizuri nilale. Haikuwa mara yangu ya kwanza kufika Kigoma, nilikuwa najua baadhi ya hoteli nzuri.
“Nipeleke Nzimano Hotel,” nilimwambia dereva teksi.
“Shilingi elfu thelathini!” Dereva teksi alijibu hali iliyofanya harufu mbaya itoke kinywani mwake.
“Pole sana, ulikuwa umelala nini?” Nilimwuliza.
“Eeh bwana wacha!” Alisema kwa sauti ya masikitiko.
Lakini hakuwa amejibu swali langu, ila nilimuelewa kwa vile nikiwa Mtanzania, naelewa jinsi ambavyo tunajibu maswali.
“Naweza kuelewa, mabasi haya yanawasili usiku sana!” Nilisema tena.
“Tutafanyaje sasa na ndiyo yenye faida maana mtu hawezi tembea kwa mguu muda huu wala hakuna daladala!” Alisema yule dereva teksi. Akaongeza mwendo wa gari.
Dakika ishirini baadae, tulikuwa tumefika Nzimano Hoteli. Dereva aliendesha taratibu akiwa anatafuta sehemu ya kuegesha gari kwenye sehemu ya kuegeshea magari ya Nzimano Hotel. Wakati huo, nikipekenyua noti za shilingi elfu kumikumi tayari kwa ajili ya kumlipa yule dereva. Niliteremka na kuvuta begi langu dogo. Nikalitupia mgongoni kwa kulivaa.
“Asante!” Dereva alisema wakati alipokuwa akipokea hela ya nauli. Sikusema kitu badala yake nikaanza kupiga hatua kuelekea ndani ya hoteli.
Niliweza kuuhisi uchovu wakati nilipokuwa natembea.
Mji ulikuwa kimya kabisa. Eneo la hoteli nalo lilikuwa kimya kabisa. Nilipofika mapokezi msichana wa mapokezi alinipokea huku macho yake yakijitahidi kushindana na usingizi.

* * *

Niliamka majira ya saa tatu asubuhi. Baada ya usafi na kifungua kinywa, hatimaye ukawadia wakati ambao niliona unafaa niingie mtaani.
Lengo likiwa moja tu, kumsaka!
Kumsaka yule mwendawazimu.
Huwa napenda kusikiliza ushauri wa rafiki zangu. Wachache nilioongea nao juu ya mkasa huu na lengo la safari yangu walinishauri nibebe nakala ya kitabu cha SAA 72. Nilibeba. Pia, niliona ni vema nikabeba na shajara yangu kwa ajili ya kuandikia matukio ya siku. Vilevile, nilichukua kamera yangu ambayo hupenda kusafiri nayo.
Nje ya Nzimano Hoteli kuna teksi ambazo zimeegeshwa kwa idhini ya wamiliki wa hoteli ili kuhudumia wateja ambao hawakupenda kutumia usafiri wa hoteli. Hivyo nilikwenda hadi kwenye teksi hizo. Nilipofika eneo ambalo teksi zilikuwa zimeegeshwa, madereva walianza kunishawishi, kila dereva akitaka nitumie usafiri wake. Nilitembea taratibu hadi nilipomwona dereva mmoja mzee aliyekuwa amevaa kofia. Kwa sababu ambazo nitakuambia baadaye niliamua kuchukua gari lake.
“Nipeleke Soko la Mwanga!” Nilimwambia baada ya kuwa nimesalimiana naye.
“Ha! Ha! Ha!, Sawa mkuu wangu!” Mzee alisema huku akicheka.
“Mbona wacheka mzee wangu?” Nilimuuliza huku nikimtazama. Meno yake yalikuwa na weusi na kwenye mashina yake kulionekana utando wa njano.
“Vijana hawa, tunawaambia wafanye sala ili wabarikiwe hawataki kufanya sala. Sasa si unaona kila pahali sasa tunawazidi, hapo inawauma umechagua teksi yangu!” Alisema yule mzee kwa furaha huku akiwa anatoka eneo la hoteli.
“Ha! Ha! Ha! Mengine yapi hayo mnayotuzidi?” Niliuliza kwa sauti ya kirafiki.
“Ha! Ha! Ha! Wewe hujui siku hizi watoto wa kike wanatupenda siye wazee?! Alisema yule mzee.
Kauli hiyo ilinifanya nishangae kidogo ila nilijitahidi kuficha mshangao wangu. Nikaanza kumwangalia juu hadi chini huku nikijitia kucheka.
“Mzee bwana, unataka kusema sala hiyohiyo inakusaidia kupata watoto wa kike?” Nilisema huku nikicheka.
“Ha! Ha! Ha! Wewe unaitwa nani kijana wangu, samahani sana lakini maana si maadili ya kazi kuwauliza wateja maswali mengi.” Alisema mzee badala ya kujibu swali.
“Naitwa Japhet Sudi.” Nilijibu.
“Heeeh, Japhet yupi, isije kuwa yule mwandishi wa vitabu!” Mzee alisema huku akiniangalia kwa kutumia kioo kilicho kwenye paa la gari.
“Ndiye! Wewe ni msomaji wa vitabu?” Nilijibu na kuuliza swali.
“Duuuh, sikuwa nasoma sana vitabu vya riwaya. Mimi hupenda kusoma vitabu vya dini lakini kuna rafiki yangu mmoja alinishawishi sana kusoma kitabu chako cha SAA 72, kikanivutia sana.” Alisema yule Mzee huku akipunguza mwendo wa gari. Hii ilikuwa ishara kuwa hakutaka tufike haraka kwenye soko la Mwanga, sehemu niliyoambiwa kuwa yule mwendawazimu alikuwa amehamishia makazi yake baada ya kufukuzwa eneo la Mbilizi.
“Unaitwa nani Mzee?” Nilimuuliza.
“Khamis Kavula, wenyewe hupenda kuniita mzee KK kiboko ya warembo!” Alisema yule mzee halafu akaongeza, “Hivi huyo Jacob Matata ni mtu halisi au ni simulizi tu?”
“Ha! Ha! Ha! Umeona unavyofanana naye eeenh?” Badala ya kujibu swali lake niliuliza swali.
“Sana, maana kama ni mtu halisi yule ndiye pekee anaweza nizidi linapokuja suala la watoto warembo!” Alisema yule Mzee huku akionekana kufurahia sana maongezi yetu.
“Yule jamaa kweli yupo, ni rafiki yangu sana. Nadhani huwa ana dawa ya warembo.” Nilisema huku nikimwangalia.
“Si kweli, sema anajua nini wanataka na ameshajua udhaifu wao. Na sasa najibu swali lako, unajua sala inasaidia kuleta mvuto kwa watoto wa kike. Mwanamke anapenda mwanaume mtulivu kwa nje ila hatari akiwa chumbani. Kamwe mwanamke hapendi mwanume mwenye tabia za kike; maneno mengi, ulegevulegevu na vitendo vya kike. Mtu akiwa mcha Mungu anakuwa mtulivu sana na hatumii nguvu zake ovyo ovyo. Unanielewa?”
“Mmmmh! Sasa mbona Jacob si mcha Mungu?” Nilisema kwa kusaili.
“Basi ujue ana tabia za kiume ambazo nimesema!” Alisema Mzee KK.
“Nini kilikuvutia kwenye riwaya ya SAA 72?”
“Mambo mengi. Umekuja kikazi, kuandika riwaya nyingine au kutembea tu?” Aliniuliza huku akionekana kupuuzia swali langu.
“Vyote tu!” Nami niliamua nimjibu jumlajumla kama yeye alivyofanya.
“Au umeletwa na kile kisa?”
“Kipi?”
“Yule mwendawazimu!”
“Yupi?”
“Mwenye mahaba na kitabu chako!”
“Kuna mwendawazimu ana mahaba na kitabu changu? Basi nitakuwa na hamu ya kumwona!” Nilisema.
“Tena yule pale, unamwona yule! Akiliona tu gari langu atakuja hapa.” Alisema mzee KK kauli iliyonishangaza.
“Kwa nini akiona gari lako lazima aje?” Niliuliza huku nikimwangalia. Niliona jinsi midomo yake ilivyobabaika kujibu.
“Am-ame-ame-nanilii- aaah kila nikija huwa napenda kumletea chakula!” Mzee KK alijibu kwa kubabaika.
“Kwa nini huwa unamletea chakula?”
“Dini, dini inataka hivyo!” Alisema kwa sauti iliyoonesha kuwa hakupenda kuendelea na yale maongezi.
“Nishushe hapo!” Nilisema huku macho yangu yakiwa yanamfuatilia yule Mwendawazimu.
Dakika chache baadaye nilikuwa nimeshaachana na Mzee KK na sasa nikawa naelekea upande ambao yule kichaa alikuwa ameelekea. Nilitembea kwa haraka kiasi. Nilipogeuka nilimwona mzee KK akiwa anaongea na simu huku akiniangalia. Lakini macho yetu yalipokutana aligeukia upande mwingine. Hisia mbaya zikanijia lakini nikapuuzia.
Utashangaa nikikuambia kuwa nilitumia saa mbili kumtafuta yule mwendawazimu, hii ikiwa ni pamoja na kuulizia watu lakini sikufanikia kumwona tena.
“Sijui, alikuwa hapahapa muda si mrefu!” Watu wengi walijibu hivyo. Niliendelea na msako wa kumtafuta mwendawazimu ambaye hatimaye nilikuja julishwa kuwa alikuwa akijiita, Kumbamasaka Jitu la Watu. Wenyeji wanasema mara kwa mara alikuwa akijipigapiga kifuani na kujiita, Kumbamasaka Jitu la Watu.
Wakati nikiendelea na msako ule hapo kwenye soko la Mwanga, mara nikashangaa nafuatwa na Askari Polisi watatu ambao waliongozana na kijana mmoja ambaye sura yake haikuwa ngeni machoni kwangu japo sikukumbuka kwa haraka nilimwona wapi. Askari mmoja kati ya wale watatu alikuwa amebeba bunduki. Ilikuwa yapata saa saba na robo mchana wakati walipokuwa wakitembea kuja mahali nilipokuwa nimesimama. Wakati huo nilikuwa nakusudia kutafuta sehemu ya kula. Yule kijana ambaye nilihisi kuwa namfahamu ama nimewahi kumwona sehemu alionekana kuwapa maelekezo wale askari. Wakaja moja kwa moja nilipokuwa nimesimama.
“Wewe ndiye bwana Japhet Sudi?
“Ndiye. Kuna shida yoyote!?” Nilijibu kwa mshangao.
“Ndiyo! Uko chini ya ulinzi kwa kuhusishwa na kifo cha mzee Khamis Kavula, wewe ukiwa ndiye abiria wake wa mwisho!” Alisema askari mmoja huku alinifunga pingu.
“Hutakiwi kujieleza sasa, maelezo yako yote utayatoa Kituo cha Polisi.” Askari mmoja aliniambia. Sikuona sababu ya kubishana nao, hata kama hiyo sababu ningeiona ubavu wa kubishana nao sikuwa nao. Nawajua hawa, sikutaka kipigo cha mbwa koko. Niliingizwa ndani ya gari na safari ya kuelekea Kituo cha Polisi ilianza. Njiani hakuna aliyekuwa tayari kuongea na mimi japo nilijitahidi sana kuwaongelesha wale watu.

Gari lilipofunga breki kwenye kiwanja cha Kituo cha Polisi, askari mmoja alininyanyua ndani ya ile Landcruser ya Polisi iliyo wazi na kunirushia nje. Nilitua ardhini kama furushi. Vumbi likatimka.
Nilikabwa na hasira kali huku maneno ya kulalamika yakinitoka.
Kofi moja la kisogoni toka kwa Polisi mmoja lilinituliza na nikaamriwa kutembea kuelekea ndani ya mapokezi ya kituo hicho.
“Vua viatu, mkanda na vingine, ubaki na suruali na shati tu!” Askari mmoja kati ya wale waliokuja kunichukua alitoa amri.
Nilitii.
“Huyu nini tena?” Aliuliza askari mmoja aliyekuwa na nyota tatu, ambaye alikuwa anatokea kwenye vyumba vya ndani vya kituo kile. Kabla hajajibu askari huyu ambaye ndiye aliyekuwa amenipiga kofi alipiga saluti halafu akasema, "Ndiye yule jamaa ambaye anahusishwa na kifo cha mzee KK!”
“Aaaah kumbe ndiyo huyu, liwekeni huko ndani tutalihoji kesho. Sasa hivi unatakiwa ufikirie namna ya kutupa majibu ya maana!” Alisema huyu mwenye nyota tatu.
Pwaaaaa! Kofi jingine la usoni nikalipata toka kwa yule yule jamaa wakati nilipotaka kujieleza mbele ya yule askari mwenye nyota tatu.
“Ingia huko ndani, umeshaambiwa utajieleza kesho!” Yule askari alisema huku akinisukumia kwenye kibaraza kingine.
Duuuh, ndiyo nikawa nimeingia selo hivyo!
Moyo uliniuma sana, hasira zikapanda na kushuka. Mwishowe nikajiridhisha kuwa sikuwa na namna zaidi ya kutulia na kusubiri muda wa kuhojiwa ili niseme ukweli wangu. Nilijua wazi kuwa wangenielewa kuwa sikuwa mhusika wa kifo cha Khamis Kavula.
Kabla ya hapa, sijawahi kulala Kituo cha Polisi.
Hii ilikuwa mara yangu ya kwanza.
Sitokaa nisahau.
Usiombe kulala kituoni.
Baridi la usiku, njaa, kubanwa haja na hali ya uchafu wa kile chumba.
Watu niliokuwa nimewekwa pamoja nao, wengine walikuwa na majeraha mazito, wengine wamelewa chakari, wengine nilihisi walikuwa wameokotwa kwenye mifereji ya maji machafu. Kulikuwa na kero za kila namna. Hali ilikuwa ngumu sana hasa ikizingatiwa kuwa nilikuwa nimewekwa mule ndani kwa kuonewa.
Tofauti na walivyokuwa wameahidi kuwa wangenihoji siku iliyofuata, hilo halikutokea.
Siku ya kwanza ilipita, yaani Jumanne yote nilishinda lupango. Jumatano asubuhi majira ya saa mbili asubuhi ndipo alipokuja askari mmoja kuniita kwa maelezo kuwa kuna ndugu yangu alikuwa amekuja kunisalimia. Kauli hiyo ilinishangaza sana, maana hakuna ndugu yangu aliyekuwa na taarifa kuwa nilikuwa nimewekwa ndani na isitoshe sikuwa na ndugu ninayemjua hapa Kigoma.
Nilisimama kinyonge.
Miguu ikiwa inatetemeka kutokana na njaa kali na mazingira ya mule ndani. Niliongazana na yule askari hadi sehemu ya mapokezi.
“Oooh, masikini, pole sana ndugu yangu Japhet!” Sauti ya mwanamke mmoja iliniambia. Badala ya kujibu, nilibaki namwangalia usoni kwa mshangao. Akaniminyia jicho moja la kulia, halafu akatabasamu. Sijui kwa nini nikajikuta nashawishika na kuelewa ile ishara yake.
“Asante sana aisee!” Nilijibu huku nikijitahidi kuficha mshangao wangu.
“Ndiyo mambo ya dunia!” Alisema huku akinyanyua kapu lake lilokuwa na chupa ya chai na bakuli kubwa la kuhifadhia chakula cha moto. Akaviweka juu ya ile meza kubwa ya kaunta ambayo askari huitumia kwa ajili ya kuandikia maelezo.
“Haya fungua uonje!” Askari alimwambia yule mwanamke. Ambaye alitii, alionja chai na chakula. Kisha akaniwekea. Kweli nilikuwa kwenye mshangao mkubwa. Lakini pasipo kujua sababu nikajikuta naogopa kumuuliza wewe nani mbele ya yule askari. Eti nikajikuta namfichia siri kwa vile tu aliniminyia jicho na kuachia lile tabasamu la kutaka nimfichie siri.
“Wewe ni nani?” Hatimaye nilimuuliza kwa sauti ya chini baada ya yule askari kutoka na kutuacha wawili kwenye kona tuliyokuwepo, hatua kama nne toka kwenye meza ya mapokezi. Niliuliza hivyo huku nikiwa najitafuna. Usiniulize kwa nini nilikula chakula cha mtu nisiyemfahamu. Wewe hujui njaa iliyokuwa ikiniuma wakati huo, hata chakula cha jalalani ningekula.
“Utanijua tu, mimi ni mjumbe!” Alisema yule mwanamke.
“Mjumbe!” Nilishangaa.
“Ndiyo!” Alijibu huku akiingiza mkono mfukoni na kutoa karatasi ndogo na kunipa.

NAJUA YOTE, UTATOKA LEO, TUONANE NYANGOFA NYUMBA NAMBA 511. Chogo.

Nilipomaliza tu kuisoma, yule mwanamke aliinyakua ile karatasi na kuifutika mfukoni. Nikabaki nimeshangaa.
“Wewe ni nani na unataka nini kwangu?” Niling'aka kwa sauti kali.
“Shiiiiiiii!” Aliweka kidole mdomoni kuashiria ninyamaze.
“Askariiiiiii!” Nilipiga kelele ili kuita askari aje.
Alikuja na kuchungulia.
“Vipi?”
“Hata simuelewi huyu ndugu yangu!” Alisema yule mwanamke huku akijifanya kuweka uso wa kushangaa.
“Nani ndugu yako?” Nifoka kwa sauti.
“Afande mimi simjui huyu mtu halafu wananitishia maisha!” Niliropoka kwa sauti kubwa. Halafu yule askari akabaki ananiangalia kama anayenishangaa.
“Mmmmh, makubwa, huyu kweli inawezekana ameua!” Yule mwanamke alisema huku akikusanya vyombo vyake.
“Kaka hebu tulia mbona unaongea vitu visivyoeleweka, hebu ongea taratibu ueleweke kama mtoto wa kiume wewe!” Alisema yule askari kwa dharau.
“Nasema hivi huyu si ndugu yangu, ana...!”
“Ni nani sasa kama siyo ndugu yako?” Askari alihoji
“Hata simjui, ana...!”
“Sasa kwa nini hukuniambia saa zile amekuja?” Askari aliuliza kwa mshangao.
“Alinishawishi kunyamaza nisiseme!”
“Alikushawishi vipi wakati na mimi nilikuwa pale na nikamsikia akikusalimia na kukuita ndugu na wewe ukaitikia bila shida?”
Askari alishangaa zaidi, nami nikaelewa kuwa lile kosa la kukubali kukonyezwa lilikuwa limeanza kunigharimu.
“Wewe hukuona ila huyu si mtu mzuri he...!” Nilijitahidi kusema.
“Sasa kwa nini umekubali chakula chake kama si mtu mzuri!?” Askari alihoji.
“Afande kwa heri, acha niende zangu, fadhili mfadhili punda siyo binadamu!” Alisema yule mwanamke huku akiondoka na kutingisha kiuno chake. Alikuwa amevaa suruali ya jeans ya bluu, shati jekundu na viatu vyeusi vilivyokuwa kama mabuti hivi. Alisuka twende kilioni, ila nywele zake zilionekana kuwa zenye matunzo mazuri sana. Macho makubwa ya mviringo yaliyokaa kwenye uso mrefu mwembamba. Alikuwa na midomo mizito, ambayo alipokuwa akiibetua ilionekana kuvutia. Sikutaka kuamini kuwa mwanamke huyu aliyejiita 'mjumbe' alikuwa anaondoka kirahisi tu hivi. Nikajiinua kwa nguvu ili nimfuate lakini nilirudishwa nyuma na kofi zito la shingoni. Nikawa mpole. Pamoja na kuropoka maneno mangi ya kulaani na kulalamika kuwa naonewa lakini nilirejea ndani ya chumba cha mahabusu. Jasho ikawa inanitoka kwa sababu ya hasira na kile chakula cha moto nilichokuwa nimekula. Mahabusu wenzangu walibaki wananiangalia. Mimi si mwepesi wa kulia, lakini mara hii nikajikuta nimeanza kulia kwa kwikwi, kile kilio cha kwikwi cha kiume.
Baadaye nikagundua kuwa kulia haikuwa inanisaidia. Nilianza kufikiria tena namna ya kujitoa kwenye janga lililokuwa mbele yangu. Kitendo cha wale askari kunikatalia kuwasiliana na ndugu zangu wowote kilinishangaza sana.
Saa nne na nusu nilikuja kuitwa tena. Niliandamana na askari hadi mapokezi.
"Bwana Japhet, kwa sababu za kipelelezi, tumeamua tukuachie kwa sasa, ila kesho asubuhi hakikisha unakuja kituoni tena, wakati huu sisi tunaendelea na upelelezi mwingine. Ila ni vema kujua kuwa mke mdogo wa Khamis Kavula ametoweka tangu jana usiku. Tunaendelea na uchunguzi.
Nikabaki mdomo wazi. Mara nikakumbuka ile karatasi niliyopewa na yule mwanamke aliyesuka twende kilioni. Moyo wangu ulipiga kwa hasira sana, lakini ukweli sikupenda kuendelea kukaa hapo kituoni hivyo sikutaka kuhoji. Maana kuhoji ingemaanisha nawauliza kwa nini mnaniachia. Nilichukua vitu vyangu nilivyokabidhi wakati naingia.
Nilitoka hapo kituoni nikiwa nimechanganyikiwa, akili yangu ilihitaji mapumziko kabla ya kuamua nini cha kufanya. Nikiwa njiani watu walikuwa wakinishangaa kwa jinsi nilivyokuwa nikinuka na nilivyokuwa mchafu.

Nilipofika hotelini nilienda moja kwa moja chumbani kwangu. Nilipoingia tu chumbani, nilipiga simu ya mezani ya chumbani humo kuagiza niandaliwe chakula. Baadaye nikaingia bafuni kuoga na kufanya usafi mwingine. Kwa kawaida miye hupenda sana usafi hivyo kukaa muda wote huo bila kuoga wala kupiga mswaki, kwangu ilikuwa ni adhabu isiyobebeka.
Dakika kumi baadaye nilikuwa nimemaliza kufanya usafi nikatoka bafuni na sasa nikawa navaa nguo. Sasa nikaona ndiyo wakati mwafaka wa kuichaji simu yangu, maana nilijaribu kuiwasha nilipotoka Polisi lakini ikaonyesha kuwa ilikuwa ineishiwa chaji. Nilikuwa na hamu ya kusalimia familia yangu maana nilijua fika kuwa wangekuwa na wasiwasi hasa baada ya kunikosa hewani kwa muda wote niliokuwa nimeshikiliwa na Polisi. Hivyo niliichomeka simu kwenye umeme.
Wakati nikisubiri chakula na simu ipate chaji nikaona nitumie muda huo kuandika kumbukumbu chache za matukio yaliyokuwa yametokea tangu nifike Kigoma.
Niliandika kwa kadiri nilivyoweza kukumbuka. Huwezi amini wakati naandika ilikuwa kama naangalia sinema vile. Kumbukumbu zilikuwa bado mpya kabisa kwenye ubongo wangu. Baadaye nilitoa kamera yangu ndogo niliyokuwa nimeenda nayo Sokoni Mwanga. Kulikuwa na picha tano tu. Moja ya hii hoteli niliyofikia, picha nyingine tatu zilikuwa za soko la Mwanga halafu moja ilikuwa ya yule mwendawazimu, Kumbamasaka Jitu la Watu. Niliipiga wakati Mzee KK alipokuwa akinionesha tulipofika pale sokoni Mwanga. Nilimwangalia yule kichaa jinsi alivyokuwa.
Mtu mrefu, nywele ndefu zisizo na matunzo, mweusi.
Macho makubwa mekundu.
Alikuwa amekenua meno ambayo yalionekana ya njano kama mhindi wa yanga wenye punje kubwa. Ndevu zake ndefu, chafu, zilikizunguka kinywa chake kama kichaka. Lakini meno bado yaliweza kuonekana. Alikuwa ameshikilia kitabu cheupe, ambacho sikupata shida kujua kuwa kilikuwa ni kile kitabu changu cha riwaya, SAA 72. Lakini begani alikuwa amebeba begi moja lilochakaa, chafu. Begi hilo lilikuwa limetuna kwa kujazwa vitu ndani. Hakuwa na shati, lakini alikuwa amevaa suruali moja ya jeshi iliyokuwa imechakaa sana, kama usingekuwa makini usingeweza jua kuwa suruali ile ilikuwa nyekundu hasa kwa vile ilivyokuwa chafu sana na kuwa na wekundu fulani uliopakazwa udongo mwekundu wa Kigoma. Miguuni alikuwa amevaa viatu vilivyochoka sana, lakini bado ungeweza kuona kuwa viatu vile vilikuwa kama mabuti ya jeshi.
Mara macho yangu yakavutwa na kitu kama filimbi ambacho kilikuwa kikining’inia kwenye shingo ya yule kichaa. Kitu hicho kilikuwa kimefungwa kwenye kamba ambayo alikuwa ameivaa shingoni. Nilikiangalia kile kitu lakini bado sikuweza kujua ni nini hasa, japo kilifanana na filimbi.
Nilishituliwa na mlio wa simu iliyokuwa chumbani humo. Niliweka chini ile kamera nikaifuata simu na kuunyanyua mkonga wake.
“Chakula chako kiko tayari, tukuletee chumbani au utakuja kulia kwenye ukumbi wa chakula?” Sauti ya kiume iliongea.
“Nitakuja kulia kwenye ukumbi. Asante!” Nilisema halafu nikaweka mkonga mezani. Niliacha vitu kama vilivyokuwa, ikiwa ni pamoja na simu ambayo bado ilikuwa ikipata moto.
Nilielekea kwenye ukumbi wa kulia chakula. Ili kufika kwenye ukumbi wa chakula ilikuwa lazima upitie mapokezi halafu ndiyo uende upande mwingine wa jengo. Wakati napita sehemu ya mapokezi msichana aliyekuwa mapokezi aliniita.
“Wewe ndiyo unaitwa Japhet Nyang’oro Sudi?” Aliniuliza baada ya kusogea sehemu ya mapokezi. Japo sikufurahia kuwa hakuwa ametoa hata salamu, lakini niliona acha nifanye wajibu wangu.
“Hujambo lakini dadangu!?” Nilisema.
“Looh! Samahani jamani kakangu, nimesahau hata kukusabahi. Sijambo, sijui wewe mwenzangu?” Alisema huku akiwa na uso uliojaa aibu.
“Wala usijali, mara nyingine kazi zikiwa nyingi ndivyo inavyokuwa. Mimi sijambo. Ndiyo naitwa Japhet!” Nilisema kwa bashasha.
“Basi kuna mtu anaitwa Jacob Matata alipiga simu jana akasema ukirejea hakikisha unampigia, anakutafuta.” Alisema yule dada huku akiwa anasoma kijikaratasi, bila shaka ni sehemu aliyokuwa ameandika jina la Jacob Matata ili asisahau.
“Duuuh, asante. Nitampigia, tena ngoja niifuate simu ili nimpigie sasa hivi!” Nilisema halafu nikageuka na kutembea kurudi upande ule niliokuwa nimetoka ambako ndiko kwenye chumba changu cha kulala. Niliingia chumbani kwangu, na kuuacha ufunguo ukining’inia mlangoni wakati nikipiga hatua kuelekea sehemu nilipokuwa nimeiacha simu yangu. Mara moyo ukapiga paaaah! Simu haikuwepo. Nikaangaza macho mle chumbani, hakukuwa na chochote. Kamera, begi langu, zile nguo chafu nilizokuwa nimevua na kubadilisha, ile shajara, vyote havikuwepo.
“Jesus!” Nilishangaa.
Niliwa bado nimeshikwa na mshangao ndipo nilipoona kijikaratasi kikiwa kitandani. Haraka nilisogelea kitandani. Nilipokiangalia tu hata kabla sijakisoma mara kumbukumbu ya kijikaratasi nilichopewa na yule mwanamke aliyeniletea chakula Kituo cha Polisi, aliyekuwa amesuka twende kilioni zilinijia. Nilipokishika tu na kuona maandishi yake ndipo nilibaki kinywa wazi.
Mwandiko uleule. Ujumbe ule ule. Karatasi ile ile.

NAJUA YOTE, UTATOKA LEO, TUONANE NYANGOFA NYUMBA NAMBA 511. Chogo.

Moyo wangu ukapiga kwa kasi sana.
“Hawa washenzi ni nani na wananitakia nini lakini?” Nilijikuta naongea mwenyewe kwa sauti kana kwamba nilikuwa naongea na mtu. Wazo la kwenda au kutokwenda kwenye nyumba niliyoelekezwa kwenye hicho kikaratasi likajaa akilini mwangu. Nikajikuta napambana vikali nafsini mwangu.
Lakini watu hawa si wazuri.
Lakini mbona wanasisitiza sana niende huko?
Kama ni kuniua wangeweza kuniua hata hapahapa chumbani.
Labda si watu wabaya kama ninavyodhani. Wameniletea chakula.
Ninahisi ndiyo waliopanga nitoke Polisi!
Wanataka nini lakini?
Au nitoe taarifa polisi kuwa kuna watu wananifuatilia?

* * *
Nikiwa nimetaharuki vibaya sana, nilipiga hatua za haraka kuelekea kwenye simu ya mezani iliyokuwa kwenye meza ndogo pembeni ya kitanda. Niliunyakuwa mkonga wa simu na kubonyeza namba 9, nikiwa na lengo la kumtaarifu yule msichana wa mapokezi. Lakini nilipoweka sikioni kile kiwambo cha kusikilizia, kulikuwa kimya na ubaridi. Ile sauti ya kuonyesha kuwa kulikuwa na uhai kwenye ule mkonga haikuwepo. Hapo nikagundua kuwa simu ile ilikuwa haina uwezo wa kufanya mawasiliano tena.
“Mmmh mbona nilitumia simu hiihii dakika chache zilizopita!?” Nilijinong’oneza kwa mshangao. Nikaanza kuangaza na kuangalia kama kulikuwa na hitilafu yoyote ya nyaya za simu hiyo. Hivyo macho yangu yalitembea kuufuata waya uliotoka kwenye mkonga wa simu kwenda ukutani. Naam! Baada ya nusu mwendo ya safari ya macho kwenye waya huo, macho yakajikuta yanaishia kwenye kingo za waya uliokatwa.
Ulikuwa umekatwa.
Majeraha ya waya kukatwa yalikuwa mapya kabisa huku ule waya mdogo wa ndani ukitoa mng’ao wake.
“Alijuaje nitataka kupiga simu?”
Hofu ikanizidi, nikajikuta nakurupuka kutoka mule chumbani. Nilifika mapokezi huku nikitweta. Pumzi na jasho vilinitoka kwa fujo. Yule msichana wa mapekezi akabaki anashangaa.
“Vipi kaka?” Aliuliza kwa mshangao.
“Umemwona akipita hapa?” Nilisema
“Nani, Jacob Matata?” Aliuliza yule dada
“Hebu acha ujinga dada!” Nilimfokea yule dada baada ya kumtaja Jacob Matata wakati mimi nilikuwa naulizia kama amemwona mtu aliyetoka na vitu vyangu.
“Eee, kaka samahani babu wee, mjinga utakuwa wewe! Mtu alipiga simu tokea Dar sasa hivi nimekwambia mpigie halafu wewe unauliza umemwona? Kama si maajabu hayo ni nini?” Alifoka yule dada.
“Neema unabishana na nani tena?” Sauti ya kiume ilisikika. Nikageuka kuangalia upande ilipotokea.
Nikakutana na mshituko mwingine tena.
Macho yangu yalikuwa yakitazamana ana kwa ana na yule askari.
Askari mwenye nyota tatu ambaye nilionana naye siku ile naingizwa selo. Hakuwa amevaa sare za kazi. Nilimkumbuka vema sauti yake na lile kovu lake kubwa, baya, lililokuwa shavuni. Aliponiona aliushusha uso wake kwa dharau.
“Kumbe unaongea na huyu muuaji, kichaa huyu. Achana naye huyu. Kwani wewe unamjua mtu huyu zaidi ya kuwa mteja wako tu?” Alisema yule askari kwa dharau huku akimwangalia yule mhudumu ambaye sasa nilijua kuwa alikuwa akiitwa Neema.
“Mi namshangaa, jana wakati hayupo kuna mtu kapiga simu kuwa huyu bwana akirejea ahakikishe amempigia simu. Kama dakika ishirini zilizopita nimempa taarifa, akasema acha afate simu ili ampigie. Sasa hivi anerejea hapa akitweta na kuuliza kama nimemwona. Nami ndiyo namshangaa!” Neema alijieleza kwa yule askari.
“Samahani, nadhani hatukuelewana, kuna mtu kaingia chumbani kwangu na kuchukua kila kitu, zaidi sana amekata waya wa simu ya ndani. Sasa kwa vile nilikuwa nimeshikwa na taharuki ndiyo maana nikauliza moja kwa moja bila kukuelewesha vema. Hivyo nilikuwa nauliza kama umemwona mtu yeyote aliyetoka na begi langu?” Nilijieleza kwa sauti ya utulivu huku nikijitahidi kudhibiti jazba yangu kufuatia maneno ya yule askari mwenye nyota tatu, ambaye sasa nilibaini kuwa alikuwa na chuki na mimi. Lakini pia, nilikuwa najiuliza nini kilikuwa kimemleta hapo hotelini.
“We jamaa fala kweli!” Yule askari alisema huku akianza kuondoka eneo hilo la mapokezi.
“We kaka acha nikuitie askari huwezi haribu simu yetu hivi hivi halafu unajisingizia kuibiwa.” Neema alisema kwa jazba. Maneno ya Neema yalimfanya yule askari ageuke na kumwangalia Neema.
“Neema mpenzi, mwache, ya nini kuhangaika na mfungwa mtarajiwa huyu!” Alisema halafu akaendelea na safari yake. Kauli yake ikamtuliza Neema. Ambaye sasa alibaki akiniangalia.
Yule askari mwenye nyota tatu alipotoweka nilimsogelea yule msichana. Nikaongea kwa sauti ya utulivu. “Neema, sina shida yoyote ya akili wala mimi siyo mhalifu, ila ninahisi kuna mchezo nimechezewa hapa na sijui lengo lake ni nini?”
Nilisema huku nikiziangalia gololi za macho ya Neema kwa ule ushawishi wa kiume.
“Sasa shida nini, maana nahisi kama uko hatarini?” Neema alisema kauli ambayo nilikubaliana nayo. Sauti yake haikuwa ile aliyokuwa akiitumia dakika chache zilizopita. Hii ya sasa ilikuwa na chembechembe fulani hivi ambazo ni ngumu kuzielezea. Sauti hiyo ilinishawishi kumuelezea msichana huyo kila kitu, kuanzia lengo la safari yangu hadi kinachonitokea sasa. Nilipomalizia kumwelezea nilikuwa natetemeka kwa hasira.
“Mimi nakushauri, nenda kale kwanza. Ukimaliza kula, akili itapata nguvu ya kufikiri kwa utulivu zaidi. Mimi sina namna ya kukusaidia kaka yangu. Pole sana!” Neema alisema.
“Je, unadhani nani anaweza kuwa ameingia chumbani kwangu kuchukua vitu vyangu?” Nilihoji kwa utulivu wa kujilazimisha.
“Hatuna historia ya wateja wetu kuibiwa vitu. Nimeshangazwa sana na tukio unaloniambia. Nitauambia uongozi wa hoteli na bila shaka watashughulikia. Mimi sijaona mtu yeyote akipita hapa, isitoshe muda huu wa saa tisa kasoro mchana wateja wetu wengi wanakuwa wameenda kwenye shughuli zao zilizowaleta hapa Kigoma. Wengi hurejea majira ya saa kumi na moja, wakati huo ndipo hoteli huanza kuchangamka tena.” Alisema Neema.
Sikuwa na namna zaidi ya kufuata ushauri wake wa kwenda kula kwanza. Nilipiga hatua kama tano hivi, halafu nikasimama, nikawa nimepata wazo. Nikarejea pale mapokezi.
“Hivi unaweza iona namba ambayo Jacob Matata alikupigia nayo? Maana sasa nashindwa kuwasiliana naye kwa vile namba yake ilikuwa kwenye simu iliyoibwa.” Nilisema kwa sauti ya kuomba.
“Hapana simu yetu ni ya mezani, tena zile za kizamani ambazo huwezi ona namba ya mpigaji. Nitakutaarifu kama atapiga tena.” Neema alisema huku uso wake ukionyesha kuwa alikuwa hataki kuendeleza mazungumzo na mimi.
Nikaelekea kwenye ukumbi wa chakula huku akili yangu ikiwa imevurugika vibaya sana. Ule ujumbe wa kwenye karatasi, NAJUA YOTE, UTATOKA LEO, TUONANE NYANGOFA NYUMBA NAMBA 511. Chogo, ulizidi kujirudiarudia kwenye akili yangu. Kiu ya kwenda kuonana na huyo mtu aliyejiandika kama Chogo ikaanza kuumbika.

* * *

Nilishambulia chakula kwa fujo. Wakati nikila mawazo na maswali mengi yalikuwa yakipita kichwani kwa kasi sana.
Yule mwendawazimu yuko wapi?
Nani kamuua KK na sasa nasingiziwa mimi?
Chogo ni nani?
Ni nani kaingia chumbani kwangu na kuchukua vitu vyangu?
Je, ni yule mwanamke aliyesuka twende kilioni?
Maana ndiye aliyeondoka na ile karatasi na sasa nimeikuta kwenye kitanda chumbani.
Yule askari mwenye nyota tatu mbona anadharau kiasi kile?
Anaonekana ana chuki sana na mimi. Kwa nini?
Nilipomaliza kula nikajiuliza nianzie wapi. Suala la kwenda polisi kutoa taarifa ya kilichonikuta nikalifuta kabisa kila nilipomfikiria yule askari mwenye nyota tatu.
“Nini kimenileta Kigoma?” Nilijihoji.
“Kuonana na yule mwendawazimu!” Nilijijibu.
“Kwa nini?” Nilijihoji.
“Kwa sababu ya mahaba yake kwa kitabu changu. Kama mwandishi nilikuwa na hamu ya kujua kwa nini alikuwa amekipenda kitabu changu kiasi hicho.” Nilijijibu.
“Kutokana na hali ilivyo je, ni lazima kuendelea na azma yangu ya kutaka kuonana na mwendawazimu?” Nijihoji tena.
Hapana, bora niache!
Ila sasa tayari ni mshukiwa wa mauaji ya KK.
Ila kuna uwezekano pia, kuwa mtu aliyeniandikia ule ujumbe alikuwa anajua kila kitu kama alivyoandika. Ni lazima nimjue, niongee naye. Kama anajua kila kitu basi awataarifu polisi ili mimi niwe huru.
Majibizano hayo ya ndani ya nafsi yangu yalihitimika kwa mimi kukata shauri kuwa niachane na suala la yule mwendawazimu, Kumbamasaka Jitu la Watu na sasa nizame katika kujikwamua kwenye kesi iliyokuwa mbele yangu.
Hivyo nikaamua nifanye hivi;
Kwanza nipige simu kwa mke wangu kumtaarifu kuwa niko mzima ila tu nimeibiwa vitu vyangu.
Pili, nikaonane na Chogo. Halafu, nikitoka hapo nihitimishe siku kwa kwenda nyumbani kwa KK ili kujua alikufaje haswa, maana hilo sikupata kuelezwa kwa kina.
Lakini jingine ni kujua mke mdogo wa KK amepotea katika mzingira gani.

Nilitoka kwenye ukumbi wa chakula baada ya kuwa nimelipia. Nilitembea hadi mapokezi. Nilimkuta Neema akisoma gazeti. Aliliweka chini aliponiona nakaribia meza ya mapokezi.
“Neema, natoka kidogo ila kuna jambo nilikuwa nataka kukuuliza. Hivi ulikuwa unajua huyo marehemu KK alikuwa anaishi wapi?” Nilisema kwa sauti tulivu.
“KK ndiyo nani?” Neema aliuliza kwa mshangao.
“Si yule dereva teksi aliyeuawa jana aliyekuwa akiegesha hapo mbele ya hoteli. Jina lake kamili ni Khamis Kavula!” Nilifafanua. Lakini bado niliona macho ya Neema yalikuwa na mshangao.
“Hapana, simjui mtu mwenye jina hilo!” Neema alisema huku sauti yake ikionyesha kuwa alikuwa akimaanisha alichosema. Nilishangaa sana.
“Una muda gani tangu umeanza kufanya kazi kwenye hoteli hii?” Niliuliza
“Miaka zaidi ya saba sasa.” Alijibu haraka.
“Je, inawezekana kukawa na dereva anayeegesha hapo nje halafu ukawa humfahamu?” Niliuliza.
“Haiwezekani! Wote wanaoegesha hapo nje huwa na vibali maalum vya hoteli. Wote hutakiwa kujaza fomu maalum ya kuomba kuwa wanaegesha hapo nje. Hii ni kuhakikisha tunakuwa na taarifa za madereva wote kwa ajili ya usalama wa wageni wetu. Hatutaki wafanyiwe kitu kibaya.” Neema alifafanua. Maelezo yake yaliniingia vema. Lakini niliona mwanya fulani hapohapo.

“Okay, kuna dereva alinitelekeza jana na nilimchukua hapa kwenye maegesho alijitambulisha kwangu kwa jina la Khamis Kavula au alisema anajulikana sana kwa jina la Mzee KK. Sasa kama humjui kwa majina hayo ina maana aliniongopea. Je, unaweza nisaidiaje? Je, inawezekana aliegesha bila ruhusa yenu?” Nilihoji.
“Haiwezekani, walinzi wasingemruhusu. Madereva wetu ni hawa hapa!” Neema alisema huku akitoa kitu kama daftari pana ambalo lilikuwa na picha na majina ya madereva. Nilianza kuangalia sura moja baada ya nyingine bila mafanikio ya kuona sura ya mzee KK. Hapo nikajua nilikuwa nimedanganywa. Lakini niliweza kuiona sura ya yule kijana ambaye aliwaleta askari polisi kule Mwanga sokoni. Sasa nilimkumbuka vema, huyo kijana alikuwa miongoni mwa madereva vijana waliokuwa kwenye maegesho wakati mimi nilipochagua kwenda na gari la mzee Khamis Kavula.
“Huyu anaitwa nani? Niliuliza nikionyesha kidole kwenye picha ya yule kijana.
“Jina lake liko hapa pembeni. Kigi Mbonea.” Neema alisema.
“Leo yupo?” Niliuliza.
“Hapana. Aliaga jana kuwa amepata safari ya kwenda Kampala.” Neema alisema.
“Unajua anapoishi?” Niliuliza.
“Ndiyo anaishi mtaa wa Ogonapo nyumba namba 0870.” Neema alisema, huku akiniangalia kwa macho ya mashaka.
“Asante, wacha niende nitarejea baadaye.” Nilisema na kupiga hatua za kutoka nje ya hoteli. Nilikuwa na hela mfukoni na kadi zangu za benki na vitambulisho vilikuwa kwenye pochi yangu. Hivyo vilikuwa vimenisurika kuibwa. Nilitembea taratibu wakati nikiwapita madereva teksi waliokuwa wameketi mahali palepale nilipowakuta jana.
“Kaka leo huchukui usafiri?” Mmoja alisema.
“Namtaka dereva wangu wa jana.” Nilisema bila kuonyesha shaka yoyote.
“Yule hayupo, alikuwa mgeni tu hivyo hayupo tena.” Dereva mmoja alisema.
“Mimi napenda wageni, dereva gani mgeni leo ili niende naye?” Niliuliza kwa sauti ya mzaha kiasi lakini swali hili lilikuwa na uzito sana kwangu.
“Aaaah! Huwa haturuhusu wageni, labda kwa sababu maalumu sana.” Dereva mwingine alisema.
“Sasa kwa nini jana mliruhusu au ndiyo kulikuwa na hiyo sababu maalumu?” Nilizidi kuhoji.
“Mwenzetu mmoja alitueleza kuwa yule mzee alikuwa na matatizo mazito na alihitaji hela ya haraka hivyo akatuomba tumpe nafasi. Kwa pamoja tukakubali.” Alijibu yule aliyeongea pale kwanza.
“Okay, huyo aliyekuwa tayari kumsaidia yule mzee mimi ndiyo namtaka huyo sasa. Maana ukitoa unapokea. Sasa leo zamu yake.” Nilisema.
“Bahati mbaya Kigi hayupo.”
“Hayupo kabisa au atarejea baadaye?”
“Amepata safari ndefu. Amekwenda Kampala, Uganda.” Mwingine alisema.
Majibu yale yalitosha na niliona kuwa yalioana sana na yale niliyopewa na Neema kumuhusu huyo Kigi Mbonea.
Unaweza kuona sasa.
Inaonekana kulikuwa na kitu kati ya huyo Kigi na KK.
Sasa nikaanza kuingiwa na wasiwasi kuwa inawezekana suala langu lilikuwa limepangiliwa vema. Hamu ya kuonana na Kigi Mbonea ikaumbika ndani ya nafsi yangu. Hivyo nikajiapiza kuwa lazima niende nyumbani kwake pindi nikitoka kuonana na Chogo.

Sikuchukua teksi pale hotelini. Nilitembea kwa miguu hadi nilipofika maeneo mengine mbali na hotelini ndipo nikachukua teksi na kuomba nipelekwe Nyangofa. Haikuwa mbali sana. Nilimlipa mtu wa teksi halafu nikaanza kusoma namba za nyumba. Sehemu aliyoniacha, nyumba zilikuwa kwenye namba 210, hivyo nikajua ingekuwa kwenye barabara ya tatu upande wa juu ndipo ningeweza kukuta nyumba zenye namba 500, kwani kwa mujibu wa ile karatasi, Chogo alitaka nikutane naye nyumba namba 511.
Hivyo nilijaribu kutafuta vichochoro vya kunipeleka mitaa ya upande wa juu.
Makadirio yangu yalikuwa sawa. Nilipotokezea tu kwenye mtaa wa tatu upande wa juu macho yangu yaligongana na geti lililokuwa na namba 501. Hivyo nikakata kushoto na kuelea upande huo ambapo namba za nyumba zilikuwa zikiongezeka.
Wakati huo nikayasikia mapigo yangu ya moyo yakienda kwa kasi. Mapigo ya moyo yaliongezeka nilipokuwa nyumba namba 509. Hii ilimaanisha nyumba ya pili toka hii ndipo ningekutana na Chogo.
Jasho ikaanza kunitoka lakini nikajipa moyo kuwa ilikuwa lazima nionane na huyo mtu. Huenda akawa na msaada kwangu kwenye mkasa huu. Mbele ya nyumba namba 511 kuliegeshwa gari aina ya Landcruiser lililokuwa na namba za usajili zenye rangi nyekundu. Nikavuta pumzi nyingi na kuziachia kwa nguvu wakati napiga hatua kuliendea geti la nyumba namba 511.
Kama zilivyo nyumba nyingi za Kigoma, nyumba hii ilikuwa kuukuu. Rangi yake ya maziwa ilikuwa imemezwa na ile nyekundu ya udogo wa mji huo. Ungeweza dhani kuwa nyumba hiyo ilikuwa ya rangi nyekundu. Ilikuwa nyumba ya ukubwa wa wastani, nilikadiria ingekuwa nyumba yenye vyumba vinne hivi vya kulala. Geti kubwa, lilikuwa limefungwa lakini mlango mdogo ambao huwa sehemu ya geti kubwa ulikuwa wazi. Hivyo nilipogonga kwa muda bila kuona mwenyeji akitoka ndani ya nyumba niliamua kuingia getini kwa kupitia ule mlango mdogo.
Nilipiga hatua zilizojaa wasiwasi huku kwa sauti yenye kutetema nikasema;
“Hodi! Hodi humu ndani! Hodi wenyewe!”
Kimya.
Wakati naendelea kupiga hatua kuelekea kwenye mlango wa mbele wa nyumba nilishangazwa na jinsi nyasi zilivyokuwa zimeshamiri kwenye kiwanja cha mbele cha nyumba. Kwa akili ya kawaida kabisa ungesema ama nyumba haikuwa ikikaliwa na mtu au mkaaji aliifanya nyumba hiyo kama kiota tu. Anatoka asubuhi sana na kurejea usiku mkali. Kingine nilibaini kuwa lile gari nililoliona kwa mbali, nilipolikaribia nilibaini kuwa lilikuwa na sifa ya kuwa vyuma chakavu. Lilionyesha kuwa halikuwa likitumiwa kwa miaka mingi sasa. Matairi yake yalikuwa yameoza huku likiwa linaliwa na kutu kwa kasi.
Kadiri niliyousogelea mlango nilianza kupata hisia kuwa inawezekana ndani ya nyumba ile hakukuwa na mtu aliyekuwa akiishi. Lakini nikiwa hatua tatu toka mlangoni niliweza kusikia sauti ya redio ndogo ikiwa inatokea ndani ya nyumba hiyo. Niliangalia saa yangu ilikuwa saa tisa na dakika hamsini alasiri. Niliufikia malango na kuugonga. Ile nguvu ya kuugonga mlango ukaanza kufunguka wenyewe.
“Hodi! Hodi humu ndani!”
Kimya.
Nikaendelea kusema hivyo kwa dakika kama kumi hivi lakini nikajiridhisha kuwa huwenda mwenyeji wangu alikuwa amelala usingizi mzito.
Nikapiga hatua moja ndani.
Nywele zikanisisimka.
Lakini nikaona wacha niingie sebuleni. Hivyo kama afanyavyo kuku aingiapo bandani jioni ndiyo nilivyokuwa nikipiga hatua na kujitahidi kuchungulia niendako.
Jasho lilikuwa linanitoka kwa fujo.
Moyo ulikuwa ukipiga kwa kasi.
Kwa vile madirisha yalikuwa yamefungwa yote, taa ilikuwa inawaka kuipa sebule mwanga.
Macho yangu yaliangaza mule sebuleni bila kuona kitu.
Yalipotua tu kwenye kochi ndipo niliona mwanamke akiwa amelala. Sura yake haikuonekana kwa vile alikuwa amegeukia upande wa kochi. Alikuwa amejifunga khanga na alikuwa amevaa blauzi nyekundu.
Achilia mbali nguo zake, maumbile yake pia yalionyesha kuwa alikuwa mwanamke.
Makalio yake. Miguu yake ilivyokuwa mizito yenye ule ukungu wa kike. Kiuno. Shingo yake.Vidole vyake pia.
Nilimwangalia kwa dakika chache.
Redio niliyosikia ilikuwa juu ya meza ya chakula. Meza ilikuwa kwenye kona moja ya sebule hiyo. Ilizungukwa na viti sita; vitatu upande huu, vitatu vingine upande huu. Ilikuwa redio ndogo tu. Taa nyekundu ya redio hiyo ikionekana wazi.
“Habari yako dada? Hodiiii!” Nilisema kwa sauti. Ikafikia wakati nikapaza sauti ili kumwamsha mwenyeji wangu lakini juhudi zangu ziligonga mwamba.
Mwishowe nilikata shauri kuwa nisogee pale alipokuwa amelala yule mwanamke ili nimwamshe. Nilipiga hatua taratibu hadi jirani na kochi.
Wakati nainama, redioni ulikuwa wimbo wa Harmonize na Diamond Platnumz uitwao Kwangaru. Wakati nainama, ilikuwa ikiimba ile sehemu isemayo;
‘Unataka maji ya kisima na mwoga wa kuchutama, aaah inama inama…’
Mtu angekuwa anachungulia dirishani angedhani nimeinama kufuata wimbo huo. Kumbe mimi nilikuwa kwenye ulimwengu wa mkasa mzito. Basi nikainama na kumtingisha mwenyeji wangu.
Mmmmh! Nikagutuka kidogo. Mwili ulikuwa mkavu. Wa baridi sana.
Tone tatu za jasho zilinitoka na kundondokea sakafuni. Wakati naugeuza mwili ili nione usoni ghafula nikasikia sauti ikiniamuru.
“Tulia hapo hapo!” Amri ilitokea mlangoni. Niligeuka haraka kuangalia kulikoni.
Macho yangu yakakutana na askari wanne wakiwa mlangoni. Walikuwa ni askari walewale waliokuwa wamenichukua toka sokoni siku ya jana. Ila leo alikuwa ameongezeka yule askari mwenye nyota tatu.
“Umemuua na huyu?” Alisema tena kwa ile sauti yake ya dharau.
“Umemuua mke mdogo wa Mzee KK?!” Alisema huku akiwa ameshanifikia. Alinipa kofi kali la usoni ambalo lilinipeleka chini. Nikalamba sakafu. Halafu akanikanyaga kwa teke kali mgongoni. Wakati nikiwa chini naugulia maumivu ndipo macho yangu yakaona kitu chini ya kochi. Ilikuwa ni kile kitu kama filimbi nilichokiona kwenye kifua cha yule mwendawazimu aitwaye Kumbamasaka. Hivyo aliponitandika teke jingine nilijifanya kuvingirika kwa maumivu na kuingia kwenye uvungu wa kochi. Nilikichukua kile kitu na kwa namna ya kujinyonga nyonga na kuugulia maumivu nikakiingiza kwenye chupi.
“Simama juu muuaji mkubwa wewe. Safari hii huna namna ya kuruka!” Alisema yule Askari huku nikifungwa tena pingu.
Ukweli nilichanganyikiwa. Balaa juu ya balaa.
Ila akili yangu ikafanya kazi haraka na kujiuliza; amejuaje ni mke mdogo wa KK kabla hata hajamwona usoni? Maana kauli yake ya pili aliniuliza, “Umemuua mke mdogo wa Mzee KK?!”
Hilo likanishangaza na kunipa mashaka makubwa moyoni.
Kama siku ile pale sokoni, hawakutaka maelezo yangu.
“Utakwenda kujieleza kituoni!” Niliambiwa.
Walimwangalia yule mwanamke pale kwenye kochi.
Kweli alikuwa amekufa, japo ilionyesha kuwa hakuwa amekufa muda mrefu uliopita. Nami nikapata fursa ya kumwangalia yule mwanamke usoni, kwa mara ya kwanza. Wakati huo nilikuwa nikiongea maneno mengi ya kujitetea kuwa sikuwa najua lolote. Lakini, maneno yangu yalikuwa kama najisumbua tu mbele ya wale askari.
Ina maana walikuwa wakinifuatilia? Au walikuwa wakinisubiri mahali niingie?
Nilijiuliza bila kupata majibu.
Waliingia kukagua vyumba vingine. Huko walipata begi langu na vitu vyangu vingine ambavyo mimi najua vilikuwa vimeibwa kule hotelini.
“Kwa hiyo haya ndiyo yamekuwa makao yako ya siri halafu unajifanya umeibiwa?” Alisema yule askari mwenye nyota tatu.
Nilijaribu kujibu na kujieleza lakini hakuna aliyenisikiliza.
Muda mfupi baadae gari la wagonjwa lilikuja kuichukua ile maiti. Mimi niliingizwa ndani ya gari lingine aina ya Landcruiser lililokuwa na namba za usajili za kiraia. Nikiwa ndani ya gari huku nikilia sana. Nilikuwa nimegeukia upande ilipokuwa nyumba namba 511. Mara macho yangu yakaona kitu ambacho sikutarajia kukiona.
Nilimwona yule mwendawazimu akiwa anatokea kwenye uchochoro uliokuwa katikati ya nyumba namba 511 na namba 512. Nilijikuta nimeacha kulia. Nikawa namwangalia tu. Alikuwa na lile begi lake na mkono wa kulia alikuwa na kile kitabu SAA 72. Niliangalia shingoni kama angekuwa na kile kitu kama filimbi. Hakikuwepo. Nikajua kuwa ni kweli kuwa nilichookota pale chini ya kochi ilikuwa ni mali ya yule mwendawazimu Kumbamasaka, Jitu la Watu.
Gari liliondolewa kwa kasi, mimi macho yangu yalibaki yanamwangalia yule mwendawazimu ambaye sasa alikuwa akitembea kwenye ule mtaa.

Tulipotoka barabara ya Kaya na kuingia kulia kuacha ile ya kushoto iliyoenda stesheni ya treni sikuwa na wasiwasi kuwa tulikuwa tukielekea Kituo cha Polisi. Tulipoambaa ambaa na barabara ya Lumumba, japo gari lilikuwa kwenye mwendo wa kasi sana lakini bado nilijua tunaelekea Kituo cha Polisi. Tulipofika njia panda mwanzoni nilidhani tunaelekea Kituo cha Polisi. Wasiwasi ulianza kunijia wakati tulipofika kwenye njia panda ya barabara iendayo Hospitali ya Mkoa wa Kigoma na ile iendayo upande wa Mwembe Togwa. Tulikunja kushoto kuchukua upande wa Mwembe Togwa. Hapo sasa nikaanza kupata wasiwasi.
Gari lilikwenda kwa kasi ileile hadi tulipokaribia SIDO Mkoa. Gari likapunguzwa mwendo. Kwa mbele niliona gari aina ya Nissan Safari likiwa limeegeshwa upande wa kulia pembeni ya barabara chini ya miti miwili mikubwa. Gari nililokuwemo lilipofika eneo hilo lilikatisha na kwenda upande ilipokuwa ile Nissan. Hili gari lilisimama pembeni ya ile Nissan ila injini ya gari haikuzimwa. Alishuka yule askari mwenye nyota tatu ambaye sasa alikuwa amevaa kiraia. Akatembea kwenda kwenye ile Nissan. Kioo cha upande wa mbele wa abiria kilishuka na hapo kukafanyika maongezi mafupi. Baadaye kioo kikapandishwa, yule askari mwenye nyota tatu alifanya ishara kuwa nishushwe. Nikashushwa na kupelekwa upande wa nyuma wa ile Nissan. Mlango wa nyuma ukafunguliwa. Kabla sijaingizwa ndani ya ile Nissan nilifunguliwa pingu halafu nikashitukia navutwa na mikono yenye nguvu na mikakamavu kama ubao. Nikatua upande wa ndani wa Nissan.
Mlango ukafungwa.
Gari likawashwa.
“Mnanipeleka wapi?” Hatimaye niliuliza kwa mshangao.
“Wewe ulitaka upelekwe wapi?” Sauti ya mtu mmoja aliyekuwa miongoni mwa watu wanne waliokuwa upande huu wa nyuma aliongea.
Niligeuka kumwangalia.
Alikuwa ameketi kwa kuridhika sana.
Mtu huyo hakuonekana kutingishika wala kuhangaika wakati naingizwa garini. Alikuwa amevaa suti nyeusi na shati nyeupe bila tai. Viatu vizuri sana na saa ya gharama sana mkononi. Alionekana nadhifu.
“Polisi, si ndiyo sehemu ya kupelekwa watu wanaotuhumiwa kwa uhalifu?” Nilisema kwa sauti ya kutetemeka, kifua kilikuwa kimejaa hofu na hasira.
“Hukumbuki ujumbe wangu?” Alisema yule jamaa nadhifu kwa sauti nzito tulivu, bila kugeuza kichwa kuniangalia. Ilikuwa kana kwamba anaongea na dirisha la gari.
“Assa, tuzungushe kwanza niongee na Japhet.” Alisema yule jamaa nadhifu, gari likaondolewa.
“Ujumbe gani?” Niliuliza.
“Ulioletewa kituoni na mchana wa leo chumbani kwako?!”
“Wewe ni nani?”
“Wananiita Chogo.”
“Ila wewe unajiita nani?”
“Napenda wanavyoniita.” Alisema huku akitoa tabasamu la kifedhuli usoni.
“Watu wako ndiyo waliochukua vitu vyangu?” Niliuliza kwa hasira.
“Mtu wangu, utavikuta chumbani kwako. Nilitaka ufanye kama nilivyokuagiza.” Alisema.
“Okay, unataka nini? Nani aliyemuua KK na yule mke mdogo wa KK?” Maswali yalinitoka.
“Hebu acha kuamini mambo ya kuambiwa. Hongera kwa kitabu ulichoandika!” Alisema.
“Nimeandika vingi, unaongelea kipi?”
“SAA 72!”
“Hii ndiyo namna ya kumpongeza mwandishi aliyekuvutia?” Nilisema kwa hasira.
‘Nani kakwambia umenivutia?”
“Sasa hongera ya nini?”
“Kwani nimesema hongera kwa kitabu kizuri?”
“Sidhani umenifanyia yote haya ili kusudi uniambie hongera!”
“Yapi hayo niliyokufanyia?”
“Kunipakazia mauaji ya KK na yule mwanamke pale nyumba namba 511.”
“Nimekwambia usiamini mambo ya kuambiwa na mara nyingine mambo sivyo kama unavyoyaona. Nadhani kama mwandishi uliyeweza kuandika kile kitabu unatakiwa uwe na uwezo wa kujua hilo. Kile kisa kwenye SAA 72 ulibuni tu au ulisimuliwa na mtu?” Swali hili la Chogo lilinifanya nimkumbuke Jacob Matata rafiki yangu. Ndiye aliyenisimulia kisa kile. Lakini kama mwandishi nisingeweza kusema nilisimuliwa na ndivyo tulivyokubaliana na Jacob Matata. Nilimhakikishia kuwa sitatoa siri hiyo. Kama ningefanya hivyo ningekuwa nimetangaza kuwa hafuati kanuni za kazi yake kama mpelelezi.
“Nilibuni tu.”
“Uongo! Huwezi kubuni kwa kusimulia mambo ya ukweli namna ile?” Sasa aligeuka na kuniangalia. Miwani yake myeusi haikuniwezesha kuona mboni za macho yake.
“Sasa kama si..!”
“Namtaka aliyekusimulia!” Alinikatisha kwa sauti kali ya kufoka.
“Ulinisimulia wewe au?” Nilijibu kwa hasira. Jibu langu hilo lilifanya nianze kupata kipigo kikali toka kwa watu watatu waliokuwa ndani ya lile gari.
“Haya niacheni nitasema!”
“Nani aliyekusimulia?”
“Rafiki yangu.”
“Hana jina?”
“An...!” Kauli yangu ilikatizwa na simu ya upepo iliyokuwa ikiita.
“Chogo........Chogo.....Chogo!” Sauti ilisema kwenye simu ya upepo.
“Chogo hapa!” Chogo alijibu taratibu kama hataki.
“Kigi hapa, tumefika Bukoba, yule abiria wangu namwona ameenda kwenye kibanda cha simu na sasa anaongea na simu. Hebu weka mtu afuatilie hiyo simu kapiga kwa nani. Over!” Ilisema ile sauti. Mara moja nikaunganisha hilo jina na yule kijana aliyewaleta polisi sokoni jana. Ambaye niliambiwa kuwa alikuwa amekwenda Kampala. Hii sasa ikawa imenihakikishia kuwa Kigi alikuwa kibaraka wa Chogo.
“Mimi nilidhani mmeshaingia Kampala, mbona muda sana?” Chogo alisema kwa sauti ya kukereka.
“Huyu msichana mtata sana. Anakwenda kwa machale machale tu. Haamini jambo lolote, naomba tu Mungu nifike.”
“Sasa unaweza kuniambia jina la hicho kibanda au alama yoyote ili mtu wetu aweze kufuatilia hilo?” Chogo alisema.
“Ndiyo, naweza kusoma maandishi ya hicho kibanda, kimeandikwa, CHINGA BOY MAPHONE, kiko jirani na ofisi za Posta hapa Bukoba mjini. Amemaliza anarudi, wacha niendelee na kazi. Over!” Simu ikakatwa.
“Niwie radhi kwa usumbufu.” Alisema huku akijiweka vema.
“Huyo rafiki yako ni nan...” Hakumalizia tena swali lake lile, simu ya upepo iliunguruma tena.
“Chogo....Chogo....Chogo...!”
“Chogo hapa!”
“Zoazina hapa...niko uwanja wa ndege naona jamaa yako kawasili. Fanya mipango haraka, yule fala Japhet yuko wapi?” Sauti ya kike ilisema. Niliweza kuitambua ile sauti kuwa ni ya yule mwanamke aliyeniletea chakula asubuhi pale Kituo cha Polisi. Duuuh! Hawa watu kuna kitu wanafanya na sijui lengo lao ni nini. Huyo mtu wanayemwongelea sijui ni nani na msichana wanayemwongelea sijui ni yupi. Sijui mimi nahusika vipi sasa?
“Habari njema, tumefanikiwa. Japhet niko naye hapa ndiyo nilikuwa nataka kumhoji. Ila nitampeleka sehemu salama kwa usalama wake hadi tumalize kazi. Over!” Chogo alisema kwa sauti ya furaha.
“Twende Kilindini tukamweke huyu.” Alisema na wakati huo huo wale watu wawili walinifunga mikono na kisha wakanifunga kwa kitambaa cheusi usoni. Nikasikia tu gari likigeuzwa na kupelekwa kwa kasi sana.
“Hebu mpeni simu yake aongee na mkewe. Hebu mwambie mkeo kuwa unaendelea vema na kuwa ulikuwa umeibiwa kila kitu sasa umenunua simu mpya.” Sauti ya Chogo ilisema. Nilisikia mlio wa simu, nikautambua kuwa ni mlio wa simu yangu unapoiwasha.
“Umesevu vipi jina la mkeo?” Jamaa mmoja aliuliza.
“Pumzi yangu ya Mwisho.” Niliposema hivyo nikasikia wote wakicheka.
“Fala kweli wewe!” Chogo alisema, nilikuwa nimeshaikariri sauti yake. Simu iliita halafu nikaisikia sauti ya mke wangu.
Nilisikia uchungu sana aliposema, hallo mara ya tatu, mimi nikiwa kimya kabisa.
“Hello honey, hujambo?” Nilisema huku nikijilazimisha kutoa sauti ya uchangamfu
“Mbona hivyo sasa, kuna nini Japhet?” Si kawaida ya mke wangu kulalamika, lakini alishahisi kuna shida.
“We acha tu, ila nashukuru niko mzima!” Nilisema.
“Una maanisha nini?”
“Kigoma si ilinipokea. Hapa ndiyo nimetoka benki wamenipa kadi mpya ya benki, nimenunua simu kukupigia.” Nilidanganya huku moyo ukiniuma kumwongopea mke wangu.
“Mbona sikuelewi, hebu nielezee vizuri, maana siku hizi mbili nimekuwa naishi kwa mashaka makubwa sana!” Alisema.
“Nilipofika tu si nikaibiwa kila kitu, halafu nikiwa kama mgeni wa hoteli nikahusishwa na wizi hivyo nikawekwa ndani. Sikupata hata muda wa kukutaarifu, nilipotoka sikuwa hata na pesa na kadi yangu ya benki iliibwa vilevile. Hivyo ikabidi nitembee kwa miguu hadi benki ili kuomba kadi nyingine. Process imechukuwa muda mrefu kwa vile sikuwa na kitambulisho chochote. Ila sasa ndiyo nimepata kadi na nimeweza kuchukua pesa. Hamjambo huko?”
"Duuh! Afadhali, yaani kidogo nichanganyikiwe, ila kuna sauti ilikuwa inaniambia uko salama. Kwa hiyo yule mwendawazimu umeshamwona? Uko salama sasa? Lini unarudi?” Aliuliza maswali mengi sana.
“Nitakupigia baadaye siko sehemu nzuri sasa hivi.” Nilisema.
“Sawa, nimefurahi kusikia uko mzima.” Alisema.
“Take care!” Nilisema halafu nikakata simu. Nilijua lile neno, ‘take care’ lingetosha kumwambia kuwa nilikuwa nimebanwa kwa namna fulani. Nilinyanganywa simu ikazimwa.
“Lengo lenu ni nini!?” Niliuliza.
“Tutakuachia kesho urudi Arusha” Chogo alisema.
“Kama sitaki kurudi?”
“Tutakuua!” Chogo alijibu bila kufikiria.
Kauli hiyo ya Chogo ilinifanya nitulie kabisa. Kipigo nilichokuwa nimepata toka kwa wale jamaa watatu ambao walionekana kuwa watiifu kwa Chogo na kuwa tayari kufanya chochote alichowaamuru sikuwa tayari kuona nakipata tena. Hivyo nikaona njia sahihi kwangu ni kutulia na kungojea hatma yangu. Nilishabaini kuwa usumbufu wowote toka kwangu ungepelekea kipigo zaidi na maamuzi yasiyotarajiwa toka kwa Chogo.

Ukweli ni kwamba nilikuwa na hasira sana. Halafu kwa mbali nikawa nasikia kichwa kinauma. Kwa vile nilikuwa nimefungwa kitambaa usoni sikuwa na namna ya kuona tulikuwa tukielekea upande gani. Nilituliza mwili wangu ili hali akili ikiwa inazunguka vibaya sana. Niliwaza hili na lile, nikatamani ingekuwa hivi na vile. Nikakumbuka kusali, lakini moyo wangu ulikuwa umejaa mashaka makubwa kiasi kuwa maombi yangu hayakuwa na hata punje ya imani.
Nilimuwaza mke wangu, ingekuwaje pindi angepiga tena na kukuta siko hewani.
Sijui kwa nini nilimdanganya?
Kuokoa maisha au? Lakini inawezekana nilimdanganya kwa vile nampenda maana ningemwambia ukweli labda angefunga safari kuja kunitafuta. Mwishowe na yeye angetumbukia kwenye janga hili. Hapo nilijifariji kuwa nilifanya kilichostahili kwa ajili yake na yangu pia.
Nilimfikiria yule mwendawazimu.
Je, ni bahati mbaya kuwa ametokea kwenye ule mtaa wa nyumba namba 511?
Hapana!
Si bahati mbaya.
Labda alikuwa amerudi kufata kile kitu chake chenye umbo kama filimbi ambayo hutumiwa na mwamuzi wa mpira wa miguu? Inawezekana! Nilijijibu mwenyewe.
Inawezekana alipata kuingia kwenye ile nyumba, lakini ikawaje akadondosha ile filimbi?
Je, inawezekana aliona ile maiti ya mke mdogo wa KK?
Huyu mwendawazimu ni nani hasa?
Je, inawezekana akawa anajisingizia kuwa mwendawazimu?
Kitabu changu je, kwa nini hataki kukiacha katu!?
Maswali yalimiminika kichwani. Halafu nilipofikiria kitabu changu cha riwaya, mara nikakumbuka maswali ya Chogo. Anataka kumjua mtu aliyenisimulia kisa kile. Inaonekana hilo ndiyo jambo kubwa alilokuwa akilitaka toka kwangu.
Je, ni kweli kuwa misukosuko yote aliyonipa lengo lake ilikuwa ni kunilazimisha nimtajie aliyenisimulia kisa kilichoko kwenye kile kitabu? Sasa mbona ameacha kunihoji baada ya kuambiwa kuwa kuna mtu amewasili na ndege? Mtu huyo ni nani? Kama hanihitaji basi si anichie sasa?
Kuna uhusiano gani wa kuja kwa mtu huyo na yeye kuacha kunihoji hadi akasema hawanihitaji tena ila wataniweka sehemu salama hadi wamalize kazi.
Kazi gani?
Wananiweka sehemu salama. Ina maana wao wanataka niwe salama au? Au labda kweli wao ni watu wa usalama. Kichwa changu kilijaa maswali mengi sana.
Nilimuwaza KK.
Nikamuwaza Kigi Mbonea. Halafu nikafikiria maelezo yake aliyompa Chogo juu ya msichana wanayesafiri naye. Msichana hatari sana! Hilo likawa fumbo jingine.
Nikamuwaza askari mwenye nyota tatu.
Mawazo yangu yaligutuliwa na honi ya gari. Ilikuwa ya gari hili tulilokuwemo. Sasa niliweza kusikia na kuhisi kuwa gari lilikuwa limesimama. Niliweza kusikia geti likifunguliwa.
Gari ikaingia ndani.
Nikasikia vishindo vya watu wakitembea nje ya gari na wakati huo huo geti likafungwa.
“Mfungueni mumuweke kwenye chumba salama. Mpeni mahitaji yake yote. Hakikisheni anapata muda wa kuongea na mke wake chini ya usimamizi. Akikosea tu kuongea na mke wake, atakufa yeye na mke wake pia. Tukimaliza kazi tutamwachia aende zake.” Chogo alisema kwa sauti huku sasa akiwa ameshashuka garini. Sauti yake ilizidi kusikika tokea mbali kadiri aliyokuwa akiongea. Inamaanisha alikuwa akiongea huku akitembea, labda kwenda ndani. Ilikuwa wazi kuwa maelezo yake alilenga yasikiwe na mimi na vijana wake.
Nilifunguliwa mikono na kuondolewa kitambaa usoni. Nilifikicha macho kwa nukta chache halafu nikaweza kutazama.
“Twende!” Nilipewa amri huku nikisukumwa.
Nikatembea kwenda mbele. Tulikuwa kwenye nyumba kubwa iliyokuwa imezungushiwa ukuta mkubwa. Huko nje, juu, niliweza kuona miti mingi sana na ndege waliokuwa wakiimba na kuruka. Bila shaka ilikuwa nyumba iliyokuwa pembeni ya mji. Niliweza kusiki sauti ya mawimbi ya maji. Hilo likaniambia kuwa tulikuwa pembezoni mwa ziwa Tanganyika.
“Hapa ni sehemu ya chakula. Saa moja na nusu utakuja hapa kwa ajili ya chakula, asubuhi saa moja na nusu kwa jili ya kifungua kinywa, mchana saa saba kamili kwa ajili ya mlo wa mchana.” Alisema yule mtu huku akinionyesha kwa mkono. Sasa tulikuwa ndani ya jumba hilo ambalo ungeweza sema ni kama hoteli tu.
“Utatumia chumba hiki, humo utakuta mahitaji yako yote.” Alisema yule mtu wakati akinionyesha chumba namba 81.
“Twende huku nikuonyeshe maeneo mengine!” Aliniamuru.
Niligeuka kumwangalia usoni, halafu nikageuka haraka kuangalia tulikokuwa tukielekea.
Sikutamani kumwangalia tena usoni.
Uso wake ulinifanya nikose hamu ya kumwangalia.
“Hapa ni sehemu ya mazoezi na pale kwa ajili ya kuogelea na kupumzika. Uwe raia mwema hadi utakapotoka. Hicho ndiyo kitu pekee ningeweza kukuambia. Usijaribu ujinga, kama unabisha nenda chumba namba 00 utapata majibu ya nini huwa kinatokea kwa watu wajingawajinga. Maisha mema!” Aliposema hivyo tu akaanza kutembea haraka kwenda upande mwingine. Nilimsindikiza kwa macho hadi alipoingia kwenye mlango uliokuwa kwenye kona upande wa kushoto.
Sijui kwa nini nikajikuta napata hamu ya kwenda kuangalia alikuwa ameingia wapi. Hivyo nikatembea kufuata alipokuwa ameingia. Nilipousogelea mlango ndipo nikakutana na maandishi, ‘WAGENI HAWARUHUSIWI KUINGIA.’ Akili ikaniwasha, kiu ya kutaka kuchungulia ikanishika. Nikagusa kitasa cha mlango ili nifungue.
Nikakinyonga huku moyo ukipiga kwa kasi.
Halafu nikasiki sauti ndogo akilini ikiniambia ‘huwa unajitafutia matatizo wewe mwenyewe!’
Nikasita baada ya sauti hiyo.
Lakini kiu ikaongezeka zaidi, nikataka nione.
Nikashika tena kitasa na kukinyonga taratibu.
Mlango ukafunguka.
Sikutaka ufunguke sana, nilipoona umeachia nafasi ya mimi kupenyeza macho, niliacha kuusukuma, nikajisogeza ili nichungulie. Nikachungulia.
‘Loooh!’ Nilinong'ona kwa mshangao, halafu nikauachia mlango kwa hofu iliyoletwa na kile nilichokiona. Kitendo cha kuuachia mlango ukajibamiza. Niligeuka ili nikimbie kuelekea kwenye chumba nilichoelekezwa kuwa ndiyo ningekaa.
Ile nageuka tu nikajikuta najibamiza kwenye mwili wa mtu aliyekuwa nyuma yangu. Niliinua mcho haraka kumwangalia.
Duuuh, bonge la mtu! Refu jeusi, ndevu nyingi, zimepakwa rangi nyekundu. Mijicho yake sasa!
Liliniangalia tu bila kusema kitu.
Bastola mkononi.
Lilikuwa limevaa kaptula iliyolibana kiasi kuwa ramani ya sehemu zake za siri ilionekana vema. Mabuti makubwa na fulana iliyopwaya lakini bado niliweza kuona kifua chake kipana na misuli utadhani mcheza mieleka John Cena, ila yeye huyu alikuwa mrefu mweusi.
“Uliambiwa ufuate maelekezo ya kuishi humu. Sivyo?” Sauti yake ilivuma kama radi. Nzito ya baridi sana, yenye vionjo vya uovu.
“Samahani sana!” Nilisema huku nikitetemeka.
“Kwa sababu ni wewe naipokea mara moja tu. Angalia pale!” Lilisema huku likionyesha kidole darini.
Niliangalia lilipoonyesha.
Kamera ya usalama!
“Tunaona kila kitu, cha ushenzi wako, tulia uondoke salama ukatuandikie vitabu vingine tuburudike. Usitake kuwa riwaya wewe mwenyewe.” Liliposema hivyo, Jamaa hilo lilianza kutembea kuondoka.
Ukweli sikuwa na nguvu zilizosalia kufanya chochote. Nilichokiona nilipochungulia na nilipojigonga kwa hili jamaa vilitosha. Onyo lake lilikuwa madhubuti kutosha kueleweka na kufuatwa na yeyote anayependa maisha kama mimi. Nilitembea kuelekea upande ambao chumba changu kilikuwepo. Safari hii nikiwa najua kuwa natazamwa kila ninachofanya.


Nilizungusha kitasa cha mlango namba 81, nikasukuma mlango, ukafunguka. Nikajikuta nimeingia kwenye chumba kimoja kizuri. Kizuri kiasi kuwa sikutegemea. Naweza kusema kuwa kulikuwa na kila kitu ambacho ningekihitaji. Mavazi, vitu vya usafi, jokofu moja dogo lilikuwa na vinywaji na matunda kadhaa. Meza moja ya kusomea iliyokuwa na kompyuta. TV kubwa yenye mashine ya kuweka DVD ili kuangalia picha. Halafu pembeni kulikuwa na DVD nyingi za filamu za aina mbalimbali. Lakini nikaamua nianze na kuoga kwanza. Niliangalia saa yangu ilikuwa inaingia saa kumi na mbili jioni, zilisalia dakika ishirini tu.
Wakati huu nilisia kichwa kinaniuma sana.
Safari hii ya Kigoma sitokaa niisahau maishani mwangu.
Kwanza ni ile sababu ya kusafiri, pili kinachonipata sasa.
Bila shaka nitaandika kitabu kuhusu safari hii.
Sijui kitabu nitakiita, SAFARI YENYE MASHAKA au MWENDAWAZIMU ALIYENIFANYA MWENDAWAZIMU au hata PATAPOTEA.
Niliwaza hayo nikiwa bafuni navua nguo tayari kwa kuoga.
Wakati navua chupi ndipo kile kitu kama filimbi nilichokiokota nyumba namba 511 kilianguka chini.
Nilikiokota na kuanza kukichunguza. Nikashikwa na mshangao. Haikuwa filimbi kama nilivyodhani. Ilikuwa ni flash disk.
Mwendawazimu alikuwa anamiliki flash disk!
Tena kwa namna alivyoithamini hadi akaifunga shingoni ili isipotee. Hilo likanishangaza. Kama kawaida yangu, ile hali ya udadisi ikanivaa tena. Nikataka kujua kulikuwa na nini kwenye flash disk ile.
Nikiwa uchi, nilitoka bafuni huku nikiwa nimeshika flash disk. Nilikuwa nimeikumbatia kwenye kiganja. Nikapiga hatua kuelekea ilipokuwa kompyuta.
Lakini ghafla nikasita.
Nikakumbuka maelezo ya lile jamaa liliponiambia, 'angalia ile'.
Nikajikuta nainua macho na kuanza kuangazaangaza darini ili kuona kama kulikuwa na kamera ya usalama.
Haikuwepo.
Hivyo nikawasha kompyuta. Wasiwasi wangu ulikuwa kama kungekuwa na uhitaji wa neno la siri ama wazungu husema 'password'. Nilipofika sehemu ya kuweka neno la siri, hapakuniuliza kuweka neno la siri, hivyo ikawa imewaka bila shida.
Haraka nikachomeka ile flash.
Macho kodo kwenye kioo cha kompyuta kuona nini kilikuwa kwenye flash ya mwendawazimu, Kumbamasaka Jitu la Watu. Nilipoifungua nikakuta kulikuwa na picha nyingi za video. Flash ilikuwa kubwa sana, ilikuwa na ukubwa wa GB 120. Kuona hivyo kiu yangu ikaanza kwisha japo nikabaki na swali kichwani. Mwendawazimu alikuwa anaangalia filamu? Alikuwa anaitumiaje ile flash?
Hivyo nikaendelea kuangalia majina ya zile filamu huku nikizidi kuishiwa hamu ya kuangalia. Kichwa kilizidi kuniuma kwa sababu ya mwanga wa kompyuta. Wakati nataka kufunga ile flash mara macho yangu yakavutwa na jina la filamu. Filamu ilikuwa imeandikwa SAA 72.
Macho yalinitoka, haraka nikabonyeza kufungua hiyo filamu.
Nilitulia tuli kuangalia.
“Shiiit!” Nilitamka.
Haikuwa filamu kamili, ilikuwa vipande vya matukio vilivyounganishwa. Ila picha zilikuwa safi kabisa na matukio yakionekana vema.
Sasa naelewa vema hawa watu wanajuana tokea mbali.
Niliangalia tena na tena.
Nilijiridhisha kuwa nilikuwa kwenye moja ya tukio la kutisha sana. Nikasahau shida zangu zote. Akili ikakimbia haraka kumfikiria Jacob Matata.
Isije kuwa ndiyo mtu aliyewasili jioni hii, kama ndiyo basi uwezekano wa kupona utakuwa mdogo sana. Nilihitaji nipate nafasi ya kumtaarifu haraka kuwa yuko hatarini.
Sistahili kuwa na hii flash, maana ikigundulika nami nitauawa.
Niliichomoa haraka na kutembea kwenda bafuni. Nilisimama ile sehemu ya chooni halafu nikaitumbukiza kwenye tenki la maji ya kuflashia choo.
Moyo ulikuwa ukipiga kwa kasi.
Moyo wangu na nafsi vilihamanika sana.
Nikafungua maji tayari kwa kuanza kuoga. Nilipoanza kuoga, nikiwa tayari nimejipaka sabuni kichwani mlango wa chumba uligongwa.
“Naniii!” Nilisema kwa sauti.
“Muda wa chakula!” Sauti ya kike ilisema.
“Asante. Naja!”
Nilimaliza kuoga nikaelekea sehemu niliyoambiwa kuwa ni ukumbi wa chakula. Sikukuta mtu nilipoingia na wala sikuacha mtu nilipotoka. Ilinishangaza japo chakula kilikuwa kingi vyomboni. Ina maana wanaotarajiwa kula ni wengi. Sikutaka kudadisi hilo. Akili yangu ilikuwa bado kwenye filamu niliyoiona. Filamu hiyo ilibadili mtazamo wangu kuhusu yule mwendawazimu, Chogo na askari mwenye nyota tatu.
Nilipoingia chumbani nilianza kusikia kizunguzungu na kichwa kikawa kinaniuma vibaya sana. Upande wa mbele wa kichwa ungedhani kuwa unadondoka kwa jinsi kilivyokuwa kikiuma. Haraka nikaanza kuangaza kama kungekuwa na boksi la huduma ya kwanza kwenye kile chumba.
Naam nililipata!
Nikafungua harakaharaka.
Hola!
Hakukuwa na dawa, bali kulikuwa na maandishi tu yaliyosomea; 'MWITE MUUGUZI PIGA 990'.
Nikaliweka chini na kuinua kichwa. Mwanzoni sikuwa nimejua kuwa kungekuwa na simu mule chumbani. Nilipoangaza niliiona ikiwa pembeni ya meza ya TV. Badala ya kumpigia muuguzi nilibonyeza namba za mke wangu.
Hola!
Simu haikuwa inatoka nje, ilikuwa ni kwa matumizi ya ndani ya jengo lile. Nikarejea kwenye wazo la asili, nikabonyeza 990. Simu ikaita, haikuchukua sekunde nyingi ikapokelewa.
“Nakuja, uko 81 sivyo?” Sauti nzuri ya kike ilisema.
“Ndiyo!’ Nilijibu. Simu ikakatwa.
Niliweka simu chini na kujikuta nimezama kwenye fikra. Nikaanza kuhisi kama tumbo linakata hivi. Nikajua hiyo ilitokana na wasiwasi na hofu niliyoipata baada ya kuangalia ile filamu.
Mlango wa chumba changu uligongwa.
“Ingia!” Nilisema. Mlango huu ulikuwa na kitasa lakini hakukuwa na ufunguo. Hivyo nisingeweza kujifungia ama kufunga malango.
Aliingia msichana aliyekuwa amevaa mavazi meupe.
“Habari yako mgeni wetu?” Alisalimia.
Sikujibu, nikabaki namwangalia tu. Nilimfananisha.
“Nzuri japo si sana!” Nilisema.
“Najua, ndiyo maana niko hapa. Ulipiga simu uuguzi sivyo?”
“Ndiyo!”
“Haya sema nikusaidie nini?”
“Unaitwa nani vile?” Badala ya kusema alichotarajia nilimuuliza swali. Bado nilijikuta naamini kuwa sura ile haikuwa ngeni kwangu.
“Sidhani kuwa ndicho kilikufanya upige simu?” Alisema kwa sauti ya msisitizo.
"Viva...Viva Davis...Ivumwe High School siyo!” Nilisema huku nikiwa nakunja uso na kuminya macho kama ishara kuwa nilikuwa navuta kumbukumbu ya mbali sana.
“Mmmmh, yeah wewe si Japhet Sudi, ulikuwa Mwenyekiti wa CASFETA?” Hatimaye alisema ila kwa kunong'ona.
“Ndiyo!” Nami nikajikuta nanong'ona bila kujua sababu hasa.
“Umefikaje humu?”
“Kwani hapa ni wapi?” Niliuliza badala ya kujibu
‘Kituo maalum cha usalama.” Alisema.
"Mmmmh!”
“Umekosea nini?” Aliuliza.
‘Sijakosea ila nimezushiwa!”
“Mmmmh!” Aliguna huku akiniangalia kwa macho ya udadisi.
“Haya sema nini kilikufanya upige simu. Maana hapa tunaangaliwa tusije shitukiwa, jifanye hunijui.” Alinitahadhairisha.
“Lakini si hamna kamera hapa.”
“Zipo. Sema unaumwa nini?” Sauti yake ilibadilika.
“Kichwa na nasikia tumbo limevurugika vibaya.” Nilisema huku sauti ikionyesha wazi kuwa sikuwa nimeridhika kukatishwa yale maongezi mengine.
“Hebu lala hapa.” Alisema.
Nikalala kitandani.
“Lala chali!”
Nikatii.
“Okay, nitakupa dawa za maumivu. Halafu...” Alisema huku akiwa kama ananiminya minya shingoni, hivyo akashuka hadi kwenye suruali.
“Naweka hii kalamu na karatasi utaniandikia maelezo yako, fanya hivyo ukiwa bafuni. Baada ya saa mbili nipigie tena nitakuja kukuona. Saa nne usiku zamu yangu inaisha anakuja mwingine mimi nitapelekwa nyumbani.” Alisema hivyo, halafu nikahisi ameweka kitu sehemu zangu za siri.
“Usijifanye mjanja, ukienda chumba namba 00 utaona!” Alisema. Akainuka na kufungua pochi yake ya dawa. Alitoa vingonge kadhaa vya maumivu na kunipatia.
Niliinuka, kwanza nikaywa dawa, wakati huo yule Muuguzi akawa anatoka mule chumbani. Baada ya kunywa dawa nilielekea bafuni. Niliona hiyo kama nafasi ya kuzitoa habari zangu nje ya kifungo.
Maswali mawili yalikuwa kichwani wakati nikiwa nimeshika kalamu na karatasi. Swali la kwanza; kwa nini nimwamini huyo msichana? Pili; niandike ujumbe gani na nimwombe anisaidieje katika janga hili?

Baada ya kufikiri sana juu ya maswali hayo, mwishowe niliona kuwa sikuwa na cha kupoteza. Nisipoandika rafiki yangu Jacob Matata angekuwa hatarini. Baada ya kuona ile filamu nilijikuta naamini kuwa yeye ndiye mtu waliyesema amewasili. Niliweka kalamu juu ya karatasi. Mkono ulikuwa unatetemeka, hivyo kalamu nayo ikawa inatingishika.
Niliandika mstari wa kwanza; Nimetekwa nahitaji msaada.
Lakini nikaufuta. Nikaandika mstari wa pili. Nao nikaufuta.
Nikajikuta nimeandika mistari saba ya mwanzo na kuifuta.
“Lengo langu ni nini?” Nilijikuta nasema kwa sauti ya chini.
Kujiokoa?
Hapana.
Kumsimulia yule muuguzi tukio zima?
Hapana hiyo haitosaidia.
Kumwokoa Jacob Matata?
Hapana ila natamani nimsaidie.
Okay, sasa ngoja niandike kumsaidia, nikimsaidia yeye naye atanisaidia mimi.
Nikakata shauri.
Kalamu ikaiangalia karatasi.
Nikaandika:

NENDA NZIMANO HOTELI, MWAMBIE NEEMA AMPIGIE MKE WANGU KWA NAMBA NITAKAZOWEKA NYUMA YA KARATASI HII. NEEMA AMWAMBIE MKE WANGU AMWAMBIE JACOB MATATA KIGOMA KUNA HATARI KUBWA, MABAKI YA ILE RIWAYA SAA 72 YANAMNGOJA. KAMA AKIJA AJE KIKAZI.
NIMESHIKWA MATEKA.
JAPHET.

Niliyasoma tena maneno niliyoandika. Nilitaka kueleza zaidi, lakini sikuona kuwa ni salama. Sikutaka kujiachia sana kwenye hiyo karatasi. Lakini kama Neema akiamua kuwa upande wangu, atafanya nilivyomuomba. Bila shaka atataka kumjua vema aliyempa karatasi hii. Sikutaka kuweka wazi mambo yote kwenye karatasi, hasa yale niliyoyaona kwenye ile flash.
Niliificha ile karatasi na kutoka bafuni. Nilijilaza kitandani nikisubiri muda nilioshauriwa. Kitandani hapo nilijifanya mgonjwa kwelikweli. Baadaye nilipiga simu na kuomba msaada wa mwuguzi tena.
Alikuja na tukaanza kufanya kama mgonjwa na tabibu.
“Umeandika?”
"Ndiyo, maneno machache sana, naomba uipeleke usiku huu.” Nilisema huku kwa siri nikimkabidhi ile karatasi. Baada ya muda alianza kuondoka.
“Subiri kidogo!” Nilisema halafu nikasimama na kuelekea bafuni. Dakika chache baadaye nilitoka na kukuta Viva akiwa ameinama akijifanya kupanga vitu kwenye kibegi chake cha matibabu.
“Nahisi maumivu hapa mgongoni!” Nilisema huku nikijilaza kitandani. Alisogea na kujifanya kuinama ili kuiniangalia.
“Sema!”
“Naomba ukampe hiyo.” Nilisema huku nikimshikisha mkononi ile flash ambayo ilikuwa imelowa maji.
“Ni nini?”
“Kampe huyo Neema, mwambie kama akifanikiwa kuonana na Jacob Matata ampatie.” Nilisema na kugeukia upande mwingine. Machozi yalikuwa yananitoka.
Viva aliniangalia kwa muda halafu akaondoka mule chumbani.
Nami nilitoka mule chumbani na kuamua kuzunguka zunguka ndani ya jumba hilo.
Katika zungukazunguka zangu ndipo nikabaini kuwa jumba lile ilikuwa kubwa sana na kulikuwa na ulinzi wa kutisha. Mara nikajikuta nimepita mbele ya chumba namba 00, nikakumbuka kuwa kama nataka kufanya unjanja niangalie chumba hicho kwanza.
Lile jamaa refu liliniambia.
Viva naye alitumia chumba hicho kama njia ya kunionya kutotaka kufanya ujanja wowote.
Nilipokuwa mbele ya chumba hicho ndipo nikapata hamu ya kuangalia kulikuwa na nini ndani ya chumba hicho.
Kama waliniambia niangalie ilimaanisha nilikuwa na ruhusa ya kuangalia.
Bila shaka ina maana hiyo, nilijiridhisha nafsi yangu.
Na sasa nikawa mbele kabisa ya mlango namba 00.
Nilishika kitasa nikakinyonga, mlango ukafunguka.
Sikutaka kuingia, nilichungulia tu.
“My Jesus, what the hell is this!?” Niliubamiza mlango nikaufunga na kutembea haraka kuelekea kilipokuwa chumba changu.
Nilisikia kichefuchefu na uchungu kwa wakati mmoja.
Chumba kile kilikuwa kimejaa mafuvu ya vichwa vya watu. Lakini kulikuwa na vichwa kama vitatu hivi ambavyo ama vilikuwa vimewekwa siku za karibuni au vilikuwa katika hatua ya kuoza. Hali hiyo ilipelekea harufu kali kutoka kwenye kile chumba. Kwa haraka naweza kusema mafuvu yalikuwa zaidi ya ishirini hivi.
Niliuvamia mlango wa chumba nilichopewa kwa fujo.
Niliingia na kupitiliza bafuni ambako nilianza kutapika.
Hali ilipotulia nilirejea chumbani na kujilaza kitandani. Ukweli sasa nilikuwa najiona kama niko jehanamu. Nilikuwa mikononi mwa watu katili kuliko nilivyodhani. Sasa nikakumbuka kile nilichokiona wakati ule naingia ndani ya jumba hili. Wakati nilipochungulia kwenye mlango ulioandikwa ‘WAGENI HAWARUHUSIWI KUINGIA’. Nilivyoona wale watu ambao ningesema ni kama majitu yakiwa na silaha nzitonzito yakiwa yamejipumzisha pembeni ya bwawa la kuogelea tofauti na bwawa ambalo mimi nilionyeshwa. Niliendelea kuwaza hivyo hadi nikapitiwa na usingizi mzito sana.

****

Siku iliyofuata ilikuwa ngumu. Lakini nilikabiliana nayo kwa kuwa mpole tu na muda mwingi kushinda ndani ya chumba nilichokuwa nimewekwa. Tofauti na jana, siku hii kulikuwa na muuguzi mwingine tofauti na Viva Davis. Hivyo sikuweza kupata mrejesho.
Jioni ya siku hii nayo ikaingia. Na hatimaye nikaingia kitandani kulala. Yalikuwa ni maisha ya upweke na mashaka makubwa. Bora kuwa Kituo cha Polisi ambapo unajua kosa lako kuliko kuwa umeshikiliwa hivi huku hujui kosa wala hatima yako.
Nikiwa usingizini nilihisi kama mlango wa kile chumba umefunguliwa. Lakini usingizi ulikuwa mzito sana nikapotelea usingizini tena.
Nlishituka usingizini, nikarukia pembeni ya kitanda.
Nilikuwa nimepigwa na kitu, kwa vile nilikuwa usingizini sikujua ni nini. Hivyo nilipotua pembeni ya kitanda kofi zito lilitua usoni kwangu. Ndipo sasa nikajua kuwa kilichoniamsha lilikuwa kofi. Mwanzoni nilishindwa kupambanua kuwa lilikuwa kofi au kipande cha ubao mpana.
“Tulia shenzi wewe, acha kurukaruka utadhani choroko za kiangazi zinavyochemka sufuriani!” Sauti ilisema.
Mara moja niliitambua sauti hiyo.
Kwa hofu nikajikuta nimekaa sakafuni.
“Utaondoka hapa, huyo malaya wako anajifanya mjanja sana. Ila unatakiwa ujue mambo mawili. Umeua. Umeua watu wawili. Ushahidi tunao, jalada lako liko polisi. Ukijifanya kuondoka Kigoma na kusemasema ovyo basi ujue utafia jela. Mchukueni mumpeleke!” Sauti ya Chogo iliongea. Sikupewa hata nafasi ya kuongea, nikabebwa juujuu na mikono yenye nguvu. Chumba kilikuwa giza, sijui kwa nini hawakutaka kuwasha taa. Wakati nahangaika kwenye mikono hiyo huku napiga kelele za hofu, niligundua kuwa ilikuwa mikono miwili tu lakini ilikuwa imara kama chuma. Mikono mizito, minene, yenye mishipa minene.
Nyumba yote ilikuwa giza.
Sikuweza kujua ilikuwa saa ngapi.
Nilitolewa hadi nje kabisa ya jumba. Nje ndipo nikakutana na taa za nje ya nyumba.
Kwa mbele upande wa kushoto niliweza kuona gari likiwa limewashwa taa tayari. Lilikuwa ni lile lile Nisan Safari. Nilijitahidi kuangalia namba za lile gari, ndiyo nilifanikiwa kuzinakili kichwani mwangu. TX086AAB.
Nilitupiwa upande wa nyuma wa gari.
“Aaaaah shiii!” Nililalamika maumivu.
“Zingatia uliyoambiwa wewe unasikia!?” Jamaa lilisema na mlango ukafungwa. Gari likaondolewa.
Baada ya mwendo wa muda kidogo, mara nikasikia gari linapunguza mwendo. Mlango ukafunguliwa.
“Shuka!” Niliamriwa.
Nikatii. Nikaangaza macho huku na huko. Eneo hili ilikuwa ni mbele ya Hoteli Nzimano. Jamaa hakutaka kupoteza muda aliingia ndani ya gari na gari likaondolewa kwa kasi. Nilijua ilimaanisha nini. Nilitembea kuelekea ndani ya hoteli.

Baada ya maswali mengi toka kwa mlinzi na yule dada wa mapokezi, Neema, hatimaye niliingia kwenye chumba changu. Nilijiona kama vile niko ndotoni.
Niliangaza macho mule chumbani, nikajitupa kitandani. Nilijaribu kujinyoosha. Mwili ulikuwa umechoka sana.
Mara macho yakanitoka. Kutazama nikaona vitu vyangu vyote ambavyo vilikuwa vimeibiwa vilikuwa vimewekwa sakafuni, ikiwa ni pamoja na begi.
Mshangao mwingine huo! Nikisema najiona niko ndotoni tafadhali unielewe. Maana mambo mengine si rahisi kuamini kuwa yanatokea katika ulimwengu wa kawaida, tena yakiwa yamepangana kwa namna haya yalivyokuwa yamepangana.
Nilienda nikachukua simu yangu.
Ilikuwa imewashwa. Nikaangalia saa kwenye simu, ilikuwa saa tano na nusu usiku.
Niliona nimpigie mke wangu ambaye nilikuwa na hakika alikuwa amejaa wasiwasi. Nikampigia tukaongea, hapo ikabidi nimwelezee hali halisi. Yeye akanishauri nirudi Arusha haraka.
Ukweli sikuwa najua nini kinaendelea sasa. Toka kule nilikokuwa nimetekwa hadi kwenye chumba cha hoteli, huku vitu vyangu vikiwa vimerejeshwa ilinishangaza sana.
Nikaanza kufikiria nini nifanye sasa. Wazo la kutoroka Kigoma na kurudi zangu Arusha lilizitembelea fikra zangu. Wazo hili lilipingwa na ukweli kuwa sikuwa na namna zaidi ya kubaki Kigoma. Sikuwa na namna kwa sababu ya kesi ya mauaji iliyokuwa inanikabili. Nikatulia kitandani nikiwa nawaza hilo kwa kina. Hapana lazima niondoke Kigoma, nikifika Arusha nitakwenda kujisalimisha mwenyewe Kituo cha Polisi. Wakati nilipowaza hili ndipo nikamkumbuka Jacob Matata.
Haraka nikatafuta namba yake kwenye simu.
Nilipoiona nikapiga.
“Namba unayopiga kwa sasa haipatikani.”
Nikakata na kupiga tena.
“Namba unayopiga kwa sasa haipatikani.”
Nikakata.
Naondoka. Acha nione kama nitaweza kupata tiketi muda huu. Nilijisemea na kuinuka toka kitandani. Niliweka vitu vyangu kwenye begi. Nikabadilisha nguo na kutoka mule chumbani.
Kutoka chumbani kwangu nikawa natembea harakaharaka kuelekea upande wa mapokezi. Ni wakati napita mojawapo ya vyumba ghafla nikashitukia nimevutwa na kuingizwa kwenye chumba kimoja.
Shabashi! Moyo ukalia paaaaah, nini hiki tena!
“Tulia tulia, ni mimi Neema!” Ilikuwa ni sauti ya Neema.
Chumba kilikuwa giza totoro.
“Washa taa sasa!” Nilisema kwa sauti.
“Shiiiiii, ongea kwa sauti ya chini. Ameondoka!” Neema alisema.
“Unamaanisha nini? Nani?” Niliuliza kwa sauti ya chini safari hii.
“Jacob Matata, alikuja ila anasema amepata dharura, ameondoka kwa ndege ya kukodi!” Neema alisema kwa sauti ya chini.
“Ulipata ujumbe wangu?” Niliuliza.
“Upi?”
“Nilimtuma Viva…!”
“Yes, niliupata. Bahati mbaya msichana ameniletea ujumbe wako wakati Jacob Matata akiwa ameshaondoka. Nimejaribu kumpigia simu hapatikani. Ila ujumbe wako ulinifanya nibadili mawazo!” Neema alisema.
“Kubadili mawazo?”
“Ndiyo, nimemwona Jacob Matata nilikuwa naye usiku uliopita, nimejikuta nashawishika kukusaidia katika suala hili. Japo hakutaka kuniambia chochote kuhusu wewe wala kilichomleta hapa Kigoma ila baada ya ule ujumbe uliompa Viva sasa najua kuwa watu hawa wana nia ya kukuua.” Neema alieleza.
“Kwa nini umeshawishika hivyo?” Niliuliza.
“Ondoka hapa sasa hivi, hawajui Jacob Matata yuko wapi, hivyo bila shaka wanataka kukutumia wewe kumpata.” Neema alisema huku akinipa ufunguo.
“Wa nini?” Niliuliza kwa mshangao.
“Utakwenda kujificha nyumbani kwangu, nitakupa maelezo zaidi nikija hiyo jioni. Tafadhali usitoke ndani.” Neema alisema kwa sauti ya kubembeleza.
“Niambie sasa hivi!” Nilisema.
“Hatuna muda. Chukua na hii karatasi!” Alisema halafu akaanza kunivuta.
“Ngoja nichukue vitu vyangu muhimu!” Nilisema huku nikitembea kuelekea chumbani kwangu. Neema akabaki amesimama akiniangalia. Niliingia chumbani, nikachukua kamera yangu, laptop, simu na vitambulisho vyangu. Nikatoka.
“Usifunge mlango.” Neema alisema. Kumbe alikuwa amesimama nje ya mlango wa chumba changu.
“Kwa nini?
“Mbona una maswali mengi hivyo? Twende!”
Sikutaka kubisha, nikajikuta namwamini huyu msichana na kumfuata.
“Hatutatumia mlango wa kawaida, kuna mlango wa nyuma ambao hautumiki. Ukipita hapo utatokea mtaa wa nyuma ambapo utakuta waendesha bodaboda. Ukifika hapo mwambie akupeleke, Ogonapo nyumba namba 0870. Nitakukuta hapo asubuhi.’ Neema alisema. Ile kusikia jina Ogonapo nyumba namba 0870 moyo wangu ukashituka.
Neema huyuhuyu ndiye aliyeniambia kuwa Kigi Mbonea anaishi Ogonapo nyumba namba 0870. Amesahau ama?
Anataka niende nyumbani kwa Kigi?
Nilijiuliza maswali mengi wakati tukitembea kuelekea mlango wa nyuma wa hoteli.
Tulifika kwenye mlango ambao ilionekana wazi kuwa haukuwa ukitumika. Neema akaingiza ufunguo, baada ya kuhangaika kidogo mlangoa ulifunguka.
“Mlango ushakuwa na kutu huu, una muda mrefu haujatumika!” Neema alisema. Sikusema kitu, nilikuwa na moyo mzito juu ya binti huyo.
“Pita kwenye ule mti wa mpera pale, halafu utakata kushoto.” Neema alisema. Nikapita kwenye mlango na kutoka nje. Nikageuka kumwangalia, nilitaka kumuuliza lakini nikajikuta nasita.
“Nafanya hivi kwa ajili ya Jacob Matata.” Neema alisema kisha akafunga mlango.
Nikabaki nimesimama nauangalia mlango.
Nifanye kama alivyonielekeza ama niende stendi ya mabasi? Nilijiuliza nafsini. Mara ile sauti ya Chogo ikanijia kichwani mwangu.
‘Utaondoka hapa, huyo malaya wako anajifanya mjanja sana. Ila unatakiwa ujue mambo mawili. Umeua. Umeua watu wawili. Ushahidi tunao, jalada lako liko polisi. Ukijifanya kuondoka Kigoma na kusemasema ovyo basi ujue utafia jela.’
Malaya yupi ambaye Chogo alimwongelea?
Au kuondoka kwa Jacob Matata kama Neema alivyosema?
Okay, inawezekana wameniachia ili niwe chambo cha kumpata Jacob Matata. Ina maana hawajui kuwa ameondoka au? Siwezi kuondoka, nadhani Chogo anajua hilo, nikiondoka nitakuwa nimeitoroka polisi. Nitakuwa nimejiweka matatizoni zaidi. Au niende kituoni mwenyewe? Hapana, yule Askari polisi mwenye nyota tatu si mtu mwema kwangu.
Nikaanza kutembea kama Neema alivyonielekeza. Nilifika upande wa nyuma wa mtaa. Hatua kama ishirini toka nilipotokezea niliona pikipiki, japo ilikuwa usiku lakini mng’ao wa yale makoti yao ulinionyesha kuwa walikuwa wao. Nilitembea kuelekea walipokuwa. Nilipokaribia pikipiki kama tatu hivi ziliwashwa. Wawiwili wakanifuata.
“Twende brother!” Walisema kwa pamoja.
Niliashiria kumfuata mmoja wao. Mwingine akageuza kurejea kwa wenzie.
“Sema kaka?” Alisema yule mwendesha pikipiki.
“Nipeleke Ogonapo.” Nilisema.
Pikipiki ikaondolewa.
Tulipofika Ogonapo yule dereva akauliza.
“Sehemu gani brother?”
Nyumba namba 0870.” Nilimjibu.

Niliwasili nyumba namba 0870. Niliangalia saa yangu tayari ilikuwa saa nane na robo usiku. Nilitembea taratibu kuufuata mlango wa nyumba. Ni nyumba ambayo haikuwa na uzio, japo ilikuwa na miti mingi mbele yake. Hiyo ilinifanya nipate taabu kidogo kuona namba ya nyumba iliyokuwa imeandikwa pembeni ya mlango wa mbele. Wakati naelekea mlangoni mara zile hisia za kilichonikuta siku moja iliyopita kwenye nyumba namba 511, zilikuwa zikiitesa nafsi yangu.
Nilipoufikia mlango wa nyumba niliingiza ufunguo niliopewa na Neema ili nifungue. Nikafungua.
Nikaingia na kuufunga mlango kwa nje.
Tofauti na mwonekano wa nje, nyumba ile ilikuwa imepangwa vizuri sana ndani. Vitu vya thamani viliifanya ipendeze sana. Nilianza kukagua sebuleni halafu nikaingia chumba kimoja baada ya kingine. Nilipoingia chumba ambacho bila shaka ndiyo cha mwenye nyumba nilitulia kwa muda. Nikaangaza macho huku na kule.
Mara moyo wangu ukapoteza mapigo kwa sekunde.
Nilifikicha macho. Ni yenyewe sijakosea!
Ina maana alikuwa hapa? Nilijiuliza.
Niliiangalia tena ile kofia. Ndiyo ni ileile ya Jacob Matata.
Niliisogelea nikaichukua.
Ni yenyewe. Ina maana Jacob Matata alikuwa hapa. Au ndiyo maana Neema anasema walikuwa na Jacob Matata usiku uliopita?
Ina maana alishajivutia huyu binti?
Nikajikuta natabasamu peke yangu. Huyo ndiyo Jacob Matata ninayemjua. Asione binti mzuri lazima tu ajitwalie.
Wakati nawaza hayo mara nikawa nimekanyaga kitu kama karatasi. Nikatoa mguu kuangalia. Karatasi ilisomeka, ‘Dume Kinga Madhubuti.’ Kazi ya Jacob Matata hii.
Huwezi amini, hiyo ikanifanya niwe na amani na kuendelea kukaa mule ndani.
Sasa nikaelewa kwa nini kauli ya mwisho ya Neema wakati ananiaga alisema, ‘Nafanya hivi kwa ajili ya Jacob Matata!’
Duuh, yule rafiki yangu hatari sana! Kawezaje ndani ya muda mfupi vile?
Niliingia jikoni nikapika.
Baada ya kula nikaamua niingie kitandani kulala.
Usingizi wangu ulikatishwa majira ya saa tatu na robo asubuhi wakati niliposikia kitu kama mashine ya faksi ikilia. Mwanzo nilidhani nakosea kusikia lakini nilipojiridhisha ndipo nikaanza kutafuta ilikuwa ikilia wapi. Hatimaye nikapata chumba ambapo mashine hiyo ya faksi ilikuwa ikilia.
Nilijaribu kufungua mlango, ukafunguka.
Nikaingia ndani ya chumba na kuanza kuangaza.
Mashine ilikuwa imeacha kulia, hii ilimaanisha ilikuwa imemaliza kupokea ujumbe. Haikuchukua muda nikaiona mashine ya faksi. Kulikuwa na karatasi ambayo ilikuwa imechapa ujumbe uliokuwa umetumwa. Nilisogea na kuichukua ile karatasi. Nikaanza kuisoma. Macho yakanitoka kwa mshangao. Nikameza mate mengi ya baridi yaliokuwa yamejaa kinywani kwa sababu ya mshangao ambao ulitokana na ujumbe uliokuwa kwenye ile karatasi.
Ujumbe ulikuwa umetumwa kwa Kigi.
Ulikuwa umeandikwa kwa namna ya ajabu sana, inaonyesha mwandishi wake alikuwa anasimulia alichokuwa amekiona asubuhi hiyo. Jacob Matata alishangaa kubaini kuwa anuani ya mtumaji ilionyesha kuwa ujumbe huo ulitumwa toka kwenye majengo ya Ofisi Fukuzi. Ujumbe ulisomeka;

Kigi,

Kama unavyotaka siku zote, nitasimulia kama nilivyoona kwa macho yangu. Bila shaka ni jukumu lako kujua nini cha kufanya na simulizi hii ambayo inakutaarifu nilichokiona.

Simulizi ya siri:

Mlango wa ofisi ile uligongwa kwa mara ya tatu. Mwanamke wa makamo alifunika jalada alilokuwa akisoma, huku akiwa na uso uliokereka. Alivuta kiti chake nyuma kisha akasema ‘pita ndani tafadhali’. Kijana mmoja mrefu mwembamba aliyekuwa nyuma ya mlango huo kwa dakika tatu sasa aliitengeneza tai yake kabla ya kufungua mlango wa chumba hicho. Mlango ulikuwa umeandikwa ‘Mkurugenzi Ofisi Fukuzi’. Alipoingia, akiwa na karatasi ndogo mkononi alikwenda moja kwa moja hadi kwenye meza ya Mkurugenzi. Yule Mwanamke alimwangalia tu bila kusema neno, ilikuwa wazi hakupenda ujio wa mtu yeyote ofisini kwake kwa muda huo. Ndiyo maana ilimchukua muda mrefu kuitikia hodi. Jalada lililokuwa limeteka fikira zake bado lilikuwa juu ya meza wakati alipokabidhiwa karatasi na yule Kijana Mrefu aliyekuwa ameingia ofisini kwake.
‘Nimeona si vema wewe kuchelewa kupata habari hii’ Alisema yule kijana baada ya kukabidhi karatasi.
‘Asante!’ Alisema yule Mama huku akiwa anaiangalia ile karatasi. Kijana huyu alikuwa anatoka kwenye chumba cha kukusanya taarifa. Taarifa ambazo baadaye hutumiwa na hiki kitengo cha kijasusi kiitwacho Ofisi Fukuzi. Hivyo Mwanamke huyu aitwaye Bi. Anita akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa kitengo hicho cha siri sana, alikuwa na vijana wa kada mbalimbali ambao alikuwa akishirikiana nao katika kuhakikisha wanafanya kwa ufasha kile ambacho walitakiwa kufanya na mtu aliyetengeneza kitengo hicho. Hivyo kazi ya Kijana huyu, pamoja na mambo mengine ilikuwa ni kukusanya taarifa toka kwente vituo maarufu vya redio na televisheni, magazeti maalum waliyochagua wao toka sehemu mbalimbali duniani. Kusoma tovuti za kijasusi na zile nyingine maarufu. Kutembelea akaunti za Twitter, Facebook, Instagram za watu maarufu. Lengo ikiwa ni kuona kama kulikuwa na habari zozote ambazo wangezihitaji katika shughuli zao. Hivyo kijana huyu alikuwa akiongoza timu ya watu watano katika kufanya kazi hiyo ya kukusanya habari. Kijana huyu anaitwa Phil, pamaoja na kuwa na uwezo wa juu wa mambo ya teknolojia ya mawasiliano na habari lakini pia, anajua kuongea lugha tano kubwa duniani.
Karatasi aliyokuwa amepewa ilikuwa imeandikwa;
Mwandishi wa habari mmoja wa kike anashikiliwa na kundi hatari la waasi huko nchini Uganda. Kundi hilo lijulikanalo kama Lord Resistance Army (LRA) linamshikilia mwanadada huyo Mwandishi wa Habari kwa kile kinachosemwa kuwa ni kufikia na kuiba taarifa za siri za kundi hilo. Mwandishi huyo kutoka DRC Congo, alikamatwa hapo jana wakati akiwa kwenye shughuli zake. Kundi hilo limekataa kumwachia kwa kudai Mwanadada huyo anakusudia kuzituma vyaraka hizo za siri kwa mashirika ya habari ya kimataifa. Hivyo LRA imedai itamwachilia Mwandishi huyo mara tu atakapokabidhi nyaraka hizo za siri.

Alipomaliza kusoma akashusha pumzi.
‘Chanzo cha habari?’ Akauliza huku macho yake yakimetameta.
‘This Time Tommorow Radio!’ Phil alijibu kwa mkato.
‘Hatari sana. Nashukuru kwa taarifa. Hebu niandalie taarifa muhimu kuhusu LRA, Joseph Kony na milango inayoweza kutufikisha huko. Nitahitaji taarifa hizo ndani ya muda mfupi ujao!’ Bi. Anita, mkurugenzi wa ofisi fukuzi alisema kauli iliyomfanya Phil ainame kwa heshima kisha akatoka nje ya ofisi ile.

Aliyoletwa ilikuwa ni sehemu ya taarifa ya habari kwenye moja ya redio za kimagharibi zinazofanya matangazo yake kwa lugha ya Kiswahili. Haikuwa habari ya maana wala mvuto kwa asilimia kubwa ya wasikilizaji. Lakini hali ilikuwa tofauti kwa huyu, Bi. Anita, mkurugenzi wa Shirika la Kijasusi na Ofisi Fukuzi, alipoisoma tu alihisi tumbo lake likimkata kwa namna ambayo alishindwa kubaini kuwa ilikuwa hofu au hasira. Hakutaka kungoja zaidi. Alinyanyua simu yake ya mezani kisha akaminya namba kadhaa.
‘Jacob Matata, nakuhitaji ofisini kwangu mara moja!” Alisema kisha akakata simu.

* * *

‘ Hakuwa na ruhusa ya kwenda Uganda imenishangaza kuwa amekwenda. Lakini kusikia yuko mikononi mwa Joseph Kony imenifanya nishituke zaidi. Kama Jasusi amekuwa akifanya kazi zake Congo DRC kwa miaka kadhaa sasa kwa mafanikio makubwa. Sasa nasikia alienda Uganda kwa kivuli cha Mwandishi wa Habari. Lazima kuna kitu cha muhimu na kizito sana alikuwa anafuatilia. Safari yake inaonekana ilikuwa ya dharura sana na kutakuwa na jambo zito amefanikiwa kupata ndiyo maana sasa amekamatwa na waasi wa Lord Resistance Army (LRA) ambao wanadai yeye kama Mwandishi wa Habari, amefanikiwa kuchukua nyaraka za siri ambazo wanazitaka.
Najua hawawezi kumuua hadi awapatie hizo nyaraka za siri. Joseph Kony ambaye ndiye kiongozi wa kundi hilo ameshasema watamshikilia hadi awapatie au kuwaambia zilipo hizo nyaraka.
Jacob, nenda Uganda kamfuate, namtaka Juliana Owima akiwa hai. Lakini nazitaka hizo nyaraka wanazodai kuwa kama zikipatikana zitahatarisha usalama wote wa Nchi za Maziwa Makuu. Nazitaka hizo nyaraka kwa gharama yeyote. Nenda Uganda kabla hatujachelewa, unaweza kujua ni mateso ya aina gani huyo Msichana anapitia sasa hivi. Tusijechelewa mambo yakaharibika, tukampoteza Juliana na hizo nyaraka za siri.’ Alisema Bi. Anita. Mpelelezi Jacob Matata baada tu ya kusikia maelezo na amri hiyo alishusha pumzi ndefu kama ishara kuwa kazi imeiva.
‘Bila shaka unamwongelea Juliana Owima, yule ambaye nilifanya naye kazi Goma mwaka ule katika mazingira tata sana?’ Jacob Matata alihoji.
“Ndiye yeye!” Bi. Anita alijibu kwa mkato huku macho yake yaking’aa.
‘Namkumbuka. Kama unavyosema lazima kuna kitu kilimsukuma kwenda huko. Yule mwanamke hatari sana!’ Jacob Matata alisema. Bi. Anita aliinua simu na kuongea baada ya kubonyeza namba kadhaa.
‘Phil unaweza niletea zile taarifa nilizokuoamba uandae?’ Bi. Anita alisema halafu akaweka chini mkonga wa simu.

Dakika chache baadaye Phil aliwasili akiwa na majalada kadhaa. Aliyaweka mezani baada ya kuwa ameshasalimiana na Jacob Matata.
‘Naweza kusema kuwa kundi linalomshikilia Juliana ni moja kati ya makundi hatari sana hapa Afrika. Hii inatokana na mundo wake na jinsi linavyokusanaya taarifa na kuzitumia. Sasa mimi na timu yangu tumekuwa tukifanya upembuzi wa taarifa tulizonazo kuona namna ambavyo Juliana anaweza kufikiwa. Kwa namna yoyote ile siyo rahisi sana ila tuna taarifa zifuatazo ambazo zinaweza kuwa za msaada kwa namna fulani.’ Phil, mtaalam wa mambo ya wamasiliano na habari wa Ofisi Fukuzi alisema kwa sauti ya kujiamini huku akiweka sawa majalada yake.
‘Kundi hili kama mjuavyo linaongozwa na Joseph Rao Kony, mtu mwenye umri wa kati, yaani miaka 56. Mtu aliyejipatia alama ya rangi nyekundu na Polisi wa Kimataifa (Interpol) kwa kuwa mtu hatari sana. Amekuwa mbabe wa kivita kwa miaka 27 sasa. Ni mtu anayetumia mbinu za kisasa na kijadi katika mapigano. Kama mnavyojua kundi lake lilianzia maeneo ya Magharibi ya Uganda kwa kile alichosema kuwasaidia watu waliokandamizwa na Serikali ya Uganda. Gulu ikiwa ndiyo Makao Makuu yake ya awali, hasa kwa vile alizaliwa hapo na alikubaliwa na watu wa makabila yaliyoko upande huo wa Uganda. Baada ya kupambana na Serikali ya Uganda kwa miaka mingi huku akiwa anatafutwa na ICC kwa kutumia watoto kama askari na kuua raia wengi, Kony amekuwa kama mzimu. Kuonekana kwake, kuishi kwake na matendo yake vimekuwa kama ndoto kwa adui zake, raia wa maeneo anayofanya kazi na hata askari wake mwenyewe.
Inaaminika kuwa Kony ana kambi aliyoifanya gereza ambalo huwashikilia mateka wake muhimu. Gereza hilo halijulikani liko wapi, kwani watu hupelekwa wakiwa hawajitambui. Kuna watu wawili tu ambao walishafika kwenye gereza hilo na kutoka wakiwa hai. Wao pia, hawakumbuki chochote kuhusiana na mahali gereza lilipo. Habari tulizopata asubuhi hii ni kuwa Kony anawaamini watu wanne tu na ndiyo huongea nao mara kwa mara. Watu hao ni Jenerali Zoazina Lakwena, mwanamke mkatili na malaya ambaye wenyewe humwita Ghost Lady. Elizabeth Achan, mke wake wa pili ambaye inaaminika ndiye aliyeuteka moyo wa Joseph Kony ambaye ana wake zaidi ya 60. Wengi wa wanawake hao ni wale ambao walikamatwa na jeshi lake wakiwa bado wasichana wadogo. Mwingine ni Lakoch Oyoo, maarufu kama Chogo ambaye inasemekana walikuwa marafiki sana na Joseph Kony tangu Shule ya Msingi, ambapo walikuwa wacheza dansi wazuri sana. Wa mwisho ambaye inasemekana ni mtu anayeaminiwa na kuwa na ukaribu na Joseph Kony ni Padri Mike Mukiibi wa Parokia ya Odek mji aliozaliwa Joseph Kony. Inasemekana watu hawa wote wanapatikana Gulu, Kaskazini mwa Uganda isipokuwa mke wa Kony na Jenerali Alice Lakwema ambaye wanasema huishi kama mzimu kama Kony mwenyewe. Wapo wanaosema Joseph Kony na Alice ni mtu na binamu yake.

Nadhani taarifa hizi ni muhimu kuzijua, hasa kwa vile kundi linalomshikilia Juliana linaongozwa na Kony. Pia, uwezekano ni mkubwa kuwa Juliana anaweza kuwa kwenye gereza hilo la siri ambalo liko msituni. Ambalo hakuna ajuaye lilipo...’ Phil alikatizwa maelezo yake na Jacob Matata.
“Je, una majina ya hao watu wawili ambao inasemekana ndiyo pekee walioweza kufanikiwa kutoka kwenye hilo gereza la siri la Joseph Kony?’ Jacob Matata alihoji.
‘Ndiyo, mmoja ni Vincent Otti, ambaye alikuwa kiongozi mwenza na Joseph Kony. Kwa pamoja walikuwa wakiliongoza kundi la LRA hadi pale ambapo Kony alikataa kusaini mkataba wa amani na Sudan Kusini. Kwa vile mazungumzo ya amani kati ya LRA na Serikali ya Sudan Kusini yalisimamiwa na Vincent Otti kwa upande wa LRA, hivyo kitendo cha Kony kukataa kusaini mkataba wa amani dakika za mwisho kulimkera sana Vincent na huo ukawa mwanzo wa yeye kuwekwa kwenye gereza hilo. Aliachiwa huru September 2007 kabla ya kusemekana kuwa ameuawa October 8, 2007.’ Phil alisema kabla ya kukatishwa tena na Jacob Matata
‘Yaani Kony alimwachia Vincent?’ Jacob Matata alihoji.
‘Ndiyo, September 2007.’ Phil alijibu huku akiangalia jalada lake.
‘Walimwachiaje? Au niseme wanafanyaje kumwachia mtu?’ Jacob Matata alizidi kuhoji.
‘Vincent ambaye aliishi siku chache sana kabla ya kuuawa tena na vikosi vya Kony, anasema unafungwa na unakuwa huoni uko wapi na unakwenda wapi hadi alipotupwa sehemu. Asubuhi akasikia sauti za watu wakimshangaa akiwa amefungwa. Walipomfungua ndipo alipojikuta kwenye kijiji kimoja huko Gulu, kaskazini mwa Uganda.’ Phil alisema huku akimwangalia Jacob Matata.
‘Okay! Sasa kwa nini unasema inadhaniwa kuwa aliuawa? Hakuna uhakika?’ Jacob Matata alisema.
‘Kuna uvumi kuwa inawezekana hakufa maana hakuna aliyeona maiti yake. Wanajeshi watiifu kwa Kony wanasema aliuawa na walimzika wao wenyew.’Phil alisema.
‘Sasa kwa nini watu hawaamini kinachosemwa na LRA?’ Jacob Matata alihoji.
‘Kuna uvumi kuwa kulikuwa na mgawanyiko mkubwa miongoni mwa askari wa LRA kufuatiwa kufukuzwa na kisha amri ya kuuawa Vincent, hivyo wapo wanaodai kuwa inawezekana askari hawakumuua na Vincent yuko mafichoni tu.’ Phil alisema.
‘Okay!. Naona itakuwa kazi ngumu sana kumpata Juliana kama yuko kwenye mikono hatari namna hii’! Jacob Matata alisema huku akimwangalia Bi. Anita.
‘Ni kweli tunajua hilo, ila kama ujuavyo kuwa usalama wa Nchi za Maziwa Makuu unadhoofu sana kwa sababu nyingi, moja wapo ni usiri uliopo juu ya mtu au watu au Serikali inayodhamini makundi ya waasi kama hili la LRA, hivyo ni hisia za wakubwa kuwa inawezekana kupatikana kwa hizo karatasi ambazo inasemekana Juliana amezipata kunaweza saidia kujua ni wapi waasi wanapata nguvu na pesa ya kuendesha operesheni zao ndani ya nchi zetu hizi. Lakini pia, kundi kubwa sana la waasi kule Congo DRC wanamchukulia Juliana kama mmoja wa watu wao muhimu kwa vile tulimpandikiza kwa miaka mingi na sasa amekuwa sehemu yao bila wao kujua. Hivyo inawezekana wao ndiyo waliomtuma Uganda, sasa swali linakuwa ni kitu gani cha muhimu ambacho waasi wa Congo walikuwa wanakitafuta toka kwa Joseph Kony. Pia, hatutaki kumpoteza mtu muhimu kama yeye ndani ya DRC, maana ndiye anayetufanya tujue undani na ukweli kuhusu siasa za Congo DRC hasa upande wa waasi. Hivyo sitaki tumpoteze.’ Bi. Anita alisema halafu akaongeza.
‘Hutakuwa na wakati mgumu sana kiusalama, Uganda na waasi wa LRA wanajua kuwa sisi hatuna maslahi yoyote eneo hilo. Juliana ni Mnyarwanda wa asili na mtu anayefanya kazi Congo DRC kwa miaka sasa. Hivyo hakuna mtu atakayeshuku kuwa ni mtu wetu na anafanya kazi kwa niaba yetu, japo itakuwa rahisi kujua kuwa mama yake ni Mtanzania, lakini hajawahi kuwa na mwingiliano mkubwa na Tanzania isipokuwa wakati ule alipoolewa na Makame. Hivyo hakuna ambaye atashikitukia au kutilia shaka uwepo wako kama mtalii toka Tanzania.’ Bi. Anita alimaliza maelezo yake.
‘Labda la mwisho tu ni kuwa, Joseph Kony ni msomaji mzuri wa Biblia. Anapenda umaarufu. Mtu asiyefikiria mara mbili linapokuja suala la kumuua mtu.’ Phil alisema.
‘Sawa nimewaelewa. Asanteni kwa utangulizi mzuri. Ila naona kila dalili kuwa kazi hii itakuwa ngumu sana!’ Jacob Matata alisema huku akiwaangalia kwa tuo.
‘Alipofika Uganda alifikia hoteli moja inaitwa Margarita Palace, iko kwenye mji mdogo uitwao Lira, Kaskazini mwa Uganda. Inasemekana muda mwingi alikuwa akitumia pikipiki ya bwana mmoja aitwaye John Helem, wenyewe hupenda kumwita Drogba, kwa sababu anafanana sana na yule mcheza soka wa kiafrica Didier Drogba.

Mwisho wa taarifa.

Kazi njema Kigi.

Ujumbe ule wa faksi uliishia hapo.
Ukweli nilijikuta naingiwa na hisia mchanganyiko.
Nilikuwa kama nasoma riwaya vile. Lakini nilishangaa kuona majina kama Chogo na Zoazina yakitajwa kuwa ni watu wa karibu sana na Joseph Kony.
Ina maana wako hapa Kigoma kwa kazi maalumu tu na kazi hiyo ni kunishughulikia mimi na kumsaka Jacob Matata. Kwa nini?
Huyo Juliana Owima asije kuwa ndiye msichana aliyesafirishwa na teksi ya Kigi?
Duuuh, nifanyeje sasa!?
Kwa hiyo ina maana Jacob Matata atakuwa njiani kuelekea Uganda. Inawezekana hili ndilo lilomfanya arudi Dar haraka? Hapana inaonyesha taarifa hii ilimjia bosi wake Jacob Matata wakati Jacob Matata akiwa yuko ofisini tayari. Ndiyo maana alinyanyua simu tu akamwita.
Wazo la kumpigia Jacob Matata lilinijia tena.
Nilirejea kwenye chumba nilichokuwa nimelala. Nikachukua simu kwa lengo la kumpigia Jacob Matata.
Simu haikuwa hewani.
Jacob Matata atawasili lini Kampala. Hii taarifa ni ya leo. Ina maana kwa sasa yuko kwenye maandalizi. Je, ninaweza kuwahi mimi kufika na kumpokea kabla yeye hajafika?
Swali hilo likanifanya nianze kuangalia ratiba za mashirika mbalimbali ya ndege na uwezekano wa Jacob Matata kuingia Uganda.
Hatimaye nikajiridhisha kuwa hata afanyeje Jacob Matata angeingia Kampala saa tano na nusu usiku. Labda akodishe ndege yake mwenyewe. Akitumia gari ina maana atafika kesho usiku.
Je, naweza kumuwahi ili nimtaarifu kuhusu hawa watu?

Wakati nawaza hayo, mlango wa kutoka nje uligongwa kwa fujo. Sikutaka kuamini kuwa Neema ndiye angegonga mlango kwa namna ile. Nilihisi maisha yangu yako hatarini. Nilivaa harakaharaka na kuchukua vitu vyangu muhimu. Nikaanza kufikiria nifanyeje. Mara nikakumbuka kuwa dirisha la chooni lilikuwa la kioo ila likifunguka linaacha nafasi kubwa. Nilikimbilia chooni. Wakati huo nikasikia mlango unavunjwa kwa fujo. Niliparamia dirishani na kupenya, nikadondokea nje kama mzigo. Nilisikia maumivu lakini sikusimama. Nilikimbilia vichakani na kutimua mbio kwa kadiri ya uwezo wangu. Nilitokezea mtaa wa tatu nikiwa bado nakimbia taratibu na kuhema kama nguruwe pori aliyekoswakoswa na mshale.

Niliacha kukimbia, nikawa natembea huku natweta vibaya sana. Nikiwa natembea hivyo ghafla likatokea gari nyuma yangu gari hilo lilikuwa likienda kwa kasi sana. Nilihisi hatari, nikajisogeza pembeni ya barabara.
Ghafla lile gari likafunga breki kwenye miguu yangu.
“Ingia twende haraka!’’ Sauti ya kike iliongea. Niliangalia, alikuwa ni Viva Davis. Yule muuguzi wa ile sehemu niliyokuwa nimeshikwa mateka.
“Twende wapi!?” Nilisema kwa hofu na mshangao.
“Watafika muda wowote, watakuua kama walivyomuua Neema!” Viva alisema kwa sauti
“Wamemuua Neema!?” Nilishikwa na mshangao mwingine.
“Utauliza tukiwa kwenye gari, twende wewe acha ufala!” Viva alisema kwa hasira.
Niliingia ndani ya gari na gari likaondolewa kwa kasi sana.
“Waligundua kuwa yeye ndiye aliyekutorosha pale hotelini.”
“Duuuh, hivi polisi hakuna hapa?”
“Nikuulize wewe ulipoenda ilikuwaje?” Viva alihoji huku akiliungurumisha gari kwa kasi sana.
“Duuuh we acha tu!” Nilisema.
“Ndiyo hivyo!” Alijibu.
“Sasa tunakwenda wapi?”
“Nikuulize wewe. Mimi sasa nitaelekea Uganda kwa ajili ya kazi maalumu. Ila kabla sijaenda huko, nataka nihakikishe uko salama. Unataka nikupeleke wapi?” Alisema huku macho yakiwa barabarani.
“Twende wote Uganda.” Nilisema kwa sauti madhubuti.
“Kufanya nini?” Aliuliza kwa mshangao.
“Kumsaidia Jacob Matata!” Nilijibu.
“Hutaki kuonana na yule mwendawazimu?” Aliuliza.
“Umejuaje nilikuja hapa kuonana na mwendawazimu?”
“Neema alinisimulia.”
“Neema alijuaje?”
“Aliambiwa na Kigi.”
“Hivi Kigi ni nani hasa?” Nilimuuliza.
“Ndicho kinanipeleka Uganda, nitajua nikiwa huko.”
“Wewe ni nani na unahusika vipi kwenye hili?” Niliuliza tena.
“Nikupeleke wapi Japhet, hatuna muda wa kupoteza?” Aliuliza badala ya kujibu.
“Nilidhani wewe ni muuguzi, sasa…!”
“Sikiliza, kuna gari maalumu limeletwa kwa ajili ya kukupeleka Arusha, ila hutajulikana uko wapi hadi nitakapomaliza kinachonipeleka Uganda. Hivyo nakupeleka kwenye gari, wakati wewe ukielekea Arusha mimi nitaelekea Uganda.” Alisema kwa sauti yenye amri. Siyo tena ile sauti ya kiuguzi.
“Hapana! Nitaweza kumsaidia Jacob Matata, namjua Chogo, namjua Kigi, namjua Zoazina, naweza msaidia.” Niliposema hivi, Viva alipunguza mwendo.
“Hivi umejuaje kuwa Jacob Matata anakwenda Uganda na kama kwenda kwake kunahusiana na hao unaowataja?” Aliuliza huku gari likiwa limepunguzwa mwendo.
Badala ya kujibu nilitoa ile karatasi niliyokuwa nimeichukua kwenye mashine ya faksi.
Nilimkabidhi.
Gari likapunguzwa mwendo zaidi wakati akisoma ile karatasi.
Alipomaliza kusoma alishusha pumzi kwa nguvu.
“Umeipata wapi?”
“Kwenye moja ya vyumba vya nyumba ya Neema.”
“Ambayo ni nyumba ya Kigi pia, ina maana Kigi ameshasoma hii?” Alidakia.
“Hapana hajasoma, imeingia asubuhi hii.”
“Oooh! Naona muda hapa. Kwa hivyo ni wewe tu na mimi sasa ndiyo tumeona ujumbe huu?” Aliuliza.
“Bila shaka, japo sina hakika kama wewe ni mtu salama au la!” Nilisema huku nikijilaumu moyoni.
“Sikiliza Japhet, sasa nakuamini. Uningekuwa mtu mbaya ungekuwa umeshaharibu mambo mengi sana kwa kuona karatasi hii. Halafu kwa vile umeng’ang’ania kwenda Uganda itabidi tusiende wote kwa wale watu wanaosubiri nikupeleke. Utabaki hapa. Ili mimi nikawaambie wale kuwa sikukuona, halafu nikipewa gari la safari ndipo nitakuja kukuchukua tuelekee Uganda” Viva alisema

Saa sita na robo mchana safari yetu ya kwenda Uganda ilianza. Tulikuwa tunatumia gari moja la Shirika la Kimataifa. Lilikuwa gari kubwa na zuri kwa safari za masafa marefu.
Tulikuwa wawili tu ndani ya gari.
“Viva, unaweza kuniambia wewe ni nani hasa?” Hatimaye nilivunja ukimya.
“Ni mapema mno wewe kujua ila tu ujue niko kazini.” Alijibu.
“Kwa hivyo ile ilikuwa kazi ya danganya toto?” Niliuliza.
“Hapana ile pia ilikuwa sehemu ya kazi yangu, ujio wako na ujumbe wako ukasababisha ikamilike.” Alisema.
“Ikamilike, kivipi?”
“Ile flash disk uliyonipa iliniwezesha kupata nilichohitaji.” Alisema.
“Unajua flash hiyo ni ya nani?” Nilimuuliza.
“Bila shaka uko na pasi ya kusafiria?” Aliuliza badala ya kujibu.
“Ndiyo, ninayo!” Nilijibu.
“Tukifika Kampala wewe utaendelea na kazi yako na mimi nitaendelea na maisha yangu.” Alisema.
Bado nilikuwa na maswali mengi kichwani mwangu. Nilihisi huyu msichana anaweza kuwa na baadhi ya majibu, hivyo nikaazimia kufanya naye mazungumzo kwenye safari hii kwa kadiri inavyowezekana.
“Unasema flash disk niliyokupa ilikufanya ukamilishe ile kazi. Kivipi?” Niliuliza.
“Uliwahi kuangalia ndani ya ile flash kulikuwa na nini?” Aliuliza badala ya kujibu.
“Hapana! Niliongopa
“Basi yaliyokuwa kwenye ile flash ndiyo yalifanya niamue kuchukua hatua moja mbele.” Alisema.
“Yepi hayo? Je, unajua ni kwa nini watu hawa wananiandama?” Niliamua niulize kuanzia upande mwingine.
“Bila shaka ni kwa sababu ya kitabu ulichoandika. Sivyo?” Alisema na kuuliza.
“Sijui. Kwani kuna muunganiko wowote wa hiyo flash unayosema na kwa nini wananitafuta?” Niliuliza tena nikijua nitampata.
“Japhet, unasema hukuangalia ile flash, lakini kwa nini uliniomba nimpelekee Neema?” Aliuliza badala ya kujibu.
“Kwa sababu ya sehemu nilipoitoa, nilitaka aangalie ndani kulikuwa na nini?”
“Uliitoa wapi?”
“Niliiokota kwenye nyumba namba 511 maeneo ya Nyangofa”
“511?!” Alirudia kutaja namba kwa mshangao.
“Unaijua?” Niliuliza.
“Nyabange Mbanga Mbia Mbanga!” Alisema kama anayewaza.
“Ndiyo nani?” Niliuliza kwa hamu.
“Kwani kuna mtu anaishi kwenye hiyo nyumba, maana mmiliki wake alishakufa miaka mingi iliyopita.” Viva alisema kwa mshangao.
“Nilipoingia sikukuta kiumbe hai zaidi ya maiti moja ya mwanamke.” Nilisema.
“Nini kilikupeleka kule?” Aliuliza kwa mshangao.
“Chogo alitaka nikutane naye kule.” Nilijibu.
“Chogo alipajuaje kule? Mlionana?” Aliuliza mfululizo.
“Hapana, nilikutwa na polisi na kushutumiwa kwa mauaji.”
“Aiseee! Sasa hiyo flash uliipataje?”
“Niliiokota chini ya kochi ambalo juu yake kulikuwa na mtu amefariki.”
“Unadhani ilikuwa ya nani?”
“Ilikuwa ya mwendawazimu Kumbamasaka Jitu la Watu, maana nilimwona nayo siku nimemwona pale sokoni Mwanga.” Nilisema.
“Shiiit! Usiniambie hii kitu ilikuwa na yule mwendawazimu. Sasa naamini yule amejisingizia ukichaa. Mwanzoni nilihisi lakini nilipomfuatilia kwa karibu nilijiridhisha kuwa alikuwa kichaa lakini sasa inanipa hamu ya kuongea naye.” Alisema halafu akapunguza mwendo wa gari. Nikabaki namwangalia.
“Turudi, haiwezekani niondoke Kigoma sijaongea na huyo mwendawazimu!
“Are you serious!?” Nilitoa sauti ya kushangaa.
“Yes! Lazima niongee naye!” Alisema huku sasa akiwa anageuza gari. Hatukuwa tumefika mbali sana. Hivyo isingechukua muda mrefu kurudi Kigoma mjini.
“Sasa unajua utampata wapi?” Niliuliza.
“Mwanga Sokoni, alihamia hapo baada ya nyumba yake kuondolewa na Manispaa.” Alisema huku sasa akilivurumisha gari kurejea mjini. Sikutaka kusema mengi kwani hata mimi nilikuwa na hamu ya kuongea na huyo mwendawazimu. Ndicho kilichonileta Kigoma, hivyo kama ningefanikiwa kuongea naye ningekuwa nimefanikisha sana kile kilichonileta.
Kwa kupitia njia za panya tuliwasili Soko la Mwanga majira ya saa saba na robo. Tuliegesha gari mahali na kuanza kuangaza macho huku na huko Sokoni pale. Gari letu lilikuwa na vioo vyeusi, hivyo mtu wa nje asingeweza kuona ndani.
“Yule pale, wewe baki hapa. Nitaenda kumshika kwa nguvu na kumleta garini.” Viva alisema. Nilitazama alipoonyesha, nilimwona Kumbamasaka, akiwa vilevile kama nilivyomuona mara mbili zilizopita.
Begi likiwa linaning’inia na mkono wa kushoto akiwa ameshika kile kitabu SAA 72.
Kauli ya Viva ilinishangaza sana. Yeye, Msichana kama alivyo, amshike yule mwendawazimu kwa nguvu. Sikutaka kuamini ila nilinyamaza kimya.
Yule mwendawazimu alikuwa kipande cha mtu. Sikubisha, nilibaki ndani ya gari, wakati yeye akishuka na kuanza kutembea kuelekea alipokuwa yule mwendawazimu Kumbamasaka Jitu la Watu. Nilichukua kamera yangu na kuanza kupiga picha.
Viva alimfikia yule mwendawazimu. Mwendawazimu na Viva walipoangaliana uso kwa uso, sikuamini pale nilipoona imeibuka vita kubwa ya mapigano baina yao. Ukweli ilikuwa kama naangalia sinema. Viva alijuaje kupigana namna ile, halafu yule ni kichaa gani anayejua kupigana kwa staili zile.
Kumbamasaka alipiga kareti na judo za kufa mtu, ukweli mapigo yale hayakuwa ya Mwendawazimu.
Hisia kuwa Kumbamasaka amewahi kuwa mwanajeshi tena mwanajeshi safi zilianza kunitawala.
Viva alikabiliana naye vema kwa kama dakika tano hivi.
Jinsi Viva alivyokabiliana na yule kichaa ilinifanya nifute mawazo kuwa alikuwa muuguzi tu. Hata askari Polisi wa kawaida hawezi kupigana namna ile.
Umati wa watu ukawa umejaa huku wakishangilia.
Hali ilibadilika wakati Viva aliporusha teke kali sana ambalo lilimpeleka Kumbamasaka chini. Teke lile lilikuwa limetua kwenye shingo ya Kumbamasaka. Wakati huo Viva akawa anamfuata pale chini. Kumbamasaka alinyanyuka na wakati huohuo kikaonekana kisu kikienda kwa kasi kwenda kwenye kifua cha Viva. Kisu kile kilichorushwa na Kumbamasaka kwa kasi, kilitua kwenye titi la kushoto la Viva na kuzama. Viva alitoa mlio wa maumivu kisha akaanguka chini. Kuona hivyo watu wakaanza kutoa vilio vya hofu. Nikamwona Kumbamasaka akiokota begi lake na kitabu kilichokuwa kimeanguka chini na kuondoka taratibu kwa kujichanganya kwenye kundi la watu.
Nami nikachukua mwanya huo kukurupuka kwenda alipokuwa ameangukia Viva. Nilifika na kuinama, nilimgusa shingoni. Shingo ilikuwa ya baridi sana. Mwili wake ulikuwa umezungukwa na damu zilizokuwa zikichuruzika.
“Ameshakufa!” Nilijisemea.
Ghafla nikasikia ving’ora vya polisi kwa mbali. Niliinuka haraka na kukimbilia kwenye gari. Niliingia upande wa dereva na kuliwasha gari.
Nikaondoka, akili yangu sasa ikaniambia achana na Kumbamasaka nenda Uganda.
Nikiwa njiani nikapishana na magari matatu ya polisi. Nikajua yalikuwa yanakwenda eneo la tukio.
Moyo ulikuwa ukipiga kwa kasi.
Mikono iliyoshikilia usukani ilikuwa ikitetemeka.
“Amekufa!” Nilijisemea tena.
“Kumbamasaka ni mshenzi tu!” Nilijisemea tena kwa hasira.

Nilifika Bukoba saa kumi na moja na robo alasiri. Ina maana nilitumia saa nne toka Kigoma hadi Bukoba, ambayo ni kama kilomita 554 hivi. Nakwambia hili gari linakimbia sana halafu zile namba za Shirika la Kimataifa zilifanya nisisumbuliwe na polisi wa barabarani. Nilitafuta sehemu ya kula, baada ya kula ndipo nikakumbuka kitu ambacho nilipokuwa njiani nilisema nitafanya nikifika Bukoba. Nilitaka kufanyia kazi maelezo ya Kigi wakati alipoongea na Chogo kwa njia ya simu ya upepo.
“Ndiyo naweza kusoma maandishi ya hicho kibanda, kimeandikwa, CHINGA BOY MAPHONE, kiko jirani na Ofisi za Posta hapa Bukoba mjini. ‘Amemaliza anarudi, wacha niendelee na kazi. over!’ Maelezo haya yalinirejerea kichwani.
Nilitafuta zilipo ofisi za Posta, nilipozipata sikupata shida kukiona kibanda cha simu kilichokuwa kimeandikwa, CHINGA BOY MAPHONE. Sikutaka kufanya chochote hapo.
“Nahitaji kupiga simu.” Nilimwambia kijana aliyekuwa amesimama ndani ya kibanda.
“Poa kaka, simu hiyo hapo.” Alisema.
Nikachukua simu na kuweka namba zangu.
Nikapiga.
“Naona haipatikani!” Nikaongopa.
“Haina noma aisee!” Alijibu huku akindelea kucheza game.
Nikaondoka.
Nilipofika ndani ya gari, kabla sijaanza safari niliichukua ile namba ya simu nikaiweka kwenye shajara yangu. Nikawasha gari na kuliondoa. Sasa nikawa naelekea Mutukula ambapo nilijua ingenichukua kama dakika kadhaa tu kufika, maana ni umbali wa kama kilometa 81 hivi. Eneo ambalo linafanya mpaka wa Tanzania na Uganda.
Nilipofika Mutukula niliazimia kuacha lile gari nililokuwa nimetumia toka Kigoma. Hivyo nilikusanya kila kilicho changu. Wakati namalizia kufanya hivyo, mara nikasikia mlango wa nyuma wa gari ukifunguliwa. Haraka nikaangalia kulikoni. Mara nikashikwa na mshangao mwingine.
Macho yakanitoka, nikabaki nimesimama nisijue nifanye nini. Ndiyo, macho yangu hayakuwa yananidanganya.
Sikuwa nimekosea wala ndotoni, niliyekuwa namtazama ni yule mwendawazimu. Kumbamasaka Jitu la Watu. Aliufunga mlango wa nyuma wa gari. Hakujali mshangao wangu.
Hakunitazama wala kuhangaika na mimi. Alitembea taratibu kuondoka kwenye lile gari. Haiwezekani kuwa nilikuwa naye kwenye gari tokea Kigoma. Lakini pia haiwezekani yeye kufika hapo muda huo kama asingekuwa na mimi kwenye gari! Nikashangaa.
Au labda wakati nimeenda kumwangalia Viva pale chini alipokuwa akipigania pumzi zake za mwisho, Kumbamasaka aliingia kwenye gari?
Inawezekana, maana nilikuwa nimeacha mlango wazi.
Lakini huu ni ujinga, ushahidi ninao halafu najiuliza maswali ya kipumbavu.
Mtu anatoka ndani ya gari halafu natilia shaka kuwa hakuwa kwenye gari? Huyu mwendawazimu wa ajabu sana.
Sasa yeye anakwenda wapi? Alikuwa vilevile, begi lake begani, kitabu cha SAA 72 kimeshikiliwa mkono wa kushoto. Lakini tofauti na wakati ule akiwa sokoni, safari hii ile flash yake ilikuwa imerejea shingoni.
Atakuwa ameichukua kwenye gari?
Labda kwenye mizigo ya Viva au?
Nilifika kwenye gari huku mapigo ya moyo yakienda kasi.
Nilianza kukagua kuona kama kila kitu kilikuwa kama nilivyokiacha.
Ndiyo kila kitu kilikuwa mahali pake, japo sikuwa na uwezo wa kuthibitisha hilo kwa mizigo ya Viva kwa vile skiwa najua undani wa mizigo yake. Hiyo haikuondoa wazo kuwa Kumbamasaka alipata ile Flash kwenye mizigo ya Viva kwa vile yeyé ndiye alikuwa nayo.
Nilimwangalia Kumbamasaka akipotelea kwenye kundi la wafanyabiashara wa matunda waliokuwa eneo hilo. Huyu mwendawazimu ananifanya mwendawazimu sasa.
Nilichukua shajara yangu nikaandika vitu nilivyodhani vinafaa kuingia humo. Nikaliacha lile gari huku ufunguo wa gari hilo nikiuacha ndani ya gari.
Nikaanza kutafuta mabasi ya kwenda Kampala.
Sikuwa na hamu na yule mwendawazimu. Ukweli ni kuwa sasa nilikuwa namwogopa. Kila nikikumbuka jinsi alivyopigana na Viva na kumwua kwa ile staili ya aina yake sikuwa nataka kuonana naye tena.
Sikufanikiwa kupata basi, bali gari dogo tu ambalo lilikuwa likielekea Kampala.
Baada ya kukamilisha utaratibu wa kupiga mihuri pasipoti yangu, upande wa Tanzania na Upande wa Uganda, safari ikaanza.

Kutoka Mutukula hadi Kampala ni umbali wa kama kilometa 224 hivi. Hii ni kama ukipitia barabara ya Masaka na Kakuto. Mwendo kama wa saa tatu hivi. Tuliwasili Kampala majira ya saa tano na robo usiku.
Badala ya kutafuta sehemu ya kulala, nilitafuta teksi ya kukodisha ambayo ningeendesha mwenyewe. Sikuwa mgeni Kampla, hivyo nilijisikia huru zaidi kuwa na gari ambalo ningeendesha mwenyewe. Nilifanikiwa kupata gari na kuanza safari kuelekea Entebbe ambako ndiko kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa. Kutokana na utafiti wangu, ndege toka Tanzania ingewasili saa sita na robo usiku.
Lengo langu ilikuwa ni kuona kama Jacob Matata angewasili niweze kuongea naye.
Niliwasili Entebbe majira ya saa sita kasoro dakika kumi. Baada ya kuegesha gari nilielekea upande wa kungojea abiria wanaowasili. Nilisimama hapo nikiwa naangalia kila abiria anayetoka. Baadaye tangazo la kuingia kwa ndege toka Tanzania lilivuma. Hapo umakini wangu ukaongezeka. Abiria waliendelea kutoka lakini sikufanikiwa kumwona Jacob Matata.

Ilikuwa saa sita na dakika arobaini wakati ambapo nilimwona Jacob Matata akiwa anatoka. Nilipata tabasamu usoni. Nilijisikia mwili umepata joto. Namjua rafiki yangu. Najua uwezo wake na udhaifu wake. Tofauti na matarajio yangu, Jacob Matata alikuwa ameandamana na msichana mmoja mrembo. Msichana huyo hakuwa na mzigo wowote, lakini nilipoangalia mabegi aliyokuwa akiyasukuma Jacob Matata kwenye kitoroli cha kubebea mizigo, nilijiridhisha kuwa hayakuwa ya Jacob peke yake, ilikuwa mizigo yao wote wawili. Haraka niliekea kwenye gari langu, lengo langu ikiwa ni kumfuatilia Jacob Matata kwa nyuma.
Nikaingiza ufunguo kwenye gari huku macho yakiwa kwa Jacob Matata na yule msichana. Walionekana kuongea kwa bashasha.
Hiyo ilikuwa ni kawaida ya Jacob Matata. Viumbe hawa huwa hawampi shida. Utadhani huwa ana kamzizi fulani hivi, lakini ukimuuliza mwenyewe siri inayomfanya awapatie sana viumbe wa kike hasa warembo, angekupa jibu moja tu ‘kuwa mwanaume, wanapenda mwanaume aliye mwanaume.’
“Fafanua kidogo Jacob?” Nilimuuliza wakati tukiongea kuhusu hiyo mada wakati fulani.
“Wao ni wanawake warembo, wanatabia zao. Hawana shida na uanamke, urembo na tabia zao, wanavutiwa na mwanaume mwenye uanaume wa kuwasisimua!” Jacob aliniambia.
“Mfano wa huo uanamume?” Nilizidi kuhoji.
“Ni suala la asili, lakini mfano, mwanaume hana maneno mengi, hujibu maswali moja kwa moja bila maelezo mengi. Halafu kama unaomba ndizi sema naomba ndizi. Mwanamke husisimuliwa na mwanaume anayemfanya yeye ajisikie mwanamke. Tofauti na wanaume wengi wanavyodhani, mwanamke hapendi kuombwa wala kubembelezwa. Wanaume wengi ambao hutumia mtindo huo huwakosa viumbe hawa. Badala yake wanawake wanapenda mguso, mguso wa hisia na mazingira mazuri ambayo yatamfanya ajisikie salama na amani kusikiliza unachosema. Badala ya kubembeleza na kuombaomba, mweleze ukweli wa kile utakacho, katika lugha ya kiume siyo ya kike.” Hiyo ilikuwa sehemu ya majibu ya Jacob Matata.
Ama kwa hakika Jacob Matata rafiki yangu aliwajua viumbe hawa. Walipokuwa wanakaribia kufika upande huu ambao teksi zinaegeshwa mara nikaona kuna msichana mwingine anakuja kumpokea huyu msichana aliyekuwa na Jacob Matata.
Nilipomwangalia vizuri nikapigwa na butwaa.
‘Mungu wangu!’ Nilijisemea.
Nikabaki mdomo wazi. Mapigo ya moyo yakaanza kunienda kwa kasi sana. Haiwezekani, labda naota.
Alikuwa ni yule mwanamke aliyesuka twende kilioni, ambaye alikuja kuniletea chakula pale Kituo cha Polisi.
Ambaye nilimsikia Chogo akimwita kwenye simu ya upepo kwa jina la Zoazina. Mara moja nikajua Jacob Matata alikuwa mikononi mwa adui. Sikuwa tayari kuona hilo likitokea mbele ya macho yangu. Hivyo nikaacha ufunguo na kushika kitasa cha mlango wa gari ili niende walipokuwa. Wakati nikifungua mlango ghafla nikahisi kama kuna mtikisiko nyuma ya gari. Ile nataka kugeuka nikashitukia napigwa na kitu kizito kichwani.
Lilikuwa pigo la nguvu na zito.
Nikasikia kichwa kimekuwa kizito sana kiasi kuwa sikuwa na uwezo wa kukizungusha.
Nikaanza kuona giza.
Fahamu zikanitoka.

Ilikuwa kama naota ndoto vile.
Lakini baadaye nikatambua kuwa sikuwa naota.
Ni fahamu zilikuwa zikirejea taratibu na hivyo masikio yakawa yanasikia. Kwa mbali sana.
“Nasikia wameweza kumkamata. Ila kaua wengi.” Sauti ya kiume ilisema kwa lafudhi iliyoashiria kuwa msemaji alikuwa ni Mganda.
“Jamaa hatari sana, kwenye pambano moja kuweza kuwaua Jenerali Alice na Kigi Mbonea si mchezo!” Mwingine alisema kwa kusifia.
“Mbona wamesema kaua watu saba akiwemo Zoazina na Kigi, sikujua kuwa na Jenerali Alice ameuawa. Duuuh, si mchezo maana yule mwanamke alikuwa kama mzimu!” Yule wa kwanza alisema.
“Sasa Zoazina si ndiyo Jenerali Alice, ila limezoeleka Zoazina.” Mwingine alisema.
“Aaah! Sasa nimeelewa. Ila hata mzee wangu alinisimulia kuwa Watanzania ni wazuri sana kwenye hii fani.” Huyu wa pili alisema.
“Mzee wako yeye alijulia wapi?” Yule wa kwanza alihoji.
“Si alikabiliana nao wakati wa ile vita ya Amin. Anasema wale jamaa ni wapole ila ukiwakorofisha ni wabaya kuliko shetani. Sasa nasikia huyo kijana ni balaa.” Yule wa kwanza alijibu.
Hisia kuwa wanamwongelea Jacob Matata zilinijia.
“Huyu naye asije kuwa kama yule!” Yule wa pili alisema kwa woga.
“Huyu hapana, wanasema yeye ni mwandishi wa vitabu. Wewe humwoni tu alivyokaa, mwili wenyewe unaonekana wazi hauna mazoezi huo. Halafu hata angekuwa kwa jinsi tulivyomfunga, ni mzimu tu unaweza toka hapo.” Alisema yule wa kwanza.
Kauli hiyo ikanifanya nifumbue macho. Sikuona kitu.
Nilikodoa zaidi ili niweze kuona.
Nikashangaa kwa vile hakukuwa na tofauti kati ya kufumba na kufumbua macho. Kote sikuweza kuona.
Giza!
Hatimaye nilibaini.
Chumba nilichowekwa kilikuwa na giza zito utadhani uko ndani ya blanketi zito jeusi.
Nikajaribu kujitingisha.
Ndipo nikabaini kwa nini yule jamaa mwingine alisema ni mzimu tu unaweza kujitoa hapo.
Nilikuwa imefungwa vizuri sana.
Nilisikia maumivu kwenye sehemu ambazo kamba zilipita.
Nikataka kuongea kuwataarifu kuwa nilikuwa nimezinduka wanifungue.
Hapo tena nikagundua jingine.
Kinywa changu kilikuwa kimefungwa kwa namna ambayo nisingeweza kutoa sauti.
Halafu nikagundua jingine.
Nilikuwa nimebanwa sana mkojo. Kibofu kilikuwa kinauma. Hilo likaanza kunisumbua sana.
Nilijaribu kufikiria niko wapi. Lakini ilikuwa wazi isingekuwa rahisi kujua.
Jacob Matata angekuwa wapi? Nilijihoji.
Bila shaka ndiye aliyeua watu saba. Akiwemo yule mwanamke aliyesuka twende kilioni. Na Kigi Mbonea. Ila wanasema hatimaye wameweza kumshika, yuko wapi.
Wakati nikiwaza hayo mara nikasikia vishindo vya watu wakija.
“Fungueni huo mlango haraka, huyu jamaa mzito sana tofauti na mwili wake unavyoonekana!” Nilisikia sauti ikitoa amri huko nje.
Amri ikaheshimiwa.
Mlango ukafunguliwa, taa ikawashwa.
Nilikodoa macho kutazama.
Waliubamiza chini mwili wa mtu waliyekuwa wamembeba.
“Mfungeni haraka tuondoke. Chogo amesema anataka amuue yeye mwenyewe!” Jamaa mmoja alisema huku akishusha pumzi nyingi.
Nilipomwangalia vema mtu waliyembwaga chini, japo uso wake ulikuwa upande wa chini. Nilitambua kuwa alikuwa ni Jacob Matata.
‘Basi, kazi kwisha. Nilizoea yeye kunisimulia, leo najionea laivu huku na mimi mwenyewe nikiwa nakufa.’ Niliwaza kwa huzuni.
Jinsi walivyombwaga chini na jinsi mwili wake ulivyokuwa umelegea huku ukiwa na damu nyingi, nilijua hakuna namna.
Sasa nikajikuta nawaangalia wale watu. Hakuna hata mmoja aliyesumbuka kujua kama nilikuwa nimezinduka au la. Tofauti na wakati walipoingia, wakati huu nilikuwa nimefumbua macho kidogo sana. Hata mtu angenitazama angedhani macho yangu yamefumbwa.
Yalikuwa mapande ya watu, ila mawili kati yao niliyatambua. Moja lilikuwa lile jamaa lenye kipara ambalo nililiona kwenye ile nyumba ambayo nilikuwa nimetekwa nyara na Chogo. Halafu mwingine ndiyo yule aliyeniambia, ‘Angalia juu, tunaona kila unachofanya’.
Jumla yao walikuwa watano. Mimi niliwatambua wawili tu.
Kilikuwa chumba kidogo sana kama mita nne kwa nne.
Kulikuwa na nguzo kama sita za chuma zilizokuwa zimesimamishwa ndani ya chumba hicho. Ndipo nikabaini kuwa nilikuwa nimefungiwa kwenye nguzo mojawapo. Sakafuni kulikuwa na damu zilizogandamana.
Zilikuwa nyingi zaidi chini ya kila nguzo.
Hii ilimaanisha kuwa chumba hiki kilikuwa maalum kwa ajili ya kutesea au kutolea uhai wa watu.
Nilijaribu kutingisha vitanga vya miguu yangu. Vilicheza. Hapo nikajua kuwa sikuwa nimegusa sakafu. Nilikuwa nimefungwa kwenye nguzo kwa kuning’inizwa kama Yesu msalabani.
Mmoja alishika kamba. Halafu wanne wakainama kumnyanyua Jacob Matata.
Sikuamini nilichokiona.
Nilifungua macho yote na kuyatoa pima. Ilikuwa kwa kasi ambayo si rahisi kuisimulia. Ilikuwa ni kwa namna ambayo, huwezi kuamini kuwa binadamu anaweza kujifyatua. Lakini ndicho nilichoona Jacob Matata akifanya.
Wakati wawili wakiwa upande wa kichwani na wawili upande wa miguuni, tayari kwa ajili ya kumnyanyua. Kama umeme, mmoja wa mbele alipokea kichwa kikali sana na mmoja wa nyuma alipata teke la kwenye paji la uso.
Wote wawili wakarushwa na kujibamiza ukutani.
Wale watatu wakahamaki. Kitendo kilichofanya wapoteze sekunde kadhaa kabla ya kufanya maamuzi. Jacob Matata alitumia sekunde hizo kumrukia mmoja wa wale jamaa walioanguka na kunyakua bastola.
“Kill him!” Alifoka yule mwenye kipara huku kila mmoja akichomoa bastola kwa lengo la kumuwahi Jacob Matata. Walishamwona alichokuwa anafanya na jinsi alivyotumia mwanya wa zile sekunde kadhaa walizokuwa wamepigwa bumbuwazi.
Wakati akimalizia ile kauli yake ‘kill him’ wawili wengine walikuwa wameshachukuliwa na risasi za bastola ambayo sasa Jacob Matata alikuwa anaitumia. Lazima nikiri kuwa, kama mwandishi ambaye nimekuwa nikiandika simulizi nyingi zinazomuhusu Jacob Matata, hapo ndipo niligundua kuwa sikuwa na uwezo wa kusimulia kikamilifu baadhi ya matukio ambayo Jacob Matata alikuwa akifanya.
Ile kasi!
Ile shabaha!
Yale mapigo na mazingira aliyokuwa nayo!
Labda ni rahisi tu uone kwa macho lakini kuiweka kwenye maandishi ni mtihani mkubwa.
Yule jamaa mwenye kipara hakuwa amepatwa bado. Hivyo aliachia risasi kadhaa pale alipokuwa ameangukia Jacob Matata. Nilifumba macho kwa hofu maana nilikuwa na hakika amekwisha.
Nilipofumbua macho, wakati huohuo nikamwona Jacob Matata akiwa anamkumba yule kipande cha mtu. Wote wakaanguka na kujibamiza kwenye nguzo.
Hapo ukatokea mnyukano mkubwa. Jamaa alimbana na Jacob Matata hadi macho ya Jacob yakawa yametoka kama ya mjusi aliyebanwa na mlango. Ila kwa jinsi walivyokuwa hakuna aliyekuwa na uwezo wa kumpiga mwenzie.
Kuona hivyo jamaa akamwachia Jacob halafu akamuwahi kwa teke. Teke likamwingia vema Jacob.
Jamaa akarusha ngumi. Ikampata Jacob, akayumba.
Kuona hivyo jamaa akarusha teke moja kali sana akiwa amelenga shingo ya Jacob Matata. Kwa namna ambayo siwezi kuelezea, Jacob alijiminya kiasi, shingo ikatoka kwa sentimeta chache toka kwenye nguzo. Teke la jamaa likaiparaza nguzo ya chuma. Kama lile teke lingeipata shingo ya Jacob Matata, ingekuwa ni sawa na kuponda kichwa cha nyoka aliye juu ya mwamba. Jiwe juu, jiwe chini. Kichwa husambaratika.
Kukwepwa kwa lile teke kukamfanya mpigaji ayumbe kidogo.
Halafu hapo nikaona kitu kingine cha kushangaza. Jacob Matata aliruka kwa kasi na kuudaka ule mguu wa jamaa. Halafu, kwa kutumia nguzo ya chuma akaupindua ule mguu sehemu ya goti. Mlio kama wa muwa unaovunjika ukasikika.
Jamaa mwenye upara akatoa mlio wa maumivu.
Wakati huohuo akachomoa kisu, hapo tena nikamwona Jacob Matata akiruka namna ambayo naweza ifananisha na tiktak ya wacheza mpira. Akapiga teke bega la yule jamaa. Pigo lile likamtegua bega, kisu kikaanguka chini.
“Yuko wapi?” Jacob Matata alifoka.
“Si huyo hapo!” Jamaa alisema huku akiniangalia mimi. Alikuwa akihema kwa pupa utadhani mtu aliyekurupushwa na nyati.
“Unajua simaanishi huyu!” Jacob Matata alisema.
“Nani sasa?”
“Juliana Owima!”
“Fala wewe, utakufa kifo kibaya!” Jamaa alisema halafu povu likamtoka mdomoni. Nukta chache baadaye akajipiga piga kwa namna ya kukata roho. Akawa amekufa. Jacob Matata akatambua kuwa jamaa alikuwa ameamua kujiua kwa kutumia kidonge cha sumu ambacho majasusi kama hili hutumia kujiua. Kidonge hicho hufichwa kinywani kwa namna maalumu, kikiwa kimefunikwa vema kisimdhuru mwenye kuwa nacho. Ila jasusi anapoona hali mbaya, huking’ata na kukipasua. Ndipo hufa.
Jacob Matata alikuja pale nilipokuwa nimefungwa na kuanza kunifungua.
“Duuuh hongera aisee!” Nilisema kwa mshangao.
“Hatuna muda hapa, hebu twende zetu!” Jacob Matata alisema wakati akimaliza kunifungua.

Ilikuwa yapata saa kumi na nusu alfajiri wakati ambao mimi na mpelelezi, Jacob Matata tuliwasili Ntinda Hill View Hotel. Tuliamua kwenda kwenye hoteli hii ambayo haikuwa ya hali ya juu wala ya chini, kwenye eneo lenye kona na vilima la Ntinda jijini Kampala.
Ina maanisha nilikuwa nimepoteza fahamu kwa muda mrefu sana. Tangu wakati ule nilipopigwa na kitu nikiwa uwanja wa Ndege Entebbe hadi wakati nilipopata fahamu na muda huu ambao tunafika Ntinda Hill View Hotel, ilikuwa muda mrefu. Nilikuwa na hamu ya kujua nini kilitokea kwa Jacob Matata. Lakini niliona nisubiri wakati mwafaka ili niulize hilo.
Saa moja na nusu asubuhi, tulikuwa tumemaliza kila kitu.
Usafi, kufunga jeraha za Jacob Matata na kufanya mawasiliano muhimu.
Jacob Matata alikuwa ameshafanya mazoezi ya kunyoosha viungo na kupata kifungua kinywa.
Ndipo ukaja wakati niliokuwa nausubiri.
“Kabla sijakwambia ninayotaka kukuambia, tangu nikiwa Kigoma na kuja hapa. Naomba uniambie ilikuwaje mbele ya wale wanawake wawili?” Nilimuuliza.
“Sikujua kama ulikuwepo pale kiwanjani. Nilikujakujua baadaye. Sijui nianzie wapi?” Jacob Matata alisema.
“Anza popote ambapo pataleta maana nami nitaweza kuelewa.” Nilisema.
“Ngoja nianzie nilipokuja Kigoma.”
“Nadhani najua kwa sehemu hiyo.” Nilisema.
“Unajuaje?” Aliuliza.
“Ulipofika ulishindwa kunitafuta kwa vile ulipata wito wa haraka kurudi Dar. Ila ulionana na Neema na mkawa marafiki, ukalala kwake. Sivyo?”
“Umejuaje yote hayo. Kwani Neema alifanikiwa kuonana na wewe kabla hajauawa?” Jacob Matata alihoji.
“Ndiyo, kwa heshima yako alijitolea kunisaidia. Akanificha nyumbani kwake. Bila shaka wakajua kuwa amenificha nyumbani kwake, wakamuua.”
“Okay, sasa ndiyo najua kwa nini walimuua.”
“Si hivyo tu, najua ni kwa nini uko hapa.” Nilimwambia.
“Nimeshangaa umejuaje. Sikutegemea wewe kuwa hapa.”
“Nikiwa kwa Neema, nilipokea ujumbe wa faksi, bila shaka mwandishi ni ama anafanya kazi ofisini kwenu au basi ana uwezo wa kupata mazungumzo yote yanayofanyika kwenye ofisi yenu. Alimtumia mazungumzo baina yako na Bi. Anita, juu ya kukamatwa kwa Juliana Owima. Halafu akamtumia Kigi Mbonea. Ila nadhani hakuwa anajua kuwa Kigi Mbonea tayari alikuwa ameshakuja Kampala akiwa anaandamana na Juliana mwenyewe. Huku Kigi akiwa kama dereva teksi ambayo Juliana aliikodisha. Hivyo ujumbe huo wa faksi uliingia wakati nikiwa nyumbani kwa Neema ambaye alikuwa akiishi na Kigi kama wapenzi. Nilipousoma ulikuwa na kila kitu mlichozungumza. Lazima nikiri kuwa aliyeandika ule ujumbe alikuwa anauwezo wa kusimulia kila kitu. Hapo ndipo nikajua kuwa kuna kitu kikubwa kinatokea hapa Kampala na kuwa wakati wowote wewe ungetakiwa kuja Kampala. Hivyo nikaharakisha kutaka kuja Kampala.”
“Okay, sasa nimepata picha. Nimeshamjua ni nani aliyefanya hivyo pale ofisini kwetu. Hilo niachie mimi. Basi kumbe unajua mengi tayari. Kwa hivyo ukawa unataka uniwahi ili uniambie kuwa nasubiriwa na adui ama?” Jacob Matata alisema.
“Haswaa! Lakini si unajua pia napenda kuandika visa vyako, hivyo akilini nilijua nimeshapata kitabu kingine. Hasa nikimfikiria yule mwendawazimu, Kumbamasaka Jitu la Watu na yaliyonipata Kigoma.” Nilisema.
“Sawa, nina hamu ya kujua nini hasa kilikupata, lakini ngoja nikusimulie kilichotokea. Hivyo nitaanzia wakati nikiwa ndani ya ndege. Ndege niliyokuja nayo ilipitia Kigali kabla ya kuja Entebbe. Hapo Kigali alipanda binti mmoja ambaye alijitambulisha kwa jina la Epiphania Ndezako. Ni Mtanzania. Kama kawaida, nikaanza kupiga naye story za hapa na pale. Lakini wakati naongea naye niligundua kuwa hakuwa msichana wa kawaida. Hakuwa na usichana, alikuwa ameshaathiriwa na matendo ya kiume. Hivyo nikaanza kumwekea shaka.
“Tulipotoka tu nje ya uwanja pale Entebbe nilikuona, ila nikajua mambo si shwari. Pupa haikuhitajika, pia nilikuona uko kama kuku anayetaka kutaga. Ulikuwa hujatulia kabisa, kwa mtu mwenye ujuzi kama wangu ingekuwa rahisi tu kujua hilo. Alipokuja yule mwanamke kutupokea, nilimtambua kuwa ni Jenerali Alice Lakwena, mtu hatari sana na msiri mkubwa wa Joseph Kony. Hivyo nikajiweka katika tahadhari ya hali ya juu. Nimesikia sifa nyingi za huyo mwanamke. Hivyo ilihitaji utulivu kuweza kushughulika na watu wataalamu kama huyo. Nilipopokelewa tu nikajua kuwa lengo lao halikuwa kuniua wala kukuua wewe kwa haraka. Uzoefu wangu kwenye haya mambo ulinionyesha hivyo.
“Wangetuua lakini kuna taarifa wanataka toka kwetu. Ulipotekwa niliona, lakini niliona kukusaidia ingehatarisha zaidi maisha yako na yangu pia. Nikajipa muda. Gari lililokuchukua wewe lilianza kuondoka.”
“Ile teksi waliiacha pale?” Niliuliza.
“Yes, walikushusha na kutumia gari jingine, ile taxi waliiacha palepale!”
“Basi baadaye itabidi niende kuchukua vitu vyangu ndani ya ile teksi, halafu nimrejeshee mwenyewe.” Nilisema.
“Siyo sasa lakini, maana sasa watakuwa wametanda kila mahali wakitusaka. Kazi kubwa niliyonayo hapa ni kumtafuta Juliana Owima na kurejea naye nyumbani.” Jacob Matata alisema.
“Sawa hamna shida. Haya nipe mchapo ikawaje baada ya mimi kuchukuliwa?” Nilisema kwa shauku.
“Gari nililokuwa nimepanda liliondoka huku yule Jenerali akiwa ni dereva aliyejifanya amekuja kumpokea rafiki yake. Wakati tukiendelea na safari, niligundua kuwa kulikuwa na magari mawili yaliyokuwa yakitufuata nyuma. Hivyo nikajua napambana na jeshi kubwa. Nikakusudia nianze kupunguza maadui. Kwa vile hawakuwa wanajua kuwa nimeshawashitukia, haikuwa kazi ngumu kutoa bastola na kuwaua wote wawili. Halafu nikaushikilia usukani mimi mwenyewe.
“Sikutaka kuwashitua hawa waliokuwa nyuma. Niliendesha hadi hoteli niliyopanga kufikia. Hoteli ambayo nilikuwa nimemwambia yule msichana niliyekuwa naye kwenye ndege. Nilikuwa na hakika atakuwa tayari ameshawataarifu wenzie kuhusu hilo. Hivyo nilitegemea mapokezi hotelini lakini pia, hawa walioko nyuma wangeongeza kashkashi.
“Nilifika Hilton, nikaegesha gari. Mwanzo nilipata wasiwasi kuwa labda wasingewaona wenzao wangetilia shaka. Lakini nikakumbuka kuwa gari hili alilokuja nalo Jenerali Alice au Zoazina lilikuwa na vioo vyeusi. Hivyo mtu asingeweza kuona ndani. Nilishuka nikalifunga gari na kuelekea mapokezi.
“Nikiwa mapokezi niliweza kuwaona vijana wengine kama watano hivi wakiwa na sura za kazi. Nikajua hawa ndiyo waliokuwa wakinisubiri. Dakika tano zilipotea kwa watu wa mapokezi kumwondoa kwa nguvu mwendawazimu mmoja aliyekuwa ametokea upande wa vyumba vya kulala wageni. Alikuwa ameshika kuku ambaye alikuwa amemnyonga shingo na kufanya damu imtapakae kwenye mavazi yake machafu.
“Baada ya purukushani ya wahudumu wa mapokezi na yule mwendawazimu kuisha. Nilijiandikisha. Nilipomaliza kujiandikisha, mhudumu wa pale mapokezi akanisubirisha pasi na sababu za msingi. Wakati huo wale vijana wakatoweka mapokezi. Nikajua haraka maana yake nini. Walikuwa wameenda chumbani kuningoja. Hivyo niliingia chumbani nikiwa najua kabisa kuwa nangojewa. Niliingia kishari. Bastola mkononi tayari kwa lolote niliufungua mlango taratibu.
“Nikashikwa na mshangao. Chumbani kulikuwa na maiti tano. Zote zimeuawa bila muuaji kutumia risasi. Akili yangu ikafanya kazi haraka, kuwa inawezekana yule mwendawazimu hakuwa mwendawazimu. Sasa akili yangu ikawa kwako.
“Nilijua wengine wangekuja baada ya kuona wenzao hawaonekani. Kweli haikupita muda wengine walikuja, nikapambana nao, lakini nikiwa na lengo la kufika ulipo. Unajua maana yake?” Jacob Matata aliuliza.
“Hapana!”
“Walipobaki wawili, ilibidi nipigane kwa malengo ya kushindwa ili wanikamate. Kweli wakanidunda kweli huku nikijitahidi kujilegeza ili kuwaridhisha kuwa kipigo kinatosha. Waliporidhika ndipo wakawasiliana na wenzao kuwa niko chini ya ulinzi. Hapo wakanileta ulipokuwa. Pale sasa nikamalizia kazi ya kukupata!” Jacob Matata alihitimisha.
Nami nikachukua fursa hiyo kumsimulia kila kitu kilichotokea Kigoma na njiani.
“Nina hamu kujua, Juliana alipopiga simu pale, CHINGA BOY MAPHONE, aliongea na nani. Halafu nataka niangalie tena hiyo video iliyoko kwenye flash ya yule kichaa Kumbamasaka Jitu la Watu. Swali ni, je, watu hawa wananitaka mimi au Juliana? Je, Kumbamasaka ni mwendawazimu kweli au la? Juliana yuko wapi saa hizi?” Jacob Matata alimaliza maelezo yake.
“Hivi inawezekana kuwa yule mwendawazimu ni Kumbamasaka?” Niliuliza.
“Baada ya maelezo yako na ukweli kuwa ulimwona mpakani, ina maana yuko hapa. Na kuna kitu anafuatilia kwenye huu mkasa. Unasema ile video kwenye flash inaonesha nikiwa Kinshasa nyumbani kwa yule Jenerali mstaafu Mbanga Mbia Mbanga?” Jacob alimalizia maelezo yake kwa swali.
“Ndiyo! Ila tofauti na ulichonisimulia kuwa ulikuta Jenerali ameuawa, kwenye ile video inaonyesha wewe ukiwa unamuua Mbanga Mbia Mbanga. Halafu kuna jambo nalioanisha na ile video. Nilipotaja nyumba 511 kwa Viva Davis, haraka akakimbilia kutaja Nyabange Mbanga Mbia Mbanga. Na akataka kuonana na huyo mwendawazimu, ambaye mwishowe alimuua. Sasa nahisi kuna uhusiano wa huyo mwendawazimu na ile nyumba namba 511, mwendawazimu na Nyabange Mbanga Mbia Mbanga…!” Nilisema kama anayewaza vile.
“Mmmmmh! Naanza kupata hisia, Nyabange Mbanga Mbia Mbanga ni mtoto wa marehemu Jenerali Mbanga Mbia Mbanga. Ambaye aliuawa kwenye ule mkasa wa SAA 72. Inawezekana wakati anatafuta chanzo cha kifo cha baba yake, ndipo akakutana na hiyo video ambayo wewe umeiona. Inawezekana yuko kwenye kufanya kisasi cha baba yake, akiamini mimi ndiye niliyemuua baba yake. Hebu ngoja, unasema Viva alipomuona tu yule mwendawazimu kwa karibu walianza mapambano. Inawezekana Viva Davis alimtambua?” Jacob Matata naye aliuliza
“Inawezekana.” Nilijibu kwa kifupi
“Hebu ngoja niulize, kwa Bi Anita kazi ya Viva Davis ilikuwa nini. Halafu nipate picha ya Nyabange Mbanga Mbia Mbanga, ili nione anafanana vipi. Hapa nashindwa kuunganisha mambo matatu; Joseph Kony, Juliana Owima na kisasi anachotaka kufanya Nyabange Mbanga Mbia Mbanga.” Jacob Matata alisema huku akichukua simu yake. Bila shaka akiwa na nia ya kufanya mawasiliano.
“Baada ya kusikiliza maelezo yako, kuoanisha na matukio ya Kigoma nahisi hivi; kwenye ile Operesheni ya SAA 72 kuna watu walibaki na machungu. Wakaamua kukumaliza ili kulipa kisasi!” Nilisema.
“Wala hilo siyo jibu haswaa. Why Juliana Owima? Wewe unahusika vipi? Joseph Kony anahusika vipi? Huyo mwendawazimu anahusika vipi? Maana Joseph Kony anasema amemkamata Juliana Owima kwa sababu kuna taarifa za siri ambazo amewaibia, hii haina uhusiano na kisasi juu yangu. Nilipokuwa nakuja Kampala sikuwa nahusisha suala la Juliana Owima na matukio yako ya Kigoma. Lakini sasa naona kuwa yameunganika, wale watu walikutumia wewe kutaka kunipata mimi. Lakini wamemshikilia Juliana, sasa kama lengo ni kulipa kisasi, wangemuua tu Juliana na kutafuta namna ya kuniua mimi halafu ikaisha!” Jacob Matata alisema
“Labda wanajua kuwa kumuua Juliana kusingesababisha wewe kuja Kampala kwa hivyo wangelazimika kukusaka wenyewe. Kuendelea kumshikilia Juliana na kunishikilia mimi kungekufanya utoke mafichoni na kuingia vitani, kitu ambacho kimetokea!” Nilisema.
“Inawezekana ukawa sahihi, lakini najiuliza hivi Joseph Kony alikuwa na mafungamano na Joseph Katanga yule muasi wa Congo DRC ambaye nilimuua kwenye SAA 72. Halafu…” Jacob Matata hakupata kumalizia maelezo yake mlio wa ujumbe wa simu ulisikika. Aliichukua simu akasoma.
Baada ya kusoma alishusha pumzi ndefu.
“Yule mwendawazimu ni Nyabange Mbanga Mbia Mbanga mtoto wa Mbanga Mbia Mbanga. Kazi ya Viva ilikuwa ni kufuatilia tetesi kuwa kulikuwa na uwepo wa washirika wa karibu wa Joseph Kony mjini Kigoma. Washirika hao ambao ni makamanda wake wa juu kabisa tena watu wake wa karibu mno ni Lakoch Par Oyoo na Jenerali Alice Lakwena walikuwa wakionekana Kigoma mara kwa mara. Hivyo ikazua hisia kuwa walikuwa wanataka kuanzisha makazi yao ya siri hapo Kigoma. Lakoch Par Oyoo amekuwa akijiita Chogo na kama unavyojua sasa kuwa Jenerali Alice Lakwena alikuwa akiitwa Zoazina. Nikiangalia picha niliyotumiwa hapa, najiridhisha kuwa yule mwendawazimu ndiye Nyabange Mbanga Mbia Mbanga. Sasa nakumbuka kabisa kuwa sura hii ndiyo ya yule mwendawazimu niliyemuona pale hotelini usiku uliopita. Sasa kama yule mwendawazimu anaamini mimi ndiye niliyemuua baba yake kwa nini jana amewaua watu wa Joseph Kony? Halafu inanipa wakati mgumu kuamini kuwa Joseph Kony ametumiwa na watu wanaotaka kuniua ili kumteka Juliana. Kama ni uongo kuwa Juliana ameiba nyaraka za siri za kundi la Joseph Kony, je nini kilichomleta Juliana hapa Kampala?” Jacob Matata aliongea kwa tafakari.
Maswali na majibishano yaliendelea kwa muda kati yangu na Jacob Matata. Kwa kweli nilijisikia vema sana kuona sasa nilikuwa ndani ya kisa chenyewe tofauti na nyakati nyingine ambazo huwa naandika riwaya tu.
“Hii ndiyo maana ya upelelezi. Ukiwa na majibu yote inaondoa ladha ya kufanya upelelezi. Maswali na kiu ya kuyapatia majibu ndiyo huleta ladha ya upelelezi. Tuna maswali mengi, niko hapa kuyatafutia majibu. Hiyo ndiyo kazi yangu. Sina budi kubadili mtazamo niliokuwa nimekuja nao. Badala ya kudhani nakuja kumwokoa Juliana Owima, natakiwa nisiondoe uwezekano kuwa kukamatwa kwake ilikuwa ni wito wa kutakiwa kuja kwenye uwanja wa vita ili watu walipize kisasi.” Jacob Matata alisema.
“Tunaanzia wapi sasa?” Niliuliza kishabiki.
“Sikuhitaji kwenye hii kazi, wewe ni rafiki yangu, mwandishi wa vitabu, inatosha. Nitakusimulia. Itatakiwa ubaki mafichoni hadi kazi iishe, kazi hizi ni hatari sana. Ujue hapa napambana na watu ambao ni hatari sana, wamefundishwa kuua, wameshafanya mauaji, sasa ni mafundi wa kuua. Hawasiti kufanya hivyo, walikuacha hai kwa vile walikuwa wanataka kukutumia kunipata, sasa hivi wewe ni takataka tu kwao. Hivyo kaa mbali kabisa. Ila naomba unipe namba ya simu ya CHINGA BOY MAPHONE.” Jacob Matata alisema.
“Iko uwanja wa ndege, ndani ya gari niliyokuwa nimekodisha. Na wewe hutaki nitoke hapa.” Nilisema.
“Twende tukachukue halafu nitakurudisha hapa.” Jacob Matata alisema.

Ilikuwa yapata saa tatu na nusu asubuhi wakati tulipowasili sehemu ya kuegesha magari ya uwanja wa ndege wa Entebbe. Huu ndiyo uwanja mkubwa zaidi wa ndege nchini Uganda. Uko kwenye mji wa Entebbe, umbali wa kilomita 40 toka ulipo Mji Mkuu wa Uganda, Kampala. Jacob Matata alikuwa ameendesha gari tulilokuwa tumekodisha. Sehemu ya kuegesha magari ilikuwa imejaa. Lakini bado tuliweza kuliona gari nililokuwa nimetumia usiku. Lilikuwa palepale. Hata hivyo kwa sababu ya ugumu wa kupata sehemu ya kuegesha magari ilibidi tuegeshe gari letu mbali kidogo na lilipokuwa lile gari. Ilikuwa kama hatua 50 hivi toka kwenye lile gari.
“Nenda kachukue vitu vyako, gari liache palepale. Tutamfuata mwenye gari na kumwambia aje alichukue yeye mwenyewe. Si kila vita ni ya kupigana, wakati huu natakiwa nijue namna ya kuchagua watu wa kupambana nao. Kupambana na vibaraka haitanisaidia.” Jacob Matata aliniambia.
Nilitii huku nikijisikia raha.
Raha kwa vile sasa nilikuwa kwenye uwanja wa mapambano pamoja na Jacob Matata.
Kwa nini nisijisikie raha kuwa pamoja na mpelelezi maarufu na makini kama yeye?.
Namjua vema.
Najua anaweza kufanya nini.
Jana usiku nimemwona alichowafanya wale majitu.
Nilitembea kwenda kwenye ile teksi.
Nilipofika niliujaribu mlango wa gari.
Kwa jinsi nilivyochukuliwa jana sikuchukua chochote, hata ufunguo wa gari niliuacha palepale.
Mlango ulifunguka. Cha kwanza kuona ni ufunguo wa gari. Ulikuwa ukininginia pale pale pa kuwashia gari nilipokuwa nimeuchomeka jana. Halafu nikatupia macho kwenye kiti cha abiria. Niliona begi langu dogo la mgongoni likiwa palepale nilipoliacha. Nililiinua na kuliweka mgongoni. Nilifunga mlango wa gari. Nikawa nimekamilisha azma yangu. Moyo ukiwa umeridhika, nikageuka ili kuondoka hapo, ndipo nikakutana na kitu ambacho sikutarajia.
Teke kali likatua usoni. Nikasikia kizunguzungu.
Nilijaribu kuangalia nani aliyefanya hivyo lakini teke jingine la mgongoni lilinipata. Mpigaji alifanya kwa kasi kwa namna ambayo hakunipa nafasi ya kufanya chochote.
Nilipopigwa la shingoni nikaenda chini na sikukumbuka chochote kilichoendelea.

* * *

Nilikohoa kikohozi dhaifu sana wakati fahamu ziliponirejea. Nilipokohoa niliweza kuhisi jinsi kifua kilivyokuwa kinaniuma. Nilifumbua macho taratibu. Nilikuwa juu ya kitanda. Chumba cheupe. Nikajua nilikuwa hospitalini.
Mara mlango ukafunguliwa taratibu. Akaingia msichana mmoja mweusi akiwa amevaa mavazi meupe. Aliniangalia kwa muda bila kusema kitu. Nilijaribu kujitingisha sikuweza, nilikuwa nimefungwa bandeji nyingi. Nilipoona zile bandeji ndipo nikakumbuka yale mapigo niliyokuwa nikiyapata pale uwanja wa ndege Entebbe.
“Niko wapi hapa!” Nilisema kwa sauti dhaifu.
Yule msichana aliyevaa nguo za kiuguzi hakujibu kitu. Alitabasamu na kuminya midomo.
Baadaye mlango ulifunguka akaingia mtu mrefu mweusi sana. Mwembamba huku akionekana kutokuwa na afya njema.
“Ooooh! Umeamka! Pole sana Bwana Japhet!” Aliniambia kwa sauti yenye kukwaruza.
“Wewe ni nani na niko wapi?” Niliuliza.
“Naitwa Joseph Kony, hapa uko kwenye nyumba yangu ya siri ambayo huitumia kwa ajili ya mapumziko!” Alijibu bila kuuma maneno. Nilishawahi kusikia habari za Joseph Kony, lakini kwa vile anavyotafutwa sana sikutegemea angejitaja kirahisirahisi tu hivyo.
“Unataka nini kwangu wewe, mbona mimi sina kosa lolote!” Nilisema kwa kujitetea.
“Hakuna aliyesema una kosa lolote. Au umenisikia nikisema una kosa?” Joseph Kony alisema kistaarabu sana kiasi kuwa usingemdhania ni mtu hatari kupindukia.
“Infact, nimekuja kukujulia hali na kukushukuru kwa kunisaidia kuhitimisha kazi kubwa na ngumu iliyokuwa mbele yangu. Asante sana Bwana Japhet Sudi! Ukishapata nafuu, utaachiwa urejee Tanzania kwa amani.” Joseph Kony alisema maneno ambayo sikutaka kuyaamini kuwa ni kweli.
“Nimekusaidia kazi gani? Sasa hivi ni saa ngapi?” Niliuliza.
“Nitakuelezea kidogo kwa vile kazi imekwisha na sasa najisikia nimefufuka upya. Kazi uliyofanya ni kubwa mno. Umeuliza muda siyo?” Joseph Kony alisema.
“Ndiyo na ni kazi gani nimekusaidia?” Nilijibu.
“Oliva saa ngapi sasa?” Alisema huku akimwangalia yule muuguzi.
“Saa mbili na robo usiku!” Alijibu yule msichana muuguzi.
“Asante!” Joseph Kony alisema huku akimminyia jicho yule msichana aliyemuita Oliva. Halafu akanigeukia na kusema; “Sisi huwa hatutembei na saa wala simu kwa sababu za kiusalama. Vifaa hivyo ni hatarishi sana kwa ulimwengu wa sasa wa teknolojia. Nitakueleza kwa kifupi kutokana na muda. Natakiwa niondoke hapa haraka. Makazi yangu siyo Kampala, nilikuja hapa kwa kazi hii maalumu. Tofauti na ambavyo umekuwa ukisikia kwenye vyombo vya habari, mimi naongoza kundi la watu ambao wamechoshwa na mateso ya uongozi uliopo sasa madarakani. Uongozi ambao umedumu kwa miaka zaidi ya thelathini sasa. Japo wengi hawapendi kusikia, naweza kusema uongozi huu ni mbaya kuliko ule wa Idd Amin. Amin alikuwa muwazi na mkweli. Aliua watu hadharani, mazishi yakafanyia lakini huu wa sasa watu wanashindwa hata kufanya mazishi kwa vile haijulikani chochote.
“Labda nije kwenye suala lako na ambalo ndilo limenileta hapa Kampala. Miaka kadhaa iliyopita baada ya Rais Kabila kuingia madarakani, niliamua kuondoka kwenye misitu ya Congo, kwa kile nilichoamini kuwa Kabila alikuwa kwa ajili ya wananchi. Lakini nilianza kupata tetesi kuwa kuna makamanda wa kundi langu, wa juu sana ambao ni wasiri wangu wakubwa, nikaambiwa kuwa walikuwa na uhusiano na Joseph Katanga. Bila shaka unamjua vema Joseph Katanga na ubaya wake wote aliofanya Congo DRC. Wewe umeuelezea vizuri sana kwenye kile kitabu chako kiitwacho SAA 72. Sasa makamanda wangu wa juu walianzisha mahusiano hayo wakati kundi langu lilipokuwa limeweka makazi yake ya muda kwenye misitu ya Congo DRC. Jambo hilo lilifanya nitulie na kusitisha operesheni zangu za kawaida kwa muda ili kujipa nafasi ya kuchunguza ukweli wa mambo. Sikutaka kabisa kundi langu liwe na mahusiano na waasi wale wa Congo waliokuwa wakiongozwa na Joseph Katanga. Kama ingeonekana hivyo kwenye jamii ya kimataifa, ingekuwa ni kulipaka matope na kuharibu heshima ya kundi langu. Sikuwahi kumpenda Joseph Katanga, kwa hivyo jambo hilo liliniudhi sana.
“Baada ya mwaka hivi wa kuchunguza, nilijiridhisha kuwa makamanda wangu wanne, watu niliowaamini sana walikuwa na uhusiano wa karibu sana na Joseph Katanga, yule mbabe wa kivita wa kule Congo DRC. Walikuwa wakipokea kiasi kikubwa cha almasi na dhahabu kama malipo ya uaminifu wao kwake na kuna wakati wakawa wanamfanyia kazi kwa siri kubwa.
“Kuanzia hapo, utendaji kwa kundi langu ukashuka sana, huku wao wakiniuliza kulikoni. Wapo waliosema nimeugua, wapo waliosema nimeishiwa nguvu lakini mimi nilikuwa natafuta namna ya kusafisha bila kuleta athari kubwa ndani ya kundi langu. Wakati nikipanga kusafisha kundi, ilibidi wakati huohuo nipange namna ya kuwapata watakao warithi hao makamanda waasi!” Joseph alisema lakini nilimkatisha kwa swali.
“Unaposema kusafisha unamaanisha nini?” Niliuliza
“Kuwaua!” Alijibu hata bila kufikiria.
“Sasa kwani kulikuwa na ugumu gani?” Niliuliza.
“Kwa mwanajeshi anajua, mtu akiwa Kamanda wa Kikosi, kikosi kile kinamtii yeye kuliko mtu mwingine yeyote. Wao walikuwa chini yangu lakini askari wangu wote walikuwa chini yao. Hivyo ilihitajika mpango madhubuti wa kuwaondoa wao bila askari wao kujua kuwa nahusika na kuuawa kwao. Sasa hapo ndipo wewe na Jacob Matata mlipoingia.” Joseph Kony alinyamaza kwa muda huku akitabasamu, kuonyesha kuwa alikuwa akifurahia kile alichokuwa akiongea.
“Sisi tungekusaidiaje sasa?” Niliuliza.
“Sema mmenisaidiaje sasa?” Alinisahihisha.
“Okay, tumekusaidiaje?”
“Nilifanya mambo mawili ya msingi, kwanza ni kutafuta watu wenye nia kama yangu, yaani ya kutaka kuwaua hawa makamanda. Pili ni kuwawezesha kufanya hivyo. Wakati nikiwa natafuta namna, ndipo kikatokea kila kisanga cha kule Goma, Congo DRC. Joseph Katanga na watu wengine wazito wakauawa. Baadaye nikagundua kuwa Mtanzania aitwaye Jacob Matata ndiye aliyehusika na kumfuata Joseph Katanga katika shimo lake mwenyewe na kumuua kishujaa na ufundi mkubwa. Hapo nikajua kuwa makamanda wangu wasingekuwa na furaha dhidi ya mtu aliyesababisha Joseph Katanga auawe. Nilipopata taarifa kuwa umeandika juu ya kisa kile kwenye riwaya uliyoiita SAA 72, niliamua kukitafuta kitabu kile na kukisoma. Kitabu kile kilinipa taarifa za ndani juu ya kifo kile. Hapo nikaanza kuangalia nawezaje kuzitumia taarifa zile.
“Ndipo nilipoona kuwa miongoni mwa watu wazito waliouawa kwatika mkasa ule ni Mbanga Mbia Mbanga, ambaye alikuwa ni jenerali mstaafu wa jeshi la Congo. Nilikuwa najua kuwa kijana wa mzee yule alikuwa miongoni mwa wanajeshi matata wanaoibukia ndani ya Jeshi la Kinshasa. Kuaawa kwa baba yake kungekuwa kumemwacha na maswali mengi sana. Nikawa na uhakika kuwa angekuwa na hamu ya kupata ukweli juu ya kifo cha baba yake na ikiwezekana kulipa kisasi. Ndipo nikamtafuta lakini nikiwa na picha ya video ambayo ilikuwa imetengenezwa kiufundi sana na kuonyesha kuwa Jacob Matata ndiye aliyemuua. Taarifa hizohizo nikazipenyeza kwa wale makamanda wangu ambao sasa nilikuwa nawaona kama waasi. Haikuishia hapo, niliwafanya wote wajue kuwa Jacob Matata ni wa asili ya Kigoma na kuwa kila mwisho wa mwaka huwa anakwenda Kigoma kwa ajili ya mapumziko. Mtoto wa Mbanga Mbia Mbanga aitwaye Nyabange Mbanga Mbia Mbanga na wale makamanda wangu wakaanza kuimarisha uwepo wao huko Kigoma. Lengo lao wote ikiwa ni kumwinda Jacob Matata. Nilikuwa na ukaribu zaidi na Nyabange Mbanga Mbia Mbanga kuliko wale makamanda wangu na wala sikutaka wajuane kuwa wote walikuwa kwenye misheni moja.
“Ni mimi niliyemsimulia Nyabange Mbanga Mbia Mbanga juu ya kitabu chako SAA 72, na yeye akasema anaweza kutumia kitabu hicho kukupata wewe. Aliamini kukupata wewe inaweza kuwa njia nzuri ya kumpata Jacob Matata na hatimaye amlipie kisasi baba yake.
“Ulipoingia Kigoma, ndipo nilimwambia kuwa kuna makamanda wangu nao walikuwa kwenye kazi ya kumlipia kisasi Joseph Katanga. Sikujua kuwa hilo lingesababisha mimi na Nyabange Mbanga Mbia Mbanga tukosane. Kwa kuwa yeyé alikuwa akitaka kumlipia kisasi babaye wakati watu wangu walikuwa wakitaka kumlipia kisasi Joseph Katanga. Hakuwa hata anataka kulisikia jina la Joseph Katanga. Hivyo mawasiliano yangu na Nyabange Mbanga Mbia Mbanga yakakatika, huku nikiwa na hakika kuwa sasa asingemwinda Jacob Matata pekee bali angekuwa tayari kuwaua wale makamanda wangu. Inawezekana wewe hujui ila Joseph Katanga aliwasumbua sana Wakongomani, hivyo yeyote aliyekuwa rafiki yake ni adui yao pia. Ndicho alichohisi Nyabange Mbanga Mbia Mbanga, kama makamanda wangu walikuwa pale kumlipia kisasi Joseph Katanga, basi yeye aliona wanafaa kuuawa pia, maana bila shaka hao ni adui wa Kinshasa.
“Niliona kuwa hilo ni kosa zuri nililokuwa nimefanya na kuwa ningeua ndege wawili kwa jiwe moja. Makamanda wangu wangeuawa na Jacob Matata angepambana na Nyabange Mbanga Mbia Mbanga…” Joseph Kony aliongea na kukatishwa na swali toka kwangu.
“Kwa hivyo haikuwa lengo lako kumuua Nyabange Mbanga Mbia Mbanga, Jacob Matata wala mimi, ulitaka kututumia tu? Vipi kama ingetokea makamanda wako wangefanikiwa kuua wote, mimi, Jacob na Nyabange Mbanga Mbia Mbanga?” Niliuliza.
“Ingekuwa bahati mbaya, ningetafuta namna nyingine ya kuwamaliza makamanda wangu. Mambo hayo hutokea sana katika kazi zetu hizi.” Joseph Kony aliongea.

Kilichonishangaza au kunifurahisha juu ya mtu huyu, hakuwa mtu wa kuongea kwa mafumbo wala kufikiria kudanganya. Aliongea haraka huku msikiaji ukihisi umeambiwa kilichoko moyoni mwake.
“Eenh endelea!”
“Tangu mwanzo Nyabange Mbanga Mbia Mbanga aliamua kujianika kama mwendawazimu. Serikali yenu ilianza kumchunguza, Viva Davis alijiridhisha kuwa alikuwa ni mwendawazimu wa kawaida na kutuma taarifa ya kumsafisha. Kama si makamanda wangu Chogo, Zoazina na Kigi, ambao walikuwa wamefanikiwa kumnunua yule askari mwenye nyota tatu, basi Nyabange Mbanga Mbia Mbanga angemuua Jacob Matata mapema sana. Lakini sasa Nyabange Mbanga Mbia Mbanga ama Kumbamasaka, Jitu la Watu kama alivyojiita mwenyewe, aliamua kupanga vifo vya wote kwa pamoja. Hilo lilimchelewesha sana. Leo mchana Jacob Matata amefanikiwa kuwamaliza makamanda wangu wale wanne. Off-course nimepoteza na vijana wengine wasio na hatia, lakini ndiyo kawaida mti mkubwa uangukapo huangukia na miti midogomidogo iliyo jirani nao. Hapo ndipo nikazuia usiuawe na kuwa nataka uzungumze nami. Lengo la kuja hapa ni kukushukuru na kukuhakikishia kuwa uterejea nyumbani salama.” Joseph Kony alisema huku akisimama kutaka kuondoka.
“Kwa hiyo taarifa ya Juliana Owima ilikuwaje!?” Niliulizia.
“Hiyo ilikuwa ni Plan B ya kuwamaliza wale makamanda wangu. Kwa makusudi nilivujisha mpango wa kulipa kisasi aliokuwa nao Nyabange Mbanga Mbia Mbanga na makamanda wangu. Juliana Owima aliupata kama nilivyotaka. Kama unavyojua, Juliana Owima ndiye aliyemsaidia sana Jacob Matata katika ile operesheni ya SAA 72. Hivyo nilikuwa na uhakika wa mambo mawili; kwanza nilijua kuwa baada ya kusikia kuwa kuna kundi linataka kufanya kisasi dhidi ya Jacob Matata, basi Juliana angeingia vitani, hiyo ingemaanisha kuja Uganda na kuwasaka makamanda wangu, pili nilijua angefanya kazi hii kwa siri bila kuhusisha ofisi yake, kwa sababu asingetaka Jacob Matata aje kwenye operesheni hii. Maana kumfanya aje angekuwa anawasaidia makamanda wangu kumuua Jacob Matata. Hilo nikafanikiwa, Juliana akaja. Lakini alipofika tu ndipo nikamkamata na kutangaza taarifa zile za ukweli na uongo, lengo ni kufanya Jacob Matata aje na akisha kuja kwa siri nimwachie Juliana Owima. Hii ina maana makamanda wangu sasa wangewindwa na Jacob Matata, Juliana Owima na Nyabange Mbanga Mbia Mbanga, hapo niliongeza uwezekano wa makamanda wangu kuuawa. Na nilihakikisha wanapata watu wachache wa kufanya nao kazi.” Joseph Kony alisema lakini akakatishwa tena na swali langu.
“Kwa nini unasema taarifa za kukamatwa kwa Juliana na kundi lako zilikuwa za uongo na ukweli?” Niliuliza.
“Zingekuwa za ukweli kwa kundi langu, maana ni kweli alikuwa na taarifa za siri; niliwaambia makamanda wangu kuwa kama mwanamke huyo ameweza kujua kuwa tuna mpango wa kulipiza kisasi dhidi ya kifo cha Joseph Katanga, ni dhahiri kuwa ana siri zetu nyingine. Hivyo tunataka atupe kila anachokifahamu ndipo tumwachie. Ni uongo kwa sababu Juliana hakuwa na taarifa zozote na ningemwachia wakati wowote ili kuhakikisha kuwa anawaweka kati makamanda wangu. Nimefanikiwa, japo Juliana na Jacob Matata wako wanakutafuta kwa sasa.” Joseph Kony alisema huku akivuta pumzi ndefu.
“Kwa heri Japhet, najua utaandika riwaya juu ya kisa hiki. Usisahau kunitumia nakala ya kitabu. Najua askari wangu watajua ni riwaya tu na hawatoamini chochote kati ya uliyoandika!”
Alikuwa ameanza kupiga hatua kuondoka wakati mlango wa kile chumba chetu ulipopigwa teke na mtu akaangukia ndani. Wakati huohuo kwa namna ambayo sikujua ni macho yangu au uchovu, nilishangaa kuona Joseph Kony akitoweka kimazingara.
Mdomo ulibaki wazi.
Alikuwa ni yule mwendawazimu, Kumbamasaka Jitu la Watu.
Nilitetemeka kwa hofu wakati aliponiangalia kwa hasira.
“Nisamehe, sina makosa!” Nilisema
“Kumbamasaka Jitu la Watu!” Alisema huku akijipigapiga kifuani. Halafu akaongeza. “Nimesikiliza maongezi yenu yote, nimeelewa. Huyu jamaa ni mshenzi sana. Tuondoke, wote waliomwua baba yangu wameshauawa. Asante kwa Jacob Matata!”
Kumbamasaka alisema huku akianza kukiweka sawa kile kitanda nilichokuwa nimelalia. Alipohakikisha kila kitu kiko sawa. Alianza kukisukuma kwa mkono mmoja huku mkono mwingine akiwa ameshikilia bastola.
Tulipotoka nje ya kile chumba ndipo nilipoanza kuona maiti zilizokuwa zimetapaa ovyo ndani ya ile nyumba na nje.
“Wote hawa umewaua mwenyewe?” Nilimuuliza Kumbamasaka ambaye sasa nina uhakika kuwa ndiye Nyabange Mbanga Mbia Mbanga.
“Mutu ya Kongo hii, nilikuwa nimejiandaa, waliniulia baba yangu hawa. Kumbamasaka Jitu ya Watu!” Kumbamasaka alijibu.
“Ukweli idadi ile ya maiti usingeweza kuamini kuwa walikuwa wameuawa na mtu mmoja.
“Unanipeleka wapi?”
“Kwa rafiki zako!”
Ilikuwa ni nyumba iliyoko porini kabisa. Nje kulikuwa na magari kadhaa. Yule mwendawazimu alichagua gari moja na kuniingiza ndani. Japo nilikuwa na maumivu mengi lakini nilivumilia.
Aliwasha gari na kuliondoa.
“Sijaelewa namna Joseph Kony ameondoka kwenye kile chumba. Wewe umeelewa kweli? Hatimaye niliuliza
“Yeye natumia ndumba, shenzi sana hiyo mutu, natesa batu ba Juganda!” Kumbamasaka alisema kwa lafudhi ya Kikongo.

Aliendesha taratibu bila shaka ni kwa kunihurumia kutokana na majeraha mabaya niliyokuwa nayo mwilini. Kimya kilitawala kati yetu. Hatimaye wazo likanijia, nilikuwa na mtu aliyenifanya nifunge safari kwenda Kigoma. Labda huu ndiyo ulikuwa wakati mwafaka wa kumuuliza. Nafasi niliyoitafuta kwa jasho, nafasi ambayo kuipata kidogo inigharimu maisha yangu. Lazima niitumie sasa japo Joseph Kony ameshanisimulia mengi.
“Kwa nini unapenda kitabu changu?” Hatimaye niliuliza.
“Kiliniwezesha kuua ndege wawili kwa jiwe moja.” Alijibu.
“Kivipi?” Niliuliza.
“Mwanzo nilipanga kukitumia kukupata wewe halafu Jacob Matata, lakini sikuishia kukishika tu, nilipokisoma kilinifungua macho kuwa inawezekana natumika tu.” Kumbamasaka alisema.
“Kivipi?”
“Niliposoma jinsi ulivyoisimulia ile Opresheni SAA 72, nilijiridhisha kuwa inawezekana siyo Jacob Matata aliyemuua baba yangu. Na jinsi ulivyosimulia watu waliokuwa karibu na Joseph Katanga wakati akiwa kwenye himaya yake kulifanya nishindwe kujua aliyemuua ni nani hasa. Hivyo nilipenda kuwa nacho ili nikitumie kumhoji kwa kumsomea yeyote ambaye ningemshika kwanza.” Kumbamasaka alijibu.
“Kwa hivyo wewe siyo mwendawazimu?’ Niliuliza.
“Uliza swali jingine.’ Alijibu.
“Kwa nini ulimuua Viva Davis?’ Niliuliza.
“Siyo Viva Davis tu, nilimuua mzee KK na mkewe mdogo!” Alijibu kwa mkato.
“Kwa nini uliwaua?”
“Kwa ajili ya usalama wangu, Viva aliponiona alinitambua na kuniiita jina langu halisi. Hivyo nikajua niko hatarini. KK alikuleta wewe nilithibitisha shuku niliyokuwa nayo juu yake na mkewe. Alikuwa akija kuniona mara kwa mara, siamini kama alikuwa dereva teksi yule.” Alijibu.
“Hata mimi nilithibitisha hilo, alikuwa akitumiwa na Kigi Mbonea. Sasa kwa nini mwili wa mke wa KK uliupeleka nyumba namba 511?” Nilihoji.
“Sekunde chache kabla hujaingia chumbani kwako kuukuta ule ujumbe, mimi niliingia na kuusoma. Hivyo niliamua kumuua yule msichana kwa vile nilijithibitishia kuwa alikuwa upande wa wale watu. Kuupeleka pale lengo langu halikuwa kukukamatisha wewe bali kuwashitua wale watu. Hivyo hata wao bila shaka walishangaa kukuta ule mwili pale.
“Ndiyo ukadondosha flash yako?” Niliuliza.
“Sikuidondosha, niliiacha kusudi, ili wakiipata wachanganyikiwe.”
“Tulisafiri wote au?”
“Ndiyo! Wewe si mzoefu kwenye mambo haya, kwa hivyo tulikuwa wote kwenye gari hadi Mutukula.” Alisema.
Duuuuh!
“Asante kwa kitabu kizuri, nitawasimulia wanangu. Sikioni kama riwaya tu, bali kisa cha kweli ambacho kilisababisha mauaji ya baba yangu.”
Kumbamasaka aliegesha gari, The Kampala Serena Hotel. Hakunishusha, aliacha milango wazi na kuondoka.
Nikabaki nashangaa.
“Kumbamasaka Jitu la Watu!” Nilisikia akisema na kuingia ndani ya hoteli.
Hakurejea tena. Nusu saa. Saa nzima. Hakuonekana tena!

Saa tano na robo usiku ndipo nilipohisi kuna mtu ananyemelea gari ambalo nilikuwa nimetelekezwa ndani yake na Kumbamasaka. Sikuwa na uwezo hata wa kusimama, hivyo nilibaki ndani yake.
“Jeff!” Nilisikia sauti ya Jacob Matata ikiita.
“Jacob Matata!” Nilijibu kwa uchungu.
“Pole rafiki yangu!” Alisema huku akinikumbatia kwa furaha.
“Asante!”
“Nani kakuleta hapa?” Jacob Matata aliniuliza.
“Yule mwendawazimu.”
“Aaaaah! Hajakudhuru?”
“Alikuja kujua ukweli akawa upande wetu.”
“Kivipi?” Jacob Matata alihoji.
“Nitakusimulia. Hongera nasikia umewamaliza wote!” Nilisema.
“Nani kakwambia na amejuaje kuwa ni wote?” Jacob Matata alihoji.
“Joseph Kony.” Nilisema.
“Usiniambie umeonana naye?” Jacob alihoji kwa hamaki.
“Alikuja na kunisimulia kisa chote.”
“Ndiyo akakwambia kuwa nimewamaliza?”
“Ndiyo, anasema wale aliotaka uwamalize umewamaliza!”
“Yaani yeye ndiye aliyetaka niwamalize, kwani mimi nilikuwa nafanya kazi yake?” Jacob Matata aliuliza.
“Ndiyo rafiki yangu, safari hii hujafanya kazi ya Ofisi Fukuzi bali Joseph Kony, muasi wa Serikali ya Uganda!” Nilisema huku nikitabasamu.
“Duuuh au labda ndiyo maana alimwachia huru Juliana Owima katika mazingira tata na wakati mwafaka kama ule!” Jacob Matata alisema kwa sauti ya kutafakari.
“Inaonyesha tuna mengi ya kusimuliana hebu nitoe humu, yule mwendawazimu asijekuwa ameacha bomu humu.” Nilisema.
“Kweli, acha nikupeleke sehemu nzuri, halafu Juliana yuko kwenye gari ananisiburi. Nilikuwa nimekuja mara moja kuongeza risasi, yeye nikamwacha ananingoja kwenye gari. Nilipofika mapokezi ndipo nikaambiwa kuwa kuna mzigo wangu kwenye hili gari.” Jacob Matata alisema.
“Atakuwa ni Kumbamasaka huyo.” Nilisema
“Kwa hivyo anajua kuwa tunaishi hapa.” Jacob Matata alishangaa.
“Inawezekana, ila hana shida na ninyi tena, pia amesema asante kwa kumsaidia kulipiza kisasi cha baba yake kwa kuwaua wale makamanda wa Joseph Kony!” Nilisema.
“Kwa nini alimuua Viva?”
“Viva alimtambua na hivyo alijua atamdhuru.”
“Anyway. Twende tukaelezane yote kwa kina. Wewe unayo ya kusema, Juliana naye ana story yake, mimi pia ninalo la kukuambia tangu ulipochukuliwa pale uwanja wa ndege.”

****

Jacob Matata alishusha kile kitanda maalumu cha wagonjwa ambacho nilikuwa nimelazwa juu yake. Alikisukuma kile kitanda kuelekea upande mwingine wa kuegesha magari. Mara nikamwona mwanamke mmoja anakuja anatembea.
“Juliana, tumeletewa Japhet. Inabidi tujadili nini kinafuata!” Jacob Matata alisema. Hata kabla Juliana hajajibu, simu ya Jacob Matata iliita.
“Yes madam! Jacob Matata alisema baada ya kupokea. Aliisikiliza kwa muda halafu akashusha pumzi ndefu.
“Nimekuelewa, tutaondoka mara moja! Alisema halafu akakata simu.
“Vipi?” Juliana aliuliza kwa shauku
“Amri! Jacob Matata alisema
“Bi Anita? Juliana aliuliza tena huku akitabasamu
“Yap! Jacob Matata alisema huku akionyesha kutofurahia.
“Japhet, kutana na Juliana Owima, mtu uliyemuandika kwenye kitabu chako SAA 72. Juliana huyu ndiye Japhet Sudi, rafiki yangu mwandishi wa vitabu!” Jacob Matata alisema.
Juliana alisogea kwenye kitanda nilichokuwepo na kunipa mkono. Mkono wake ulikuwa laini ila wenye nguvu na imara sana.
“Nimefurahi kuonana nawe Japhet, lakini hesabu kuwa hatujawahi kuonana na mimi!” Juliana alisema halafu akasogea pembeni.
“Nimefurahi kuonana nawe pia. Hivi ninyi hebu niambie haya majina ndiyo majina yenu halisi au?” Nilijikuta nauliza
“Kwani wewe unaonaje? Jacob Matata alijibu kwa swali
“Nimeshawahi kujaribu ku-google ili nione lakini sijaambulia chochote. Ikanipa wasiwasi kuwa inawezekana majina haya ni ya kazi.” Nilifafanua
“Kwenye ulimwengu tunaoishi mambo muhimu yote yanafanywa kuwa si halisi bali mambo yasiyo na muhimu ndiyo huachwa kuendelea kuwa halisi” Jacob Matata alisema
“Sasa?” Juliana alihoji
“Tuliyekuwa tunamtafuta huyu hapa kitandani, niliyetumwa kumtafuta hapa Uganda ni wewe, Bi Anita anasema kuna ndege maalumu ambayo itatoa hapa hadi Dar usiku huu huu. Halafu kesho utaelekea Congo DRC.” Jacob Matata alisema
“Lakini tulikuwa jirani sana na kumpata huyu mshenzi kwa nini asituache?” Juliana alisema
“Anasema si salama kwa sasa, maana kuna adui wa ndani pale Dar ambaye inafaa ashughulikiwe kabla hatujaamua kumsaka huyu mtu.” Jacob Matata alisema.
“Adui gani?” Juliana alihoji.
“Okay, ambaye alikuwa akimtumia Kigi taarifa za kinachoendelea ndani ya ofisi yenu pale Dar es salaam?” Nilirukia maongezi yao.
“Hujakosea Japhet, inaonyesha kuna hali ya usaliti wa ndani. Hivyo mkuu wetu wa kazi ameona ni vema tukatoka kwenye uwanja wa mapambano kwanza hadi ndani pasafishwe.” Jacob Matata alielezea. Wote tukatingisha vichwa kuonyesha kuwa wazo la Bi Anita, mkurugenzi wa ofisi fukuzi, ofisi ambayo Jacob Matata na Juliana Owima walikuwa wakifanya kazi chini yake lilikuwa na maana na uzito.
“Sawaaaa!” Juliana alisema huku akishusha pumzi.
“Kwa mujibu wa Bi Anita, tuna masaa manne hadi wakati ambao ndege yetu hiyo itaondoka. Ina maana tutaondoka Uganda saa kumi asubuhi.” Jacob Matata alisema.
“Napendekeza twende moja kwa moja uwanja wa ndege tukangojee muda huo.” Nilisema kwa sauti ya mashaka.
“Hata mimi nadhani hivyo, maana na sasa najisikia kuwa kama chuma cha kilichokuwa kimepata moto halafu kikamwagiwa maji ya baridi ghafula.” Juliana Owima aliunga mkono wazo langu.
“Sawa, wengi wape.” Jacob Matata alisema.
“Sasa nyie ingieni garini mimi nikachukue mizigo yetu michache tayari kwa safari.” Juliana Owima alisema.
Wote tukaafiki.

Ilikuwa mwendo wa saa sita na dakika hamsini na nane wakati ambao tulikuwa tunaketi kwenye mgahawa mmoja ulioko ndani ya uwanja wa ndege wa Entebbe. Tulikuwa tumeshakamilisha taratibu zote za kupata vibali vya kusafiri na kukaguliwa pasi zetu za kusafiria. Mimi niliendelea kutumia kile kitanda maalumu ambacho kilikuwa na magurudumu hivyo kingemwezesha mtu kusukuma kama toroli.
“Amefurahi sana yule jamaa, nadhani alishadhani ameingizwa mjini.” Jacob Matata alisema
“Yupi?” Juliana alihoji.
“Si yule jamaa mwenye gari ambayo Japhet alikuwa ameikodish.” Alijibu Jacob Matata.
“We acha tu, ulimwona alivyofurahi ulipompa ufunguo wa gari hakuwa hata na haja na pesa.” Nilisema.
Wote tukacheka.
“Haya Jacob hebu niambie ilikuwaje nilipokuwa nachukua vitu vyangu pale garini? Maana baada ya kipigo sikujua nini kiliendelea.” Niliuliza nikiwa tayari kwa simulizi.
“Ukweli sikudhani tungekutana na hali kama ile, hivyo sikuchukua tahadhari yoyote. Nilikuja shituka dakika chache baadae wakati huo wewe hukuwepo. Nilikuta damu pale kwenye gari. Bahati nzuri mkoba wako ulikua pale chini. Niliuchukua na humo nikapata namba za simu za kile kibanda cha simu cha CHINGA BOY MAPHONE cha pale Bukoba. Haraka niliituma kwa mtaalamu wa mawasiliano wa ofisi fukuzi Dar es salaam. Ambaye hakuchelewa kuniambia kunipa namba ambayo Juliana Owima alikuwa amepiga. Cha ajabu akabaini kuwa mtu ambaye Juliana Owima aliwasiliana naye ndiye ambaye aliwasiliana na Lakoch Oyooo au maarufu kama Chogo. Mazungumzo ya kwenye simu yaliwawezesha wao kubaini hilo. Hivyo ikawa wazi kuwa mtu huyo alikuwa amemtega Juliana.” Jacob Matata alisema huku akimwangalia Juliana.
“Ni kweli, wiki chache zilizopita nilipigiwa simu na mtu huyo aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Drogba. Akasema niende posta nitapata mzigo wangu. Nilipokwenda posta nilipata flash disk ambayo ilikuwa inaonyesha mauaji ya Mbanga Mbia Mbanga. Lakini kwenye kipande kingine cha video niwaona wau kadhaa amba sura zao zilikuwa zimefichwa wakiwa wanapanga namna ya kumlipiza kisasi Jacob Matata kwa kosa la kumuua Joseph Katanga. Mara moja nikajua kuwa Jacob Matata alikuwa hatarini. Wakati nikifikiri nini cha kufanya, simu yangu ikapata picha za watu na majina yao na maeneo waliyokuwa wakiishi hapa Kampala. Mtumaji akiwa ni yule yule Drogba. Baada ya kutafakari sana niliamua nifuatilie suala hilo. Halafu kwa vile sikutaka Jacob Matata apate taarifa zile, niliamua kuja Uganda bila kuihusiha ofisi yetu, yaani Ofisi Fukuzi. Hapo ndipo nikaanza safari ya kuja Uganda, sikutaka kutumia ndege ili isije kuwa nimenasa kwenye mtego wa kunimaliza.” Juliana Owima alisimulia na kuvuta pumzi kidogo.
“Inawezekana ni mtu huyo huyo aliwasiliana na Kigi na kumwambia kuwa uko njiani. Kwani ulimwambia kuwa unakuja Uganda?” Niliuliza.
“Hapana ila niliwasiliana naye mara mbili nikiwa safarini, mara moja wakati niko kwenye mpaka wa Rwanda na Tanzania, hapo alinipigia yeye halafu mara ya pili nilimpigia nilipofika pale CHINGA BOY MAPHONE, Bukoba. Hayo yakawa mawasiliano ya mwisho na mtu huyo na nikaamua kuharibu ile simu na sasa nikawa naingia kwenye uwanja wa mapambano. Katika safari yote sikuwa na hisia kuwa Kigi alikuwa adui yangu.” Juliana Owima alisema.
“Kwa hivyo inawezekana walikuwa wanatumia yale mawasiliano kujua uko wapi. Walipojua uko kwenye mpaka wa Rwanda na Tanzania, wakajua kuwa ulikuwa unatumia usafiri wa barabara. Lakini kama ni hivyo si wangekumaliza ulipofika Kigoma?” Jacob Matata alisema.
“Kama nilivyokwisha wasimulia, kwa mujibu wa Joseph Kony alikuwa anamtaka Juliana Owima afike Kampala, ili aje aunganishe nguvu na wewe utakapofika Kampala. Inawezekana aliamuru aachwe ili akakamatiwe Uganda na ndiyo maana Kigi akamwendesha hadi Kampala. Kwa hivyo ulipofika Kampala Kigi alikuacha?”
“Aniache wapi? Nilipofika akanisaidia kutafuta hoteli ya kukaa. Nilipoingia tu chumbani haikupita hata nusu saa walikuja watu kunichukua. Walinikuta niko bafuni naoga, hivyo sikuwa na ujanja sana. Ndipo wakanishika mateka.” Juliana Owima alisema kwa sauti ya kuona aibu. Bila shaka ni kwa vile alisema walimkuta akiwa bafuni anaoga.
“Walikula kwa macho?” Jacob Matata alisema kwa mzaha.
“Nilijua tu utasema hapo!” Juliana alisema.
“Kwenye kazi humo humo saa nyingine huwa tunajilipa kwa matukio kama hayo.” Jacob Matata alisema. Halafu akaendelea “Basi kwa kushirikiana na mtaalamu wa mawasiliano toka ofisi fukuzi tukaweza kudaka mawasiliano ya Drogba na Juliana na hivyo nikaweza kujua huyo Drogba alikuwa akiishi wapi. Lakini pia nikazipata picha za wabaya wangu ambazo Drogba alimtumia Juliana Owima.” Alisimulia Jacob Matata.
“Kwa hivyo Joseph Kony yuko sawa kusema taarifa ya kukamatwa kwa Juliana ilikuwa ya uongo na ukweli kwa wakati mmoja. Maana taarifa alizomtumia Juliana zilikuwa za ukweli lakini si kweli kuwa alikuwa na siri nyingi za kundi hilo.” Nilisema.
“Yes, hapo Kony alikuwa sawa.” Juliana alisema.
“Hivyo nikaona sasa nimtafute huyo Drogba kwani ndiye angenifikisha kwa wengine. Kwa mujibu wa mawasiliano, mara nyingi Drogba alifanya mawasiliano tokea kwenye nyumba moja iliyoko Kitintale, sehemu moja iliyoko pembezoni mwa ziwa Victoria hapa Kampala. Kumbuka hapo nilikuwa nimepotelewa na watu wawili, Juliana na Japhet. Hivyo sikutaka kupoteza muda, nilielekea Kitintale na kuanza kutafuta mwelekeo wa hiyo nyumba. Sikupata shida nikaiona. Haikuwa na ulinzi wowote, hivyo kwa mbinu kidogo tu nikawa nimeingia ndani. Ilikuwa nyumba ya kifahari yenye vyumba vingi, kwa bahati mwenyeji wangu nilimkuta yuko sebuleni anafanya kazi kwenye computa. Hakutarajia ujio wangu, alishituka nusura apoteze mapigo ya moyo.
“Tulia, sina madhara kama utashirikiana nami! Nilimwambia. We nani unayeingia kwenye nyumba yangu bila ruhusa? Alifoka kwa sauti iliyochanganyika hofu na hasira.
“Imebidi, wakati mwingine hakuna namna,’ nilisema huku nikiegemea ukuta, bastola yangu mkononi yeyé akiwa bado amekaa vile vile nilivyomkuta.
“Juliana na Japhet wako wapi? Niliuliza.
Swali hilo lilikuwa kama radi, niliona jinsi alivyohangaika kuficha mshituko aliokuwa nao. Alibabaika kujibu.
“Unahakika unamuuliza mtu sahihi? Isije kuwa umekosea nyumba! Alijtahidi kusema
“Najua ninachokifanya, halafu nasikitika kuwa nina muda mchache sana wa kukuvumilia bwana Drogba! Nilipotaja jina lake alishituka tena.
“Wewe ni nani na unataka nini? Aliuliza
“Naitwa Jacob Matata, nataka kujua Juliana Owima na Japhet Sudi wako wapi?
“Kwa nini unadhani miye najua walipo watu ambao hata siwafahamu?
“Kwa sababu umekuwa ukiwasiliana na Juliana tangia alipokuwa Congo na kumpa maelekezo fulani fulani! Jibu langu lilimshitua zaidi. Tukiwa bado tunaongea nikasikia kishindo nyuma yangu, nikageuka kuangalia, likuwa ni jibwa kubwa mithili ya ndama. Niliwahi nikalitandika risasi, lakini kitendo kile kikampa nafasi Drogba, alinirukia na kunitandika teke la mbavuni. Halafu akanipa ngumi kali ya uso. Uzito wa mapigo yake uliniambia kuwa hakuwa mzuri wa kupigana. Nilijivuta pembeni kupisha teke lake jingine halafu nikampiga teke moja la wastani katikati ya mpaka wa kifua na tumbo. Akakohoa kwa taabu na kutema damu. Nikamfuata na mkuvunja mkono wa kushoto, akalia kwa uchungu sana.
“Haya niambie wako wapi?
“Sijui…! Sikumwacha amalize, niliunyonga tena ule mkono.
“Aaaaah niache nasema nasema!
“Haya sema la sivyo nakuua!
“Munyonyo nyumba namba 890! Alisema huku akihema kwa tabu.
“Joseph Kony yuko wapi?
“Huyo sijui, nimewahi kumwona mara tatu tu, huwa haonekani ovyo! Alisema kwa namna ambayo nilijua anasema kweli.
“Je walikuwa wanajua kuwa nakuja Kampala?
“Ndiyo!
“Walijuaje kuwa nakuja?
“Sijui, miye kazi yangu ilikuwa ni kumleta Juliana Owima!
“Kwa nini ulimtumia Juliana Owima picha za kweli za makamanda wa LRA?
“Niliamuriwa kufanya hivyo na baba!
“Baba ndiyo nani?
“Nabii Joseph Kony!
“Nabii?
“Ndiyo!
“Nabii kivipi?
“Huwa anaongea na Mungu na ndiye aliyemtuma kuokoa Uganda!
“Je makamanda walijua kuwa picha zao zimetumwa!?
“Amri ya Nabii huwa hawaambiwi wengine hadi akuwambie!
“Ukiwaambia je!?
“Huwa Mungu anamwonyesha na utashangaa amejua na adhabu yake ni kifo!
“Nani alikuwa anawasiliana na mtu wetu?
“Sijaelewa unamaanisha nini?
“Hakuna mawasiliano juu yangu mliyoyapata toka Dar?
“Hapana miye sijui chochote!
“Na um…..! Sikumaliza kusema wakati niliposikia gari likipiga breki kwa fujo nje ya nyumba. Nilimtia risasi yule mtu na kumvutia chumba cha jirani. Walikuwa wameshafika mlangoni sikuwa na muda wa kuficha maiti ya lile jibwa. Sehemu nzuri ya kusimama ingekuwa ni nyuma ya mlango ambao nilikuwa na hakika wangeingilia. Hivyo ili kuwahi upande ule, ilibidi niruke kama sarakasi mbili na kutua bila kelele. Niangalia sebule yote, ikawa wazi kuwa wa kwanza kuingia pale mlangoni macho yake yangevutwa na mzoga wa lile jibwa.
Sekunde chache baadae kulisika mlio kama wa saa, halafu mlango ukafunguka. Hiyo ikanijulisha kuwa alama ya kidole ilitumika kufungulia mlango. Aliingia wa kwanza, aliangalia pale ilipokuwa kompyuta ya Drogba, ni wakati huo huo yule wa pili aliingia.
“Shiit! Huyu wa pili alisema. Nikajua macho yake yatakuwa yameuona ule mzoga wa mbwa.
Haraka nikamlamba risasi yule aliyekuwa ameingia kwanza. Huyu wa pili alibaini risasi imetokea wapi. Aligeuka na kupiga teke mkono wangu bastola ikaangukia juu ya maiti ya yule wa kwanza. Jamaa aliruka sarakasi kwa wepesi wa karatasi halafu akanitandika teke moja zuri sana la begani. Tukawa tunatazamana. Kwa maelezo ya Japhet na picha ulizotumiwa Juliana na Drogba, sasa naelewa kuwa huyu alikuwa ni Chogo. Nakiri kuwa jamaa alikuwa fundi sana wa kupigana.
“Jacob Matata right? Alisema kwa dharau
“Chogo? Nilijibu
Aliachia mapigo matatu mfululizo, kwa namna ambayo ilinitatanisha. Mawili yakanipata. Moja nikaliona. Sasa nikajua kuwa nilikuwa nakabiliana na mtu wa kiwango changu.
Nilijitanua kidogo akaja, nikafyatua kwa mateke ya kufuatana, akayaona yote. Alipokuja akanipa wimbi moja la ngumi tatu zenye utata. Nikapatwa, lakini sikutaka wimbi liishe bure, hivyo nikazingusha na kumpa kichwa cha kisogoni. Hakutarajia, akaguna. Ghafla nikashangaa teke linatua kwenye shingo, wakati naugulia maumivu nilitafuta mwanya haraka. Korodani zake zilikuwa jirani sana nami, nilipiga ngumi kale kwenye korodani. Akaruka na kuinama kwa maumivu, kifuti kimoja cha nguvu kilikutana na paji lake la uso ambao ulikuwa umeinama. Akaanguka chini, nilimuwahi kwa teke jingine kwenye korodani halafu likafuata teke jingine. Teke la mauti likatua kwenye paji lake la uso. Teke hilo lilimpasua vibaya.
“Mwana wa Hayawani wewe Jacob Mataaaaa aaah!!!!! Ilikuwa ni kauli yake ya mwisho kabla hajakata roho. Jamaa alikuwa fundi sana wa kupigana. Nadhani katika maisha yangu nimekutana na watu wachache sana walio kama yeye!” Alisema Jacob Matata halafu akaweka pozi.
“Anamfikia Ben Kiroboto, Poka Kingu, Max the fuse au Ua Jekundu?” Nilisema huku nikijaribu kukenua meno. Nilikuwa na maumivu makali sana. Shukurani kwa dawa za maumivu nilizokuwa nimepewa.
“Ha ha ha ha wewe unawaza riwaya zako tu, jua tu kuwa jamaa alikuwa fundi sana. Nilipomuua huyo jamaa sikutaka kupoteza muda hapo, niliamua kwenda haraka kwenye nyumba aliyokuwa amenitajia Drogba.” Jacob Matata alisema.
“Eeenhe ikawaje?” Juliana Owima aliuliza.
“Akili yangu iliniambia kuwa mambo yote yangekuwa huko Munyonyo. Niliendesha kwa fujo sana. Nilipoanza kukaribia eneo la Munyonyo nilipunguza mwendo. Nikaanza kuitafuta nyumba namba 890. Niliipita Commonwealth Resort kwa mwendo wa wastani huku nikijitahidi kusoma namba za nyumba kwa usiri. Hatimaye niliipita nyumba namba 890. Nilirejea kwa miguu na kuanza kufikiria namna ya kuingia ndani. Tayari ilikuwa inaelekea kuwa saa moja kasoro hivi jioni. Nilipochunguza vema niligundua kuwa kulikuwa na ulinzi mkali sana eneo hilo. Hivyo nikaazimia kungojea kigiza kiongezeke kidogo. Ukiwa kwenye hiyo nyumba sauti ya mawimbi toka ziwani ilisikika.
“Saa mbili na robo usiku niliingia ndani ya jengo. Nilipitia upande wa kushoto wa jengo. Sababu ya kuchagua upande huo ni vile nilibaini kuwa ndiko kulikokuwa na jiko la nyumba hiyo. Uzoefu unaniambia kuwa ulinzi wa upande wa jikoni huwa ni tofauti na ulinzi wa mbele au nyuma ya nyumba. Hivyo nilinyataka kuelekea upande ule wa jikoni. Ilibidi niue walinzi wawili kabla sijaufikia mlango wa jiko. Wakati nikiwa nataka kushika kitasa cha mlango wa jiko ndipo nikasikia mlio wa bastola. Halafu nyumba yote ikawa giza. Nikashikwa na mshangao. Hisia kuwa ni Juliana ndiye amepigwa risasi zikanijaa. Niliparamia mlango wa jikoni. Kwa bahati nzuri ulikuwa wazi. Nilipoingia ndani nilihisi kama nimepishana na mtu. Halafu ni kama aliniita jina langu halafu akatoweka!” Jacob Matata alisema.
“Inawezekana ni Joseph Kony!” Juliana alisema.
“Kwa nini unadhani hivyo?” Jacob Matata alihoji.
“Saa mbili na nusu alikuja kwenye chumba ambacho nilikuwa nashikiliwa mateka. Tofauti na siku nyingine, alikuwa mtulivu sana. Aliniangalia kwa muda bila kusema kitu. Halafu hakuwa na mlinzi yeyote aliyeandamana naye. Baadae alinifungua na kunirushia bastola moja. Hata kabla sijaiokota ile bastola akaniambia; “jiponye mwenyewe, Jacob Matata yuko njiani kuja kukusaidia. Asanteni! Alipomaliza tu kusema hivyo ndipo ule mlio wa risasi ukasikika na nyumba yote ikawa giza. Nilikurupuka na kuichukua bastola halafu nikatoka nje ya chumba. Ilibidi nijibanze sehemu fulani ili kuyapa macho nafasi ya kuzoea giza. Sekunde chache baadae nikasikia vishindo vywa walinzi wakikimbia kuja upande huu wa chumba nilichokuwa.
“Mshikeni huyo mwanamke, msimuue, Nabii alisema anataka amuue mwenyewe! Amri alitolewa. Nilikuwa nimejibanza vizuri, hivyo nikangoja hadi waliponipa migongo ndipo nikaanza kuwacharaza risasi huku nikiwa nimelala chini. Waligeuka haraka na kuanza kujibu lakini kwa sababu ya giza hawakuwa wakijua risasi zilikuwa zinatokea chini nilipokuwa nimelala. Niliwamaliza wote. Una bahati hukuingia haraka maana na wewe ningekucharaza risasi….” Juliana alisema.
“Au labda miye ningekuwahi wewe, unajuaje?” Jacob Matata alisema.
Wote tukacheka.
“Baada ya maelezo ya Japhet, naamini kabisa kuwa Joseph Kony alikuwa kwenye operesheni safisha kundi. Maana ni kwenye hiyo nyumba Kigi na yule askari wa Tanzania mwenye nyota tatu waliuawa. Tumejiridhisha hivyo baada ya kupata taaarifa toka Kigoma kwa watu waliotumwa kwenda kwenye ile nyumba ambayo Japhet ulikuwa umeshikiliwa mateka.” Juliana aliongeza.
“Yes, aliamua kuwamaliza wote. Maana nilipochunguza ile nyumba inaonesha walikuwa wameitwa wote kana kwamba walikuwa na mkutano. Hivyo Joseph Kony ametutumia sisi kuwaangamiza watu aliowaita wasaliti.” Jacob Matata alisema.
“Lakini lazima turejee hapa siku moja kumsaka huyu mtu.” Juliana alisema.
“Tukijaaliwa na inategemea vipaumbele vya ofisi fukuzi.” Jacob Matata alisema.
“Sasa ninyi mlitambuanaje kwenye lile giza?” Niliuliza.
“Tuna ishara zetu za mawasiliano. Nilikuwa na hakika Juliana alikuwa ameshikiliwa kwenye jumba hilo, hivyo hali ilipotulia kabisa nilifanya moja ya ishara zetu. Kama isingejibiwa ningejua kuwa nimeshampoteza. Lakini bahati nzuri ilijibiwa. Nikajua yuko upande gani na kwa ishara hivyo tukaonana.” Jacob Matata alisema.
“Vipi kama ishara hiyo inajulikana na mt…..” Kabla sijamaliza swali langu. Alikuja mtu aliyekuwa amevalia kirubani.
“Bila shaka ni Japhet, Jacob na Juliana?” Mtu huyo aliuliza.
“Ndiyo wenyewe!” Jacob Matata alijibu.
“Ndege iko tayari kwa safari!”
Wote tukamfuata huku Jacob Matata akiwa anasukuma kile kitanda ambacho nilikuwa juu yake.

****

Tuliwasili Dar es salaam majira ya saa kumi na mbili na dakika arobaini na tano asubuhi.
“Vipi unajisikiaje kufika nyumbani salama?” Jacob Matata aliniuliza.
“We acha tu, sasa nahitaji matibabu tu” Nilijibu.”
“Halafu uandike kitabu?” Alisema Jacob Matata huku akicheka.
“Hili suala lenu la kuandika vitabu vya mambo ya kweli silipendi kabisa!” Juliana alisema.
“Nitajitahidi kufanya isiwe kisa cha kweli.” Nilisema.
“Miye itabidi niende Kigoma ili nikahitimishe mambo.” Jacob Matata alisema.
“Kwenye msiba siyo?”
“Haswaa!” Jacob Matata alijibu.
“Hivi una jibu la nani ndani ya ofisi yenu alimtumia Kigi ile taarifa ya kikao chako na Bi Anita?” Niliuliza.
“Hiyo imeshaanza kufanyiwa kazi na itaitwa Operesheni Safisha Nyumba.” Jacob Matata alisema wakati mlango wa ndege ndogo tuliyokuwa tmetumia ukifunguliwa.
“Kitabu cha mkasa huu utakiitaje?” Jacob Matata alihoji.
“PATAPOTEA.” Nilijibu.
“Jina zuri!” Juliana Owima alisema. Akaongeza. “Maana kweli ilikuwa patapotea!”
“Juliana vipi una mwenyeji Dar? Maana baada ya kazi nzito kama hii unahitaji dawa kidogo!” Jacob Matata alisema.
“Ha ha ha haaa!” Nikacheka.
“Mmmh nitaangalia ratiba yangu.” Juliana alijibu.
“Basi poa miye nipo, huwa naweza kuwa mwenyeji mzuri sana.” Jacob Matata alisema akitabasamu.
Wote tukacheka.
Niliona jinsi Jacob Matata alivyomeza funda kubwa la mate alipomtazama Juliana. Nikajua rafiki yangu yuko anayatumikia yale maradhi yake awaonapo warembo aina ya Juliana.
Tulipotoka tu nje, sehemu ya mapokezi ambayo watu huja kupokea wageni wao, nilishangaa kumwona mke wangu akiwa miongoni mwa wasubirio wageni wao. Alipotuona tu, huku mimi nikiwa kwenye kile kitanda cha mataili, aliangua kilio kizito.

MWISHO

____________________________________________

Je umependa simulizi hii?
Je ungependa kupata kitabu kingine chanye simulizi inayofanana na hii?
Basi kwa taarifa yako, mwandishi wa kitabu hiki ana vitabu vingine vizuri sana. Unaweza jipatia nakala yako leo.

Kwa mfano; Kitabu cha SAA 72 ambacho yule mwendawazimu Kumbamasaka Jitu la Watu alikuwa ameking’ang’ania kinapatikana kwa sh10,000 tu, nakushauri ukisome ili ujue nini hasa kimo ndani yake. Unaweza soma vitabu vingine vya namna hii vilivyoandikwa na Japhet Nyang’oro ambavyo ni;

PATASHIKA
MSAKO I
MSAKO II
HEKAHEKA
MDHAMINI
MKONO WA SHETANI
WIMBI LA MAUTI
OPERESHENI PANAMA
SAA 72
ZONU
PLAN B
FUVU NAMBA 53

Vitabu hivi vinapatikana mikoa ifuatayo, mpigie simu au mtumie meseji muuzaji ili akuelekeze mahali alipo ili ukanunue kitabu;

Dar - POSTA - ‭0755454152‬‬
Dar - KARIAKOO- ‭0765227777‬
Dar-Kinondoni - Biafra - ‭065 542 8085‬
Dar - U B U N G O - ‭067 868 3278‬
Dar - Keko - ‭+255 65 638 1406‬
Dar - Ukonga- ‭+255 65 638 1406‬
Arusha -‭ 0757690302‬ au ‭0656744390‬
Mwanza - ‭ ‭0715057315‬ au 0754057315
Moshi - ‭ ‭0754963999
Kilindi- 0713731821
Kasamwa - ‭068 810 2030‬
Dodoma -‭ 0715368220‬
Kibondo - 0655555750
Mpwapwa - 0715368220
Mbeya - 0753914696
Babati ‭0787513647
Maswa - 0766048469
Kasulu- ‬ 0655555750
Bukoba- ‭ 0675 309 841
Namanga- 0757690302
Handeni- 0713731821
Zanzibar - 0652084191
Lindi - 0716725662
Kemondo- 0675 309 841
Kigamboni - 0755454152
Tukuyu- 0753914696
Bariadi- 0766048469
Bunda - 0759142940
Sengerema - ‭068 810 2030‬
Ifakara - 0717708524
Mtwara - 0712962005
Muleba- 0675 309 841
Karatu- 0787513647
Zanzibar - 0652084191
Bihalamulo- ‭068 810 2030
Chunya- ‬ 0753914696
Mutukula - 0675 309 841
Arusha -‭ 0757690302‬
Sumbawanga- 0764123845‬
Moshi - ‭ ‭0754963999‬
Morogoro -‭ ‭ ‭0717708524‬
Longido - 0757690302
Kahama - ‭0753 574 124‬
Chato - ‭068 810 2030‬
KIGOMA - 0655555750
Geita - ‭ ‭068 810 2030
Mbozi - ‬ 0753914696
Rudewa- 0753705024‬
Songea - 0762353918
Tabora - 0689192984
Mpanda - 0764123845‬
Kilombero - 0717708524
Karatu - 0757690302
Dodoma -‭ 0715368220‬
Ushirombo - ‭0753 574 124‬
Musoma - 0759142940
Katoro - ‭068 810 2030‬
Morogoro -‭ ‭0621075891‬
Songwe - 0753914696
Iringa -‭ 0753705024‬
Tunduma - ‭0764123845‬
Kondoa - 0715368220
Ngara - 0655555750
Kagera - ‭0758274733‬
Mvomero - 0717708524
Kakora - ‭068 810 2030‬
Tanga - ‭0713731821‬
Tarime - ‭0759142940
Bahi- ‬ 0715368220
Bukombe - ‭068 810 2030‬
Shinyanga - ‭0766048469‬
Lushoto - 0713731821
Singida - ‭0764 393 260.
M P I G I E MUUZAJI AKUELEKEZE ANAPOUZIA
Ukiuliza sehemu halafu ukaambiwa vimekwisha tafadhali nitaarifu kwa namba 0762204166 ili nifanye utaratibu wa kutuma vingine.
Kama havijafika wilaya yako basi angalia eneo la jirani vilipofika halafu wasiliana na muuzaji ili akutumie kwa basi.


Ili uweze kuendelea kusoma Tuma Tsh. 5000 kwenda namba +255 762 204 166 ili uweze kusoma kitabu PATAPOTEA


RIWAYA ZA KUSISIMUA NA MAFUNZO

SAA 72 ZA KUFA NA KUPONA
SAA 72 ZA KUFA NA KUPONA
SAA 72 ZA KUFA NA KUPONA

Kurejea kwa yule mbabe wa kivita bwana Joseph Katanga huko Congo DRC kunasababisha hali ya wasiwasi mkubwa. ICC wanamwachia wakati ambapo kiongozi wa nchi hiyo anatarajiwa kutangaz

Endelea Kusoma

  • Tsh 5000
PATASHIKA
PATASHIKA
PATASHIKA

Furaha Kijana Maganga, ambaye amebakiza mwezi mmoja kuhitimu mafunzo yake ya Upadri anajikuta yuko katikati ya wimbi zito la maisha pale mtandao wa kijasusi na wahalifu wa kimatai

Endelea Kusoma

  • Tsh 5000
HEKA HEKA
HEKA HEKA
HEKA HEKA

Utangulizi

Endelea Kusoma

  • Tsh 5000
MKONO WA SHETANI
MKONO WA SHETANI
MKONO WA SHETANI

Furaha aliyokuwa nayo mkurugenzi wa shirika la JEPA, Bwana Makia Kimisa kutokana na kupokea hati za msaada wa kipesa wa mamilioni ya dola toka nchi wahisani inatoweka ghafula. Hii

Endelea Kusoma

  • Tsh 5000
MSAKO
MSAKO
MSAKO

Kugundulika kwa gesi katika pwani ya mji wa Mtwara nchini Tanzania kunakuja kama tumaini jipya la kiuchumi kwa serikali na raia wa kawaida. Kila upande unajawa matumaini ya kuishi

Endelea Kusoma

  • Tsh 5000
MSAKO II - The Game
MSAKO II - The Game
MSAKO II - The Game

"JACOB, tumepata taarifa muhimu, zimethibitishwa na shirika la kijasusi la Urusi FSB ambalo zamani lilijulikana kama KGB kuwa, Rais Obama alipoingia madarakani, kwenye ile siku amb

Endelea Kusoma

  • Tsh 5000
NI ZAMU YAKO KUFA
NI ZAMU YAKO KUFA
NI ZAMU YAKO KUFA

Katika kisa hiki safari ya mpelelezi Jacob Matata inaanzia pale anapoitwa na bosi wake na kutumwa Arusha kupeleleza tetesi za kuwepo kwa silaha za hatari katika jiji hilo. Jacob Ma

Endelea Kusoma

  • Tsh 5000
PATAPOTEA
PATAPOTEA
PATAPOTEA

Taarifa ziliponifikia kwanza nilizipuuzia. Niliendelea na shughuli zangu kwani niliziona kuwa ni taarifa za ajabu na zisizo na msingi wowote. Lak

Endelea Kusoma

  • Tsh BURE
MDHAMINI
MDHAMINI
MDHAMINI

Watoto watano wa kiume walifunzwa na kulelewa mfumo wa kuruka na kuwinda kama wana wa Tai. Hii ikawafanya kuondokea kuwa mafundi sana katika masuala ya kupigana na kutumia silaha.

Endelea Kusoma

  • Tsh 5000